![Untitled](http://dewjiblog.com/wp-content/uploads/2012/10/Untitled3.jpg)
Hamdu
zote ni za Allah, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehema za Allah na
salamu Zake zimfikie Mtume Mtukufu Mwaminifu na Aali zake watoharifu,
wateule na masahaba wake wema.
Msimu
wa Hija uliojaa rehema na baraka umewadia na kwa mara nyingine na watu
waliofanikiwa kwenda katika miadi hii iliyojaa nuru, wamo katika
kumiminiwa baraka za Mwenyezi Mungu. Hapa, ninatoa mwito kwenu nyote
mahujaji kutumia fursa ya kuwepo mahala hapa na kuwemo katika wakati
huu, kujiimarisha kimaanawi na kimaada. Hapa, Waislamu wanaume kwa
wanawake wanaitikia labeka mlingano wa Mola wao Mkubwa wa kujipamba kwa
sifa na matendo mema; kwa nyoyo na midomo yao.
Hapa
watu wote wanapata fursa ya kufanya mazoezi ya kudumisha udugu,
mshikamano na kujiepusha na maasi. Hii ni kambi ya malezi na mafunzo, ni
maonyesho ya umoja, adhama na jinsi umma wa Uislamu ulivyokusanya
pamoja sura za watu tofauti, ni kambi ya kupambana na shetani na
mataghuti. Hapa Mwenyezi Mungu Mwingi wa hekima na Muweza amepafanya
kuwa ni mahala ambapo waumini waweze kuona manufaa yao ndani yake.
Tutakapofungua macho yetu ya busara na ibra basi ahadi ya mbinguni
itaweza kuenea katika maisha yetu yote; ya kila mmoja wetu na ya jamii
nzima.
Sifa
za kipekee za amali za Hija ni kule kuchanganya kwake dunia na Akhera
na kuchanganya kwake masuala ya watu binafsi na ya kijamii. Al Kaaba
isiyo na doa na iliyotukuka; kutufu miili na nyoyo za watu katika
mhimili mmoja madhubuti na wa milele; amali ya Sai (baina ya Safa na
Marwa) na kufanya jitihada za mfululizo na za mpangilio mmoja kutoka
nukta ya kuanzia hadi nukta ya kuishia; kugura mahujaji wote kuelekea
kwenye nyuga za ufufuo za Arafa na Mash’ar na shauku na uhudhurishaji wa
moyo katika Mash’ar na maqam hayo adhimu, huleta unyofu na hali mpya,
mapambano ya pamoja ya watu wote ya kukabiliana na vielelezo vya
shetani, na hatimaye kwa pamoja na kutoka kila mahala na kila rangi na
kila namna; wote wanashiriki kwa pamoja katika amali hizo tukufu
zilizojaa neema na utukufu na zilizojaa maana na ishara za uongofu. Sifa
za kipekee za faradhi hii zimejaa maana na madhumuni.
Ni
amali kama hii ndiyo ambayo inauunganisha moyo na kumkumbuka Mwenyezi
Mungu, na kuujaza nuru na kuunawirisha upweke wa moyo wa mwanadamu kwa
imani na taqwa na wakati huo huo kumvua mwanadamu kutokana na mzingiro
wa ubinafsi na kumsahilishia mambo katika jamii iliyopambika kwa sura za
kila namna, ya umma wa Kiislamu na kumvisha nguo ya kujiepusha na
madhambi ambayo huilinda roho yake kutokana na mashambulizi yaliyojaa
sumu ya mashambulizi na vile vile humuongezea nguvu na moyo wa kupambana
na mashetani na mataghuti. Ni mahala hapo ndipo ambapo hujaji anapoweza
kuonana na Waislamu wenzake wengi wanaunda umma mkubwa wa Kiislamu na
kuona kwa karibu nguvu na uwezo wa umma huo na hivyo kupata matumaini
kuhusu mustakbali mwema na vile vile kupata hisia za wajibu wa kutoa
mchango wake wa kuimarisha umma huo na pia kama atapata taufiki na
msaada wa Mwenyezi Mungu aweze kutoa bay’a na kutangaza utiifu wake kwa
Mtume (Muhammad) Mtukufu wa daraja na kufunga mithaki na ahadi imara kwa
Uislamu azizi na kutia nia ya kweli ya kuijenga kiimani nafsi yake,
kuleta marekebisho katika umma na kutia nguvu neno la Uislamu.
