Na: Albert Sanga- Iringa.
Mwaka 2001 nilihudhuria kongamano
la kidini ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili hali ya maendeleo ya
Afrika. Kongamano hilo lilifanyika katika shule
ya sekondari ya Bihawana iliyopo nje kidogo ya mji wa Dodoma. Mada iliyowasilishwa kuhusu Afrika
ilikua na kichwa, “Je, Afrika imelaaniwa?”.
Mtoa mada mkuu alikua ni mzungu
mmoja (mmishenari), ambaye aliamsha mjadala mkali kweli kweli mara baada ya
kumaliza kuwasilisha hoja zake. Katika mjadala uliofuatia (baada ya mtoa hoja
kumaliza) kulijitokeza makundi mawili baina ya wanakongamano; moja likisema na
kuamini kua Afrika imelaaniwa na jingine likipinga kabisa laana ya Afrika.
Upande uliokua ukisema Afrika imelaaniwa ulikua na hoja zenye nguvu kweli kweli
na ulionekana kuuzidi ule upande uliopinga laana ya Afrika.
Mmoja wa wachangiaji alisimama na
kusema maneno yafuatayo, “Ndugu zangu mimi nawathibitishia kua Afrika
tumelaaniwa na uthibitisho huu tunaupata kutoka kwenye Biblia katika Kumbukumbu
la Torati 28: 15- 40. Biblia inasema kuwa; …..utalaaniwa mjini na vijijini,
wageni waliopo kati yako watafanikiwa wewe ukididimia, utapanda mzabibu nawe
hutakula matunda yake, utaandamwa na vita na magonjwa, utadhulumiwa rasilimali
zako…..; Kwa maandiko haya mnabisha nini kusema Afrika imelaaniwa?”.
Mchangiaji mwingine ninaemkumbuka
ambae aliamsha hisia tafakarishi miongoni mwa wote tuliokuwepo pale alieleza
mwonekano wa kijiografia wa Afrika akiulinganisha na laana. Yeye alisema hivi,
“Afrika imelaaniwa na uthibitisho tunaweza kuupata hata kutoka kwenye ramani ya
Afrika yenyewe. Ramani ya Afrika ina umbo la kiulizo hii ina maana kua tutakua
watu wa kuandamwa na mambo yasiyo na majibu maisha yetu yote”.
Upande uliokua ukipinga
ulifurukuta kweli kweli ukitumia hoja ambazo japo kuwa zilionekana kua na
mantiki lakini zilikosa nguvu na ushawishi wa kutosha. Mathalani upande huu
ulisema, Afrika haijalaaniwa kwa sababu Yesu Kristo alipozaliwa baba na mama
yake waliambiwa na malaika wakimbile Afrika katika nchi ya Misri. Kwa maana hii Afrika ilimlea mkombozi wa
ulimwengu.
Hadi leo hoja zilizokua zikisema
Afrika imelaaniwa zingali zimenasa katika akili yangu kutokana na namna
zilivyokua zinagusa picha halisi ya Afrika. Baada ya mjadala huo mtoa mada alisimama
na kuhitimisha mjadala kwa kusema maneno yafuatayo, “Inawezekana Afrika ikawa
imelaaniwa na inawezekana ikawa haijalaaniwa. Hayo yote sio mambo ya
kujishughulisha nayo; ila tunatakiwa kujishughulisha na ukweli uliopo ya kwamba
watu wote ni mali
ya Mungu. Mungu huyu anasema kua anawawazia mambo mema watu wake, wakiwamo watu
wa Afrika. “
“Hakuna sababu ya kukata tamaa ya
maisha eti kwa sababu Afrika imelaaniwa, kwa sababu unaweza kuishi maisha kama
ya Ulaya hata ukiwa Afrika na msisahau kuwa hata katika nchi zilizoendelea kuna
masikini wa kutupwa ambao wanaitamani sana
Afrika.”. Baada ya kuhitimisha huko wahudhuriaji wote tuliingia kwenye maombi
ya siku mbili kuiombea Afrika ipokee ‘upya’ na rehema za Mungu.
