VYOMBO VYA HABARI VIDHIBITI KAZI CHAFU ZA WASANII - BASATA.

VYOMBO VYA HABARI VIDHIBITI KAZI CHAFU ZA WASANII - BASATA.

Mdau wa Sanaa na mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime (kushoto) akisistiza jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari Godfrey Mungereza.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari BASATA Bw. Lebejo akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu sekta ya muziki nchini.
Rais wa Shindano la Urembo la Miss Utalii Gideon Chipungahelo naye hakuwa nyuma katika kuchangia juu ya tasnia ya muziki nchini. Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti kazi za Sanaa zisizo na maadili kabla ya kwenda hewani ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua wakati akiiahirisha programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa, wakati Baraza limefikia hatua nzuri ya kudhibiti hali hiyo, wadau wakuu katika kumaliza tatizo hili ni wasanii wanaotakiwa kutunga kazi bora na zenye maadili huku vyombo vya habari vikiwa na wajibu wa kuchuja kila kazi ya Sanaa inayopokelewa kabla ya kuirusha hewani.

“Basata imeshaviandikia vyombo vya habari kuvielekeza kuwa na kamati za ndani za kudhibiti maadili kwenye kazi za sanaa kabla ya hazijaenda hewani. Hili ni muhimu sana katika kujenga maadili ya mtanzania” alisisitiza Shalua.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini na hatua zake mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime alisema kuwa, kumekuwa na changamoto mbalimbali miongoni mwa wasanii wa fani hiyo hali inayoufanya usifike mbali.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na wasanii kutozingatia sheria ya hakimiliki na hakishiriki iliyopo, kuiga midundo ya muziki kutoka nje hali inayosababisha kutokuwepo kwa muziki wenye utambulisho wa Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika hususan Afrika Kusini.

“Tatizo kubwa ni wasanii wetu kuiga miziki na hata tamaduni za kigeni, hatuwezi kuandaa kazi za Sanaa kufurahisha wazungu au watu kutoka nje tu, tutapotea” alionya Kitime.

Kwa upande wake Rais wa Shindano la ulimbwende la Utalii (Miss Utalii) Gideon Chipungahelo alisema kuwa, kihistoria wanamuziki wetu ukianza na wakongwe waliopo walijikita katika kuiga miziki ya Zaire hivyo kinachofanywa na wasanii wetu wa sasa ni mwendelezo tu.

“Ni wazi kazi iliyopo sasa ni kuwafanya wasanii kujikita katika utajiri mwingi wa makabila yenye midundo mbalimbali tuliojaaliwa. Hapa ndipo tunapaswa kusisitiza” alishauri Chipungajelo.

Post a Comment

أحدث أقدم