Mambo
yote haya mawili, yaani kuijenga nafsi na kuujenga umma (wa Kiislamu)
ni faradhi zisizoishiwa na wakati na wala zisizofungwa. Njia za kuweza
kufanikisha faradhi hizo mbili si nzito kwa watu wenye mazingatio na
wanaoangalia mambo kwa kina katika utekelezaji wa majukumu ya kidini na
kutumia vizuri akili, tabasuri na wenye mtazamo wa mbali.
Kujenga
nafsi huanzia kwenye kupambana na hisia za kishetani na kufanya juhudi
za kujiepusha na madhambi na kujenga umma huingia sura kwa kumjua adui
na njama zake, kufanya jitihada za kupelekea mashambulizi, hadaa na
uadui wa maadui usiwe na athari zozote na hadi kufikia kwenye
kuziunganisha nyoyo na mikono pamoja na lugha za matabaka yote ya
Waislamu na mataifa yote ya Kiislamu.
Katika
wakati huu tulio nao hivi sasa, moja ya masuala muhimu zaidi ya umma wa
Kiislamu ambalo lina mfungamano (wa moja kwa moja) na mustakbali wa
umma wa Kiislamu, ni matukio ya mapinduzi katika nchi za kaskazini mwa
Afrika na katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo hadi sasa
yameshapelekea kuanguka tawala kadhaa fasidi na vibaraka wa Marekani na
waitifaki za Uzayuni na kuzitikisa tawala nyingine kama hizo. Kama
Waislamu watapoteza fursa hii adhimu na iwapo watashindwa kutumia fursa
hii katika kuujenga vizuri na kuleta marekebisho kwenye umma wa
Kiislamu, basi watakuwa wamepata hasara kubwa. Hivi sasa mabeberu
wavamizi na waingiliaji wa masuala ya ndani ya mataifa mengine wanafanya
juhudi zao zote kujaribu kupotosha harakati hizo adhimu za Kiislamu.
Katika
harakati hizo kubwa, Waislamu wake kwa waume wamesimama kupambana na
ukandamizaji wa watawala (wao madhalimu) na kupambana na udhibiti wa
Marekani ambao umepelekea kudhalilishwa na kudunishwa mataifa ya
Waislamu na kusababisha kushuhudiwa ushirikiano baina ya tawala za nchi
hizo na utawala mtenda jinai wa Kizayuni. Waislamu wamegundua kuwa kitu
kinachoweza kuwaokoa katika mapambano haya ya kufa na kupona ni Uislamu,
mafundisho ya dini hiyo tukufu na nara na kaulimbiu zake zenye uwokovu
na hilo wamelitangaza wazi wazi. Ajenda yao kuu wameifanya kuwa ni
kulitetea taifa madhulumu la Palestina na kupambana na utawala ghasibu
(wa Kizayuni). Wamenyoosha mkono wa urafiki kwa mataifa yote ya Waislamu
na wanataka kuona umma wa Kiislamu unashikamana na kuwa kitu kimoja.
Hii
ndiyo misingi mikuu ya harakati za wananchi kwenye nchi ambazo katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita, wananchi wake wamenyanyua bendera ya
uhuru na mabadiliko na kujitokeza kwa viwiliwili na roho zao kwenye
medani za mapinduzi na ni mambo kama haya ndiyo yanayoweza kuwa misingi
mikuu ya kuleta marekebisho katika umma mkubwa wa Kiislamu. Kusimama
imara na kushikamana vilivyo na misingi mikuu ni sharti la lazima la
kuweza kupata ushindi wa mwisho wa harakati za wananchi kwenye nchi
hizo.
Lengo
la adui ni kutaka kuhakikisha anateteresha misingi hii mikuu. Mikono
fasidi ya Marekani na NATO na Uzayuni inatumia baadhi ya mighafala na
mitazamo finyu kujaribu kupotosha wimbi la harakati ya vijana Waislamu
na wanatumia jina la Uislamu kuwagombanisha Waislamu na wanaiita jihadi
ya kupambana na ukoloni na Uzayuni kuwa ni ugaidi usio na macho katika
ulimwengu wa Kiislamu ili Waislamu wauane wao kwa wao na hivyo maadui
hao wa Uislamu waweze kuokoka na Uislamu na wanajihadi wake watazamwe
kwa sura mbaya na chafu.
Baada
ya maadui kukata tamaa kwa kuona kuwa hawawezi kuushinda Uislamu wala
kuzima nara na kaulimbiu zake, hivi sasa wameamua kuzusha fitna kati ya
makundi tofauti ya Waislamu na wanafanya njama za kueneza chuki dhidi ya
Ushia na chuki dhidi ya Usuni ili kuzuia kupatikana mshikamano na umoja
katika umma wa Kiislamu.
