Joseph Mketto: Baba alimkimbia mama kwa kutuzaa albino watano!

Na Editha Majura
http://www.mwananchi.co.tz/
TUKIO la Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima kutuliza mzuka wa Mbunge wa Viti Maalum, Al-Shaymaa Kwegyir aliyeangua kilio limeacha simulizi.
Si kawaida ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma kushuhudia vilio, lakini kwanini Mbunge Al-Shaymaa Kwegyir (CCM) aliangua kilio?
Huku akivuta hatua kutoka nje ya ukumbi wa bunge, mbunge huyo aliendelea kulia na kufuta machozi aliyoshindwa kuyazuia.
Kisa? Ni baada ya kushindwa kustahimili mzigo wa uchungu alioubeba moyoni mwake, kufuatia ukatili na mauaji dhidi ya wenye ulemavu wa ngozi, (albino) yanayoendelea nchini huku kasi ya wanaohusika na matukio hayo kutiwa mbaroni ili wahukumiwe kwa mujibu wa sheria ikisuasua.
Kwa tukio hilo, Kwegyir ambaye pia ni mlemavu wa ngozi amewaambukiza Watanzania wenye utu simanzi ikitarajiwa kuonekana mabadiliko katika namna ya kudhibiti mauaji hayo kwa kuwepo ongezeko la wanaohusika kufichuliwa na kutiwa nguvuni.
Mfano halisi wa mateso wanayopata walemavu hao nchini ni maisha ya ukimbizi wanayoishi Omari Mketo na Joseph Mketo (21) wazaliwa wa baba na mama mmoja.
Ni wazaliwa wa Kilwa Kipatimu mkoani Lindi, lakini kwa sasa wanaishi Dar es Salaam eneo la Mtoni Kijichi walikohamia wakitokea Kanda ya Ziwa, Mwanza ambako alikwenda baada ya baba yao kumwacha mama yao kwa sababu alizaa kwa mfululizo watoto watano wenye ulemavu huo.
“Tumezaliwa saba, watano tukiwa wenye ulemavu wa ngozi, lakini mmoja wetu alifariki tumebaki wanne, wawili wa kike na sisi ni wa kiume,” anaeeleza Omari anaeleza na kisha kuendelea:
“Mtoto wa kwanza na wa pili hawana ulemavu huu, lakini kuanzia wa tatu mpaka wa saba ambaye ni Joseph aliyezaliwa mwaka 1991 tuna ulemavu na ndiyo sababu mwaka 1996 baba alimwacha mama, nasi tukalazimika kwenda kuishi naye naye nyumbani kwao Mwanza.”
Joseph anasema, kutokana na ugumu wa maisha pamoja na hofu kwamba hata baba yao anaweza kuwasaliti kwa sababu haikuwa na kificho kwamba aliwachukia, waliamua kutorokea Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza huku wakimwachia mama yao huzuni isiyoelezeka.
Anasema wanashukuru Mungu, dada zao wenye ulemavu wameolewa mmoja anaishi Mbagala na mwingine Chanika, “sisi bado tunaishi kwa kuhamahama tukihofia kuuawa huku tubuni na kutekeleza majukumu yanayotuwezesha kupata mahitaji muhimu katika maisha yetu ya kila siku.”
Wakiwa Kanda ya Ziwa, Joseph anasema walinunua ndizi sehemu mbalimbali mkoani Kagera na kuzisafirisha mpaka Mwanza ambapo waliziuza.
Anasema kazi hiyo iliwawezesha kujipatia mahitaji yao ya kila siku ikiwamo dawa wanazotumia kuzuia magonjwa mbalimbali yanayowaandama kutokana na ulemavu wao, hususan magonjwa ya ngozi.
Mtoto wa baba yao mdogo, Salumu Mzome ambaye pia ni mlemavu wa ngozi aliungana nao mkoani Mwanza ambako kutokana na biashara waliyokuwa wakifanya maisha yalikuwa mazuri.
Hata hivyo, walilazimika kuendeleza utaratibu wa kuhamisha makazi ambapo sasa yapata miezi Minane tangu walipohamishia makazi yao jijini Dar es Salaam, Mtoni Kijichi.
“Ingawa hatujakumbwa na jaribio la kuuawa matukio alinayotokea mara kwa mara Tarime, Tabora, Shinyanga na maneno ya watu kila walipotuona kama vile ‘dili hizo’ tukaona umuhimu wa kuhamisha makazi,” Joseph anabainisha
Kutokana na Dar es Salaam kuwapo Juakali, wanashindwa kufanya kazi ambazo hufanywa na watu wengi wenye kipato cha chini ili kujikimu kimaisha, kwa sababu ya kuepuka miale ya Jua ambayo huathiri ngozi na hatimaye kuugua ugonjwa wa saratani.
Wamebuni mradi wa intaneti ambamo pia watauza vifaa mbalimbali vya ofisini na shuleni (stationery) wakiamini kuwa wakifanikiwa katika hilo, watamudu kujipatia mahitaji yao muhimu katika maisha yao ya kila siku na ngozi zao kubaki salama bila hatari ya saratani.
Ili wafanikiwe katika hilo, vijana hao wanahitaji ufadhili kutoka kwa watu binafsi, taasisi binafsi, za serikali, za kidini na mashirika ya umma. Mahitaji wanayoainisha kuwa ni muhimu katika kufanikisha mpango huo ni Sh 5,150,000 (milioni tano na laki moja na nusu)
Wanahitaji kompyuta nne zinazogharimu Sh 1,400,000, mashine ya kurudufia, Sh 1,000,000, mashine ya lamination Sh 100,000  na gharama za uendeshaji Sh 1,000,000 Pango, Sh 720,000, feni Sh 150, 000 Meza mbili Sh 400,000, Viti vya plastiki Sh 60,000 mashine ya binding Sh. 120,000 na printer ya Sh 200,000
Wao wana matumaini makubwa kwamba, Watanzania wengi wenye imani na wanaoguswa na hali ngumu ya maisha ikiwamo ya kiusalama inayowakabili, watajitolea kuwawezesha kufanikisha mpango wao huo ambao pamoja na kwamba utawasaidia pia utatoa mwanya kwa baadhi ya vijana wasiokuwa walemavu kupata ajira.
Wanamwomba yeyote mwenye nia ya kuwachangia kwa kiwango chochote, kuwasilisha mchango wake kwa kupitia katika Akaunti yenye nambari 054206006477 NBC au kupitia ofisi za gazeti la Mwananchi, Tabata Relini.

Post a Comment

أحدث أقدم