WAKATI mgomo wa walimu ukiingia siku ya tano leo, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa madai yao hayatekelezeki.
Rais aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Madai ambayo walimu wamekuwa wakiitaka serikali kuyatafutia ufumbuzi
ni pamoja na ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya
kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55, asilimia 50 kwa walimu wa
masomo ya Sanaa na asilimia 30 posho kwa walimu wanaoishi katika
mazingira magumu.
Katika hilo rais alisema: “Mgomo si jambo zuri na linanisononesha
lakini sitaki kuzungumzia sana hili kwa sababu kesho (leo) mahakama
itatoa uamuzi juu ya kesi hiyo.
“Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali sana,
tunawathamini, tunatambua mchango wao hata mimi ninayeongea hapa ni kazi
ya walimu… kwa hiyo hatuwezi kuwapuuza,” alisema Kikwete.
Akifafanua kwa nini madai hayo ya walimu hayatekelezeki, Rais Kikwete alisema ni makubwa na yanazidi uwezo wa serikali.
Alisema endapo watakubali kuyatekeleza madai ya walimu, serikali
itatumia shilingi trilioni 6.574 (karibu trilioni 7) kwa ajili ya
kulipana mishahara wakati uwezo wa serikali kukusanya mapato ni trilioni
nane.
Hivyo alisema haiwezekani mapato yote ambayo serikali inakusanya yakatumika kwenye kulipana mishahara.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, endapo serikali itaamua kulipa mishahara
kwa kiwango hicho kuna hatari ya mapato yote yakatumika huko na kuacha
miradi mingine ya maendeleo pamoja na huduma za kijamii.
“Tukifanya hivyo, utatokea mgomo wa wananchi…hawatapata maji, dawa,
barabara na huduma nyingine…tufike mahali tuseme kuna ukomo wa
kulipana,” alisema Kikwete.
Kikwete alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa walimu walio tayari
kufundisha kuendelea kufanya hivyo na kuonya baadhi ya walimu
wanaowatisha wenzao walio radhi kufanya kazi.
Mbali na hilo, Rais Kikwete alionekana kukerwa na tabia ya walimu
waliogoma kuwatumia watoto wadogo kuandamana na kusema kuwa: “ Jamani
hakuna mtoto mdogo hapa sote tuna akili, hivi ni mtoto gani anaweza
kuandamana na kwenda kulala barabarani yeye mwenyewe, hili si jambo
jema, wadai haki yao lakini watoto wawaache”.
Rais Kikwete pia alisema wakati wote wamekuwa wakiyafanyia kazi madai
ya walimu pamoja na kutekeleza haki zao ikiwa ni pamoja na kukaa pamoja
katika meza ya mazungumzo.
Hata hivyo alionekana kusikitishwa na kitendo cha Chama cha Walimu
Tanzania (CWT) kumuandikia barua siku ya Ijumaa na kuikabidhi kwa
Katibu Kiongozi wakati wakijua kwamba Jumamosi na Jumapili hakuna kazi.
“Jamani hii ni sawa na yule mtu ambaye anakupeleka polisi siku ya
Ijumaa wakati anajua Jumamosi na Jumapili huwezi kutoka mpaka Jumatatu
wakati wa siku ya kazi,” alitania na kuongeza kuwa: “Narudia kusema tena
hatuwapuuzi walimu ila madai haya ni magumu, tuendelee kuzungumza,
turudi kwenye meza ya mazungumzo.”
Julai 29, mwaka huu, CWT walitangaza kuanza mgomo usio na kikomo,
hatua ambayo ilikuja ikiwa ni siku moja baada ya serikali kutangaza kuwa
mgomo huo ni batili.
Tayari mgomo huo umesababisha athari kubwa nchi nzima, baada ya wanafunzi kukosa masomo kwa takriban siku tano sasa.
Leo Mahakama Kuu kitengo cha Kazi itatoa uamuzi kuhusu kesi iliyofunguliwa na serikali kuzuia mgomo huo wa walimu.
Serikali ilifungua kesi hiyo kupinga mgomo huo ulioitishwa na CWT, kwa madai kuwa ni batili kwa sababu ulikiuka sheria.
Katika kesi hiyo, serikali inadai kuwa CWT ilitumia sheria ya utatuzi
wa migogoro ya wafanyakazi wa serikali namba sita, kifungu cha 26,
inayotumiwa na wafanyakazi wote wa umma na wengine badala ya kutumia
sheria ya majadiliano ya pamoja ya utumishi wa umma ya mwaka 2003.
Pia inadai kuwa katika sheria waliyotumia inataka kutoa notisi ya saa
48 badala ya ile ya watumishi wa umma ambayo inawahusu walimu ambao ni
kundi maalumu, ambayo ingetoa notisi ya siku 60.
Mgogoro mwingine kati ya CWT na serikali umedumu kwa zaidi ya miaka
mitano sasa, ambapo licha ya ahadi ya kulipwa madai hayo, fedha zimekuwa
hazikidhi ukubwa wa tatizo na kusababisha madeni kurundikana
إرسال تعليق