AKUFFO AZIDI KUTISHA, NGASSA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO MSIMBAZI
Akuffo akishangilia bao dhidi ya Mathare Jumapili. Leo amefunga tena. |
SIMBA imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 jioni hii
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha dhidi ya wenyeji JKT Oljoro
katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza katikati ya mwezi ujao.
Mshambuliaji kutoka Stella Abidjan ya Ivory Coast,
Mghana Daniel Akuffo ameendelea kutunisha akaunti yake ya mabao Msimbazi, akifikisha
mawili wakati Mrisho Khalfan Ngassa amefungua rasmi akaunti yake ya mabao leo
katika mchezo huo.
Akuffo aliifungia bao la kwanza Simba SC dakika ya
25, akiunganisha pasi ya Ngassa- hilo likiwa bao lake la pili tangu aanze
kuichezea timu hiyo mwezi huu, baada ya awali kufunga kwenye Uwanja huo huo
Jumapili dhidi ya Mathare United ya Kenya katika ushindi kama wa leo, 2-1.
Ngassa alifungua akaunti yake ya mabao Simba SC
dakika ya 76 akiunganisha pasi ya Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ na Oljoro ilipata
bao la kufutia machozi dakika ya 89 kwa penalti iliyotiwa nyavuni na Markus
Mpangala baada ya Paschal Ochieng kumuangusha mchezaji huyo wa timu ya Maafande
wa Jeshi la Kujenga Taifa kwenye eneo la hatari.
Simba itakuwa na mechi nyingine ya kujipima nguvu
Jumapili, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam dhidi ya Coastal Union ya Tanga,
kabla ya kumenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 8, mwaka huu,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
إرسال تعليق