WANACHAMA WAKUMBUSHWA KULIPIA KADI:- SIMBA SC
MAANDALIZI
ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa Simba SC yanaendelea vizuri na utafanyika
kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu kwenye ukumbi wa Polisi Oysterbay,
Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Simba SC, Evodius Mtawala amesema kwamba
uongozi unarudia kuwakumbusha wanachama wote, ambao hawajalipia ada zao
za uanachama kufanya hivyo mapema ili washiriki Mkutano huo.
“Tunarudia
kuwakumbusha wanachama wetu, ambao hawajalipia ada zao za uanachama
kufanya hivyo mara moja, ili wapate haki ya kushiriki Mkutano
Mkuu,”alisema Mtawala.
Wiki
iliyopoita, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ilikabidhi hundi ya Sh.
Milioni 20 kwa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, kwa ajili ya Mkutano
huo.
Akikabidhi
mfano wa hundi hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geofffrey Nyange
‘Kaburu’, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inayozalishwa na
TBL, George Kavishe alisema kwamba anawatakia mafanikio Simba SC katika
mkutano wao huo Mkuu.
Kwa
upande wake, Kaburu au Perez ambaye klabu yake, inadhaminiwa na
Kilimanjaro Beer, alisema kwamba anashukuru kwa fedha hizo na akawataka
wanachama wote hai wa Simba kuhudhuria mkutano huo siku hiyo kujadili
maendeleo ya klabu.
Kaburu
alisema kwamba, katika siku hiyo ya Mkutano watazindua Wiki ya Simba SC
na jamii, ambayo itahusu wachezaji, viongozi na walimu wa timu hiyo
kufanya ziara sehemu mbalimbali za kijamii, kama hospitali, vituo vya
watoto wa yatima, shule za msingi na kiwanda cha TBL, wadhamini wao
wakuu.
Kaburu
pia alikumbushia kuhusu tamasha la kila mwaka la Simba SC, Simba Day,
ambalo na mwaka huu tena litafanyika Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. “Maandalizi ya Simba Day yamekwishaanza na yanaendelea vizuri na
kwa sasa kocha yupo kwenye harakati za kuboresha timu,”alisema Kaburu.
Kwa
upande wake, Kavishe aliahidi siku ya Simba Day wataikabidhi Simba SC
basi lake jipya kubwa, ambalo kwa sasa lipo kwenye hatua za mwishoni za
matengenezo.
RATIBA YA WIKI YA SIMBA NA JAMII:
Agosti 5, 2012: Mkutano Mkuu wa mwaka Simba SC (Polisi Oystrebay)
Agosti 6, 2012: Kutembelea watoto yatima Maungu Orphanage Center, K’ndoni Mkwajuni
Agosti 7, 2012: Kutembelea wagonjwa Mwananyamala hospitali
Agosti 8, 2012: Simba Day (Uwanja wa Taifa, burudani na mechi)
Agosti 9, 2012: Kutembelea shule ya msingi Mgulani kuhamasisha michezo mashuleni
Agosti 10, 2012: Kutembelea kiwanda cha TBL Ilala.
إرسال تعليق