
MAMBO vipi watu wangu? Natumaini kwamba mambo ni freshi na mnaendelea
vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi ni mzima bukheri wa afya na
tunakutana tena kupitia safu hii lengo likiwa ni lile lile la kuwekana
sawa katika masuala kadhaa yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Wiki
iliyopita niliandika mada iliyokuwa inaeleza jinsi wapenzi wanavyoweza
kujifunza kutokana na kifo cha msanii maarufu, Steven Kanumba. Ni
matumaini yangu mmejifunza kitu na kubadilika itakuwa ni jambo jema
kwenu.
Baada ya utangulizi huo, nigeukie sasa kwenye mada yangu ya
wiki hii. Wakati flani huwa najiuliza kwa nini tunakuwa na wapenzi, kwa
nini mapenzi yakawepo? Kwa nini tunaoa ama kuolewa? Kwa nini baadhi ya
watu huamua kujinyonga baada ya kuachwa na wapenzi wao? Kwa nini mapenzi
yamekuwa sehemu ya maisha yetu?
Kwa nini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi na kupata majibu mengi pia.
Kwa
vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika
maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu
ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa
mwingine.
Mapenzi hayo hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia
sawa za mapenzi. Elewa kwamba kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye
hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa
mapenzi. Kama ndivyo, kwa nini ukubaliane na hali hiyo ambayo unaweza
kuepukana nayo?
Unadhani hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kukupenda
kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti
na ilivyo sasa? Inawezekana! Huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu
ambaye unaona wazi kwamba hampendi.
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu,
kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni
wazi maisha yako yatakuwa yenye furaha isiyosimulika. Mapenzi yapo hivyo
na kama ukienda kinyume chake lazima utaumia.
Wakati mwingine
unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa
wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka
wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe?
Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake na hao hao ndiyo wamekuwa
wakiongoza kwa kutoa machozi pale wanapotendwa.
Anatokea mwanaume
anampenda sana, anapomtongoza anajikuta hampendi, anachokifanya ni
kumwambia kuwa atamjibu baadaye. Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili
ya kujipanga na kufikiria. Mapenzi hayafikiriwi kiivyo ndugu zangu.
Kama
mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako utakuambia bila
kukuficha na utabaki wewe tu kufanya maamuzi sahihi. Hii ina maana kuwa
atakapokuambia anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha
kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana na lazima
utamkaribisha.
Tatizo lilipo
Baadhi ya wasichana wakitongozwa na mwanaume ambaye
anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha,
huamua kumkubalia kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.
Hufanya
hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na
mwanaume huyo kitu ambacho hakipo katika ulimwengu wa mapenzi.
“Fedha
anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitakwenda naye hivyo hivyo
mwisho wa siku penzi litajijenga lenyewe taratibu,” baadhi ya wasichana
huwaza hivyo. Baada ya wazo hilo kuingia akilini mwake, huwa hana muda
wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika
ndoa.
Madhara yake
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na
mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la
dhati ambalo ndiyo msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na
wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote. Kinyume cha hivyo,
furaha utakuwa ukiisikia kwenye bomba tu.
Madhara makubwa zaidi ni
pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa
ajili ya kusaka penzi la dhati. Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta
magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, lazima utafukuzwa nyumbani
kwa mwanaume huyo na kama ana hasira, anaweza kukuua.
JAMBO LA MSINGI
Ushauri kwangu ni kwamba, kamwe usijaribu kuingia
katika mkumbo huu wa watu wanaoingia kwenye uhusiano na watu ambao
hawajawapenda.
Maisha yenyewe ni mafupi hivyo kuwa makini, fanya
maamuzi sahihi yahusuyo maisha yako ya kimapenzi kwa umakini wa hali ya
juu ili usije ukawa mmoja kati ya wanaolizwa na mapenzi na kuishia
kujuta kila siku.
Story na:- http://ujanatz.blogspot.com
إرسال تعليق