STEWART AFUKUZWA KAZI AZAM - KISA NGASA
Stewrt Hall; Ngassa amemponza kupoteza ajira Azam |
STEWART Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana
amefukuzwa rasmi katika klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya
Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya
fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Habari ambazo zimezipata kutoka ndani
ya Azam, zimesema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo
na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa
anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya
Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na
kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na
kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea
Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu
kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya
kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Kwa sasa mazungumzo yanaendelea kati ya Yanga na
Azam juu ya Ngassa ili mchezaji huyo arejee Jangwani, lakini wakati huo huo,
Simba nao wameweka dau la Sh. Milioni 25 katika 50 zinazotakiwa na Azam ili
kumuuza mchezaji huyo.
Mbali na Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ pia
yuko katika wakati mgumu na jana inadaiwa alionekana akilia wakati anazungumza na
kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi kosa lake.
Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana
ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ jana hajafanya mazoezi na leo pia, naye pia
akituhumiwa kucheza kinazi katika mechi dhidi ya Yanga.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne
kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin,
Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji
na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita
Chanzo:- Bin Zubery
إرسال تعليق