Na: Daniel Mjema, Mwanga, MWANANCHI.
WAZIRI
Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amewataka waumini wa madhehebu yote
nchini kuonyesha mshikamano katika ujenzi wa shule nchini bila kujali
shule inayojengwa ni ya Wakristo au Waislam.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alitoa kauli hiyo jana wilayani Mwanga katika harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya Kiislamu ya Lambo iliyopo kata ya Shighatini.
Lowassa alitumia fursa hiyo kusema kuwa Wilaya ya Mwanga ni ngome ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na kwamba kwa kusema hivyo hakipigii debe chama chake bali huo ndio ukweli.
Katika tamasha la harambee hiyo iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, Masheikh na Wachungaji wa madhehebu mbalimbali, Lowassa alichangia Sh10 milioni.
“Mwanga ni nguzo yetu ya CCM na wala hili sio jambo la siri…Namfahamu Profesa Maghembe, katika kura hapa hamkukosea hili ni jembe…ni kiongozi hodari na mchapa kazi,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye anatajwa kuw amiongoni mwa watakaoingia katika kinyang’anyiro cha kugombea Urais mwaka 2015, alimpongeza Profesa Maghembe pamoja na mtangulizi wake, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya kuwa wana mipango mizuri ya maendeleo.
Akizungumzia kujitoa kwake kuchangia shughuli za kijamii, Lowassa alisema japokuwa ana mialiko mingi lakini suala la kuitwa Mwanga kuchangia ujenzi wa sekondari limemfurahisha sana.
“Watu huwa wanaogopa kuchangia lakini ni lazima wanadamu wafahamu kuwa vyote vilivyomo duniani ni vya mwenyezi Mungu…tushikamane wakristo na waislamu tujenge shule,” alisema.
Lowassa alisema suala la ujenzi wa shule za msingi na sekondari ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na Watanzania akisema wanaodai elimu ni ghali basi wajaribu ujinga.
“Kuna maneno yanasemwa kuwa Waislamu huwa hawajengi shule bali wanajenga misikiti mikubwa lakini nyinyi hapa hapa Mwanga mmefuta dhana hiyo na ni mfano wa kuigwa,” alisema.
Awali, Profesa Maghembe alisema amezunguka kwa marafiki zake ambao walichangia Sh25 milioni kabla ya jana, na kabla ya kuanza harambee alikuwa amepata michango mingine ya Sh19.5 milioni.
Katika harambee hiyo, Profesa Maghembe alichangia Sh3 milioni wakati mfanyabiashara Seleman Mfinanga akichangia Sh1 milioni na hadi mchana bado harambee hiyo ilikuwa ikiendelea.
Akisoma risala kwa Lowassa, mjumbe wa Halmashauri ya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), linalomiki shule hiyo, Sadik Ramadhan, alisema shule hiyo itagharimu Sh2 bilioni hadi kukamilika. Alifafanua kuwa harambee ya jana ililenga kukusanya Sh255 milioni kwa ajili ya kujenga jengo la utawala, maabara na mabweni mawili lakini kwa siku ya jana zilihitajika Sh150 milioni.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
إرسال تعليق