Imepita miaka takribani kumi
tangu nishiriki kwenye mjadala na hatimaye maombi kuhusu Afrika. Katika miaka
hii kumi nimeshuhudia mabadiliko makubwa yakitokea katika maendeleo ya Afrika
kiasi ambacho najiridhisha kua maombi ya watu kwa Mungu kuhusu Afrika bila
shaka yamesikika na Mungu ameamua ashuke ‘upya’ hapa Afrika
Kuna msemo maarufu sana usemao, ‘historia hujirudia’ na hilo naona limeanza kutimia kwa Afrika.
Wafuatiliaji wa historia bila shaka wanakumbuka kuwa Afrika ilitangulia kupata
maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii kabla hata ya Ulaya. Bara hili lilikua
na viwanda, lilikua na dola kubwa na zenye nguvu sana tena zilizoendeshwa kidemokrasia na kwa
utulivu mkubwa. Gunduzi nyingi za kisayansi, lugha na kijamii zilitokea Afrika
ikiwemo ugunduzi wa umeme, maandishi ya kwanza, kalenda na hata uhandisi wa
majengo.
Vyuo vikuu vya kale kabisa
duniani vinapatikana Afrika hii ikitupa picha moja kuwa hata kielimu Afrika
ilianza na wengine wakafuata. Orodha ya maendeleo ya Afrika yaliyokuwepo kabla
ya kuingia kwa ukoloni ni ndefu sana
lakini itoshe tu kusema ujio wa ukoloni uliivuruga ‘kabisa’ Afrika. Lakini ile
historia ya maendeleo iliyovurugwa na wakoloni sasa imeanza kujitokeza kwa upya
tena. Afrika imeanza kuinuka.
Yanayoendelea Afrika kwa sasa
yanatia moyo sana kiasi kwamba hata ile misemo ya
kifedhuli kwamba, “Afrika ni bara la giza”,
“Afrika ni kisima cha vita na migogoro” inazidi kupoteza mashiko kwa kasi ya
ajabu. Bila shaka hata viranja wa magharibi ambao wanaimba kuhusu demokrasia
nao wanashangaa yanayotokea Afrika. Ile demokrasia yetu ya ustaarabu na
uungwana sasa inatumika. Vyama vya siasa vinabadilishana madaraka kwa amani,
udikteta unazidi kutokomea, ukibaraka wa viongozi wa Afrika kwa ‘wamagharibi’
unayoyoma kwa kasi ya ajabu.
Siku zote masikini hafilisiki na
anaeinuliwa ni yule aliyechini. Kama tukiwa
makini kutafsiri hali tete za kichumi zinazoendelea duniani tunaweza kuelewa
bila shida mambo yafuatayo; Afrika kwa sababu ni masikini haina kitu kikubwa
cha kupoteza lakini kwa sababu ipo chini ina nafasi ya kuinuliwa.
Anaefilisika ni tajiri, mwenye
kitu ndio hupoteza na aliye juu ndie hushuka. Nchi za magharibi zinaporomoka
kwa kasi na sasa zinapeana mbeleko kuzuiana zisifilisike, lakini wapi!
Zinaendelea kupoteza rasilimali, zinapoteza ushawishi na zinahaha na kutoa
jasho. Walisema waswahili adui yako mwombee njaa; hii ni saa ya Afrika kuinuka
tena!
Ripoti za kimataifa pamoja na
hali mbalimbali tunazozishuhudia zinaeleza picha kamili ya namna hatua za
Afrika zinavyoongezeka hata kama ni pole pole.
Kumekua na ripoti za tafiti mbalimbali kuihusu Afrika zinazotolewa na vyanzo
tofauti tofauti yakiwemo mashirika makubwa ya kimataifa , nchi za magharibi na
mawakala wao. Baadhi ya watoa maoni wanasema ripoti hizi zimekua zikichora
picha hasi kuhusu hali na maendeleo ya Afrika. Na mahali ambapo zinachora picha
chanya basi unakuta eidha ni kwa maslahi fulani ama ni kutaka kuonesha kuwa
walitoa msaada ambao umeleta tija.
Kwa maana hii tunapoitazama
Afrika inayoinuka tena ni busara sana
kutumia vyanzo huru vya takwimu na uhalisi wa mambo katika tathmini zetu
wenyewe. Hata hivyo ripoti na takwimu zinazolalamikiwa kuikandamiza Afrika
zingali zinatufaa kwa kua iwe kwa wema ama kwa ubaya zingali zinabeba kitu fulani kuhusu Afrika
Kwa upande wa uchumi (eneo ambalo
tumekua hatujiwezi kwa miaka mingi) hali inatia moyo sana. Katika nchi kumi ambazo uchumi wake
unakua kwa kasi sana duniani nchi sita zinatoka
katika bara la Afrika; zikiongozwa na Ghana ambayo uchumi wake unakua kwa
kasi ya asilimia 13%. Ghana
ndio nchi inayoongoza kwa kua taifa lenye uchumi unaokua kwa kasi kuliko
mataifa yote duniani.