Maadui
wanawatumia vibaraka wao katika eneo (la Mashariki ya Kati), kuzusha
mgogoro nchini Syria ili kuzishughulisha akili za mataifa ya dunia na
kuzifanya zisahau masuala muhimu ya nchi zao na zisahau pia hatari
zinazowakabili. Maadui hao wanajaribu kuwashughulisha (Waislamu) na
masuala ya umwagaji wa damu ambayo maadui wameyazusha wao wenyewe. Vita
vya ndani nchini Syria na kuuliwa vijana wa Kiislamu kwa mikono ya
Waislamu wenzao ni jinai ambazo zilianzishwa na Marekani na Uzayuni na
tawala tiifu kwa maadui ambazo wanazidi kuchochea moto huo. Nani anaweza
kuamini kuwa, tawala ambazo zilikuwa waungaji mkono wa madikteta waovu
wa Misri na Tunisia na Libya, hivi sasa wamekuwa waungaji mkono wa
kutaka demokrasia taifa la Syria? Kadhia ya Syria ni suala la kulipiza
kisasi dhidi ya utawala wa nchi hiyo ambao katika kipindi cha miongo
mitatu ulikuwa umesimama peke yake kupambana na Wazayuni maghasibu na
kuyaunga mkono makundi ya wanamuqawama wa Palestina na Lebanon.
Sisi
tunaliunga mkono taifa la Syria na tunapinga uchochezi na uingiliaji wa
aina yoyote ile wa kigeni nchini humo. Marekebisho ya aina yoyote ile
nchini humo inabidi yafanywe na wananchi wenyewe na kwa kutumia njia
zinazokubaliwa kikamilifu na wananchi wa taifa hilo. Hatua ya mabeberu
wa kimataifa ambao kwa msaada wa tawala za vibaraka wao katika eneo hili
wanatumia kisingizio cha kuenea mgogoro na wakati huo huo kutumia
kisingizio cha kuweko mgogoro kuhalalisha kufanya kila aina ya jinai
nchini humo ni hatari kubwa ambayo kama tawala za eneo hili
hazitajiepusha nayo basi inabidi zisubiri zamu yao ifike ya kukumbwa na
hadaa hizo za kibeberu.
Makaka
na madada! Msimu wa Hija ni fursa ya kutaamali na kuyaangalia kwa kina
masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu. Hatima ya mapinduzi ya eneo
hili na juhudi za madola makubwa yaliyojeruhiwa kutokana na mapinduzi
(ya wananchi wa eneo hili) za kutaka kuyapotosha mapinduzi hayo ni
miongoni mwa masuala hayo (muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu ambayo
inabidi kuyaangalia kwa kina). Njama za wasaliti za kutaka kuzusha
hitilafu kati ya Waislamu na kuleta ugomvi na suutafahumu kati ya nchi
ambazo zimeamua kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu; kadhia ya Palestina
na juhudi za kuifanya itengwe na kuizima jihadi ya Wapalestina;
propaganda za kueneza chuki dhidi ya Uislamu zinazofanywa na tawala za
Magharibi na uungaji mkono wa tawala hizo kwa watu wanaomvunjia heshima
Mtume Muhammad SAW; kuandaa mazingira ya kuzuka vita vya ndani na
kugawanywa vipande vipande baadhi ya nchi za Waislamu; kuzitisha tawala
na wananchi wa nchi za Kiislamu zilizofanya mapinduzi kuhusiana na
hatari za kupinga siasa za kibeberu za Magharibi na kueneza dhana potofu
kuwa mustakbali wao unategemea kujisalimisha kwao mbele na madola ya
kibeberu na masuala mengine muhimu sana kama hayo, ni miongoni mwa
kadhia muhimu ambazo inabidi ziangaliwe kwa taamuli na kwa mazingatio
makubwa katika fursa inayopatikana kwenye Hija na chini ya kivuli ya
kupendana na kuwa na fikra moja nyinyi mahujaji.
Ni
jambo lisilo na shaka kwamba uongofu na msaada wa Mwenyezi Mungu
utawaangazia njia za salama na amani waumini wenye kufanya jitihada
katika mambo yao, ?????? ?????? ???? ???????? ?????Na wanaofanya juhudi
kwa ajili Yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia Zetu. (al Ankabut – 29:69).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Sayyid Ali Khamenei,
Post a Comment