HARAKATI za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
mwaka 2015 umeanza kuwatesa viongozi wa vyama vya siasa ambapo safari
hii, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), Zitto Kabwe, amesema kama
akiandikiwa kuwa rais hakuna wa kumzuia.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alijitapa kuwa kama
urais upo, utakuja tu, kwani ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa
Amiri Jeshi Mkuu.
Zitto ameibuka na kuzungumzia sakata la urais ikiwa ni siku moja tu
imepita baada ya wabunge wenzake kulalamika na kukanusha taarifa za
kumpigia debe kwa ajili ya urais mwaka 2015.
Wabunge hao, Halima Mdee (Kawe) na Joshua Nassari (Arumeru
Mashariki), waliandika barua za kulalamikia habari iliyochapishwa na
gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima), wakidai liliwalisha maneno
kuwa walimpigia debe Zitto wakiwa mkoani Kigoma kwamba anapaswa kuwa
rais mwaka 2015.
Akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya
bajeti ya Wizara ya Mawasilaino, Sayansi na Teknolojia jana mjini hapa,
Zitto alitumia muda mfupi kufafanua sakata hilo lililozagaa kwenye
vyombo kadhaa vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.
“Tamasha letu la wasanii la Kigoma limeleta maneno maneno…lakini
napenda kusema kuwa urais kama upo utakuja tu. Sina mashaka hata kidogo
kwamba uwezo, uadilifu na uzalendo wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ninao,”
alisema Zitto na kushangiliwa na wabunge wenzake.
Mjadala huo ulichukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii juzi ambapo
baadhi ya watu walionekana kumlaumu Zitto, wakimhusisha na habari hiyo
kuwa aliitengeneza mwenyewe kama sehemu ya kujiandalia mazingira hayo.
Zitto ambaye amekuwa akiandamwa mara kadhaa na wanasiasa ndani na nje
ya chama chake, baadhi wakimtuhumu kuwa mamluki na wengine wakimwelezea
kuwa ni mwanasiasa mwenye malengo makubwa hapo baadaye, alifafanua zaidi
suala hilo kwenye taarifa yake kwa kusema:
“Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na
habari yenye kusomeka: ‘Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015?.
Habari hii imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala
umekuzwa zaidi baada ya wabunge, Halima Mdee na Joshua Nassari kukanusha
maneno waliyonukuliwa kusema. Napenda kusema masuala yafuatayo:
“Moja, waheshimiwa wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola,
Esther Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David
Kafulila walihudhuria tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa
na Mratibu wa kundi hilo, Mwasiti Almasi.
“Wabunge wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwamo Joseph
Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba.
Wabunge hawa hawakualikwa na mimi na wala sikufanya mazungumzo nao
yoyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana nini cha kuzungumza au
hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa.
“Waheshimiwa wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza.
Wabunge waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua
Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola.
“Hotuba za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na
video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary
ya tamasha lile la kihistoria.
“Pili, sikuhusika kwa namna yoyote ile na kuandikwa kwa habari hii
iliyozusha mjadala. Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa, maana
katika ziara ile sikuita mwandishi hata mmoja, maana nilitaka liwe tukio
la Kigoma tu.
“Kama mwandishi kaandika mambo ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi
itaonekana kwenye video hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao
nini walichosema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema waliyoyasema.
Nisingependa kuhusishwa kwa njia yoyote ile na matamshi yao, habari
iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio
utasimama.
“Suala la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya
kujadili kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya
urais yanapotajwa zinashangaza sana.
“Chama changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea
urais. Hivi sasa chama hakina mgombea urais mpaka hapo mchakato
utakapotangazwa, ambapo wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha
bendera ya chama. Mwanachama wa chama chetu atakaye kubalika na jamii na
wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa
hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili.
“Mzee Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema
‘weka akiba’ si akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya
maneno. Tusimalize yote.”
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili mjini hapa jana mara baada ya
Bunge kuahirishwa kwa ajili ya mapumziko ya mchana, Zitto alikanusha
tuhuma hizo zinazomhusisha kuandaa habari hiyo akisema ni matusi kwa
tasnia ya habari, hivyo kuvitaka vyombo vya habari kutowaendekeza
wanasiasa wanaotukana waandishi na vyombo vyao.
“Ni upuuzi kudhani kwamba mimi naweza kuandaa habari kwenye gazeti
hilo…nimeshangaa na wewe unaweza kuniuliza jambo hili…unaliamini?”
alihoji Zitto.
Kuhusu habari hiyo inayolalamikiwa na wabunge wenzake kuwa
ilipotoshwa, alisema kwamba haoni ubaya kwenye habari husika akidai hata
hivyo mengi yaliachwa kuliko kuongezwa chumvi. “Hakuna aliyenukuliwa
kwa ambalo hakusema. Tamasha zima limerekodiwa kwenye video”.
Kwa muda sasa kumekuwepo na mjadala juu za Zitto kuhusu kauli yake
kwamba anautaka urais, jambo liliotafsiriwa kuwa ni mikakati ya kutaka
kukivuruga chama chake kwa kikigawa kimakundi lakini Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amekuwa akisema kila wakati kuwa ajenda yao
kwa wakati huu si kujadili nani anafaa kugombea urais 2015 badala yake
wanajikita kutatua kero za wananchi.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق