Na Ratifa Baranyikwa
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana
katika kikao maalumu kutafakari na kupanga mikakati katika mambo makuu
manne, likiwamo la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014/2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika
Hoteli ya Blue Pearl, ambako kikao hicho kinaendelea leo, Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wameamua kujifungia na
kupanga mikakati ya Uchaguzi wa Serikali na Mitaa mwaka 2014 na ule
Mkuu wa mwaka 2015 ili kujiweka sawa.
Hatua hiyo ya CHADEMA imekuja wakati ambapo vita ya urais imeendelea
kushamiri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vigogo wanaotajwa
kuwania nafasi hiyo nao wakionekana kujipanga na kuandaa mikakati
kuelekea mwaka 2015.
CHADEMA kinaonekana kuwa ndicho chama pekee cha upinzani ambacho
kimejizolea umaarufu mkubwa kwenye medani ya siasa katika miaka ya hivi
karibuni, kikichukua nafasi iliyokuwa imekaliwa na Chama cha Wananchi
(CUF), hivyo kuonekana kuwa tishio dhidi ya chama tawala.
Upepo wa CHADEMA ulionekana kuvuma vema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 ambapo kilishika nafasi ya pili nyuma ya CCM, hali ambayo
imesababisha macho na masikio mara zote kuelekezwa kwenye chama hicho
kikuu cha upinzani, hasa linapokuja suala zima la kuangalia jinsi
kilivyojipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika mkutano huo wa jana na wanahabari, Mnyika alisema kikao hicho cha
siku mbili ambacho kinamalizika leo kimekuwa maalumu kwa sababu ya
unyeti wake, lakini pia kimeshirikisha wabunge wa chama hicho na kuahidi
kueleza namna uamuzi utakavyofikiwa mara baada ya kikao hicho.
Wakati wakipanga mikakati ya 2014/2015, pia vigogo hao wa CHADEMA
wanaangalia namna ya ujenzi wa oganaizesheni ya chama nchi nzima wakati
ambapo mwaka huu watakuwa na uchaguzi mkuu wa ndani.
Katika kujipanga huko, CHADEMA pia imesema kuwa imejiweka sawa kuangalia
namna ya utekelezaji wa kile ambacho chama kiliahidi kukifanyia kazi
kutoka katika maeneo ambayo ina wabunge sambamba na kutafakari namna
ambavyo kambi rasmi ya upinzani bungeni inatekeleza majukumu yake.
Baada ya kikao hicho cha Kamati Kuu, Mnyika pia alisema CHADEMA
inajiandaa kutoa kauli nzito kuhusiana na migogoro inayoendelea nchini,
ikiwamo ya wafugaji na wakulima mkoani Morogoro, wanafunzi wa vyuo vya
St. John, IFM pamoja na suala zima la gesi ya Mtwara mara baada ya
kukutana na Baraza Kuu kesho, ambapo pamoja na mambo mengine watapatiwa
taarifa rasmi kutoka kwa viongozi wao Mtwara, ikiwa ni pamoja na
mapendekezo yao.
Akisisitiza kuhusu suala hilo la gesi, Mnyika alisema kuwa mgogoro
unaoshamiri wa gesi mkoani Mtwara ni matokeo ya sera mbovu ya usimamizi
wa rasilimali za umma, na udhaifu wa kiongozi kushughulikia migogoro.
Katika hilo, Mnyika alisema wao kama CHADEMA wanatoa wito kwa rais
pamoja na serikali yake kurekebisha kauli za vitisho zilizotolewa dhidi
ya wananchi wa Mtwara, kwani ndiyo sababu ya kuendelea kuchochea mgogoro
huo.
CHADEMA mbali na kumtaka rais kutoa kauli zinazojenga muafaka, pia
wamewataka wananchi wa Mtwara wawe watulivu wakati kiongozi huyo wa nchi
pamoja na serikali watakapokwenda kurekebisha kauli.
“Baraza kuu la chama litakutana na wilaya zote Tanzania na tunahitaji
taarifa kutoka Mtwara na hatua wanazozipendekeza tuchukue, hii ni pamoja
na migogoro mingine…hatua ambazo CHADEMA itachukua itatolewa baada ya
mkutano wa Baraza Kuu la chama,” alisema.
Kuhusu suala la baadhi ya wabunge kuhongwa na kwamba wao ndio
wamewachochea wananchi kufanya vurugu, Mnyika alisema jambo hilo kamwe
lisipotoshwe na kuitaka serikali ijibu hoja za wananchi.
Aidha, akifafanua kuhusu hilo Mnyika alikwenda mbali zaidi akisisitiza
kuwa wabunge pia wametofautia mitizamo, lakini akasisitiza kuwa wananchi
wamesukumwa kudai masilahi yao.
Chanzo: freemedia.co.tz
إرسال تعليق