Ghana yetu imezitupa mbali kabisa
hata nchi nyingi za Ulaya ambazo uchumi wake unajikongoja kukua kwa asilimia
moja. Mataifa ya Afrika ambayo uchumi wake unakua kwa kasi yameshayapiku hata
yale mataifa ya Asia ambayo yanafahamika kama
“Asian Tigers”. Mwaka huu pekee, uchumi wa bara la Afrika unakadiriwa kukua kwa
wastani wa asilimia 6%, hii ni hatua kubwa kutoka mgando wa uchumi katika
asilimia 4% kwa miaka ya nyuma.
Nimesema hapo juu ya kwamba adui
yako mwombee njaa ndipo utamshinda kirahisi. Hadi sasa kuna mataifa ya Ulaya
ambayo yanahenyeshwa na mzigo wa madeni kuliko mataifa ya Afrika. Leo hii nchi
ya Angola
kutoka Afrika inaikopesha fedha na kuipa misaada nchi ya Ureno. Kumbuka kuwa
Ureno iliitawala Angola
wakati wa ukoloni lakini leo Ureno imegeuka kuilamba miguu Angola-huu ni
muujiza!
Benki yetu ya nyumbani, ‘African
Development Bank-AfDB’ kupitia ripoti yake ya kiuchumi inasema kua ifikapo
mwaka 2060 watu wa uchumi wa kada ya kati watakua ni asilimia 42 ikiwa ni
ongezeko la asilimia 10 ukilinganisha na idadi iliyopo kwa sasa. Miaka 50 ijayo
inatazamiwa kuwa idadi ya watu watakaokuwa wakiishi chini ya mstari wa
umasikini uliopindukia watakua ni chini ya asilimia 30. Hii ina maana kua
umasikini unaendelea kupungua kwa kasi ya ajabu na uchumi unazidi kupaa ukilinganisha
na hapo zamani.
Kukua huko kwa uchumi kunaleta
mwanga wa kuongezeka kwa biashara na uwekezaji. Ushahidi tunaweza kuupata kwa
kuyaangalia makampuni ya kibiashara ya Afrika namna yanavyoshindana na
kutunisha misuli katika anga za kimataifa. Mathalani, kampuni ya South Africa
Breweries Miller (SAB) ya nchini Afrika kusini hivi karibuni iliinunua kampuni
ya American Breweries ya nchini Marekani.
Hii inaifanya SAB kuwa kampuni ya
pili kwa ukubwa duniani miongoni mwa makampuni ya vinywaji vya pombe. Jambo
kama hili usongelitazamia kutokea katika miaka ya ‘giza’ la Afrika. Huu ni mfano mmoja kati ya
mifano lukuki ambapo kwa sasa ni kawaida makampuni makubwa ya magharibi
kuyapigia magoto makampuni ya Kiafrika yakiomba eidha kuokolewa kifedha ama
kununuliwa.
Miaka ya zamani kuna hadithi
tulikua tunazipata eti kule Ulaya kuna watu ambao hata hawajui hiyo Afrika iko
upande gani duniani! Inadaiwa walijifanya ‘kuipotezea’ kwa sababu Afrika ilikua
haijisomi kwa kila kitu. Lakini sasa ni tofauti kwa sababu hata makampuni yale
makubwa na yenye viburi yanakimbizana kuja kuwekeza na kuuza Afrika. Jirani
zetu nchi ya Kenya kuna
mamia ya makampuni ya teknolojia kiasi cha kwamba Nairobi
imebatizwa kama kitovu cha teknolojia ya mawasiliano kusini mwa jangwa la Sahara.
Sisi waafrika wenyewe wala
hatuhitaji takwimu za ‘kumulika na tochi’ kujua kua huu ni wakati wetu bali
tunajionea mabadiliko. Wana na binti zetu waliokimbilia ughaibuni kwa
Zaidi bofya hapa ( http://www.mjengwablog.com/)
Post a Comment