SIMBA SC KUANZA KUTETEA KOMBE(LIGI KUU) SEPTEMBA 15

SIMBA SC KUANZA KUTETEA KOMBE(LIGI KUU) SEPTEMBA 15

Wachezaji wa Simba SC; Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu


LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuanza Septemba 15, mwaka huu.
Kikao cha pamoja baina ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika jana kimefikia uamuzi ligi hiyo ambayo kwa kawaida huanza Septemba 1, sasa itaanza wiki ya pili ya Septemba.
Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF, imesema;
1.   Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa, yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.

2.   Mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.

3.   Kukamilika kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na masuala mengine muhimu.

4.   Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu

5.   Kutokana na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku itakayotangazwa baadaye.

6.   Kuhusu chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho

Wakati huo huo: TFF imeandaa semina kwa ajili ya makamisaa watathmini wa marefa wa daraja la kwanza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao.
Kwa upande wa makamisaa na watathmini wa marefa, semina itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 29-30 mwaka huu. Washiriki wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri, malazi na chakula wawapo kwenye semina.
Semina kwa waamuzi itafanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza kuanzia Agosti 31- Septemba 2 mwaka huu. Pia nao watajigharamia kwa kila tu. Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni ambao hawakushiriki ile iliyofanyika Juni mwaka huu na wale walioshiriki lakini hawakufaulu mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test).
Marefa wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Kimataifa (FIFA) hawashiriki kwa vile wao wamekukuwa wakishiriki semina zao zinazoandaliwa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.

Post a Comment

Previous Post Next Post