THIERRY HENRY - ARSENAL BILA VAN PERSIE INAWEZA

MKONGWE Thierry Henry, amesisitiza kuwa Arsenal inaweza kuziba vizuri pengo la mshambuliaji wake,  Robin van Persie iwapo ataondoka Emirates.
Bosi, Arsene Wenger anatarajia kufanya mazungumzo na Van Persie wiki hii, lakini nyota huyo wa Uholanzi bado dhamira yake ya kuondoka iko palepale.
Klabu za Manchester City, Manchester United na Juventus zote zinahitaji kuinasa saini ya Persie, mfungaji bora wa Ligi ya Barclays msimu uliopita.
Henry, aliyecheza Arsenal kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka nane na kuondoka mwaka 2007 kabla ya kurudi kwa mkopo Januari mwaka huu, amesema kuna kila sababu ya Arsenal kubaki imara hata kama Robin ataamua kuondoka.
"Tunatumaini atabaki, ndivyo ilivyo," alisema Henry, raia wa Ufaransa."Sifahamu nini hasa kinachoendelea, lakini nikiwa kama shabiki wa Arsenal, ningependa kumwona anabaki Emirates."
"Yeye bado kwa sasa ni mchezaji wa Arsenal, na bosi ndiye anayesimamia suala lake. Napenda kuiona Arsenal ikifanya vizuri. Robin atafanya atakachoweza na sisi tuko tayari kusubiri kuona.
"Nilipoondoka kila mmoja alilia, lakini mwaka mmoja baadaye Arsenal ilikuwa mbele kwa tofauti ya pointi nane kwenye msimamo. "Watu wanakuja na kuondoka, maisha ndivyo yalivyo."
Henry amesema angependa kumwaona kiungo wa kimataifa wa Arsenal na England, Jack Wilshere anayesumbuliwa na matatizo ya kifundo cha mguu na goti anapata nafuu mapema.
Wilshere anatarajia kurejea uwanjani Oktoba baada ya kutumia msimu mzima uliomalizika akipatiwa matibabu.

Post a Comment

أحدث أقدم