Gavana Ndulu ajitosa fedha za Uswisi

Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu
SAKATA la mabilioni ya fedha zenye utata zinazodaiwa kuwa ni za Watanzania zilizofichwa katika baadhi ya benki za nchini Uswisi, limeingia katika sura mpya, ikibainika ya kwamba kwa sasa wanaodaiwa kuwa na akaunti hizo ni lazima watoe idhini ya kukaguliwa kwa taarifa zao za kibenki.
Fedha hizo takriban Sh. bilioni 303.7 zinadaiwa kufichwa na baadhi ya viongozi nchini Uswisi, wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa.
Tayari Bunge limekwishatoa maelekezo kwa serikali kufuatilia sakata hilo na kuwasilisha taarifa yake katika mkutano wa Bunge wa Aprili, mwaka huu, huku  viongozi mbalimbali nchini wakitoa kauli za kukinzana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora, George Mkuchika, kwa upande wake, mara kwa mara amekuwa akiwataka viongozi wanaodai kuwajua waliotunza fedha hizo wawataje kwa majina, lakini wengi wakimkosoa na kutaka Serikali itimize wajibu wake katika suala hilo.
Safari hii, akizungumzia mchakato wa kuzirejesha fedha hizo katika mahojiano yake na mwandishi wetu hivi karibuni, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, anakiri ugumu wa kurejesha fedha hizo na kueleza kwamba mchakato wa kuzirejesha utahitaji pia taarifa kutoka kwa wenye fedha hizo.
“Kitu kikubwa katika hili ni kwamba Serikali kwa sasa iko katika mchakato wa kulifanyia kazi suala hili. Ninachoweza kusema kiujumla, ziko ripoti za kimataifa zinazotolewa kila mwaka kwa nchi zote, zinazoeleza ni watu wa taifa gani wanaweka fedha katika taifa gani.
“Kwa mfano, Uswisi inatoa ripoti hii kila mwaka, na Marekani inatoa ripoti yake kila mwaka, inayosema wakazi wa Tanzania, katika akaunti za benki za nchi ile wanaweza kuwa wameweka kiasi fulani cha fedha katika akaunti zao.
“Lakini benki hizo, chini ya sheria zao, huwa hawataji (mteja wao) mmoja mmoja, wakisema huyu ana kiasi hiki, huyu ana kiasi kile…inaitwa ‘confidentiality law.’ Wao (Uswisi) wamekuwa kivutio kikubwa kwa watu kuweka fedha zao huko kwa sababu hawatoi siri za wateja wao.
“Kwa hiyo, itatubidi tufanye kazi ya ziada kuzipata, hata hiyo ya kusema tunaifanyia kazi, wenyewe wale wenye akaunti zao kule ni mpaka wao wakubali kutoa taarifa zao, na ujue kwamba wakikubali wenyewe watakuwa wameharibu msingi wa biashara yao. Kwa hiyo, changamoto zipo.
“Tunafanyia kazi, lakini changamoto ya kupata taarifa za mtu mmoja mmoja, tukubali hizi zipo,” anasema Gavana Ndulu katika mahojiano yaliyochapishwa ndani ya toleo hili.
Sakata hilo la mabilioni ya Uswisi liliwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na kuwekewa azimio la Bunge la kuitaka Serikali kufuatilia suala hilo na kurejesha ripoti yake bungeni.
Kati ya viongozi wengine walionukuliwa kuzungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti, ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, na Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave, ambaye amepata kunuliwa akisema Serikali haijaonyesha nia ya kufuatilia sakata hilo.
Katika maelezo yake, Jaji Werema alinukuliwa akisema Serikali inaendelea kufuatilia suala hilo na tayari imeundwa timu maalumu.
Kwa mujibu wa Werema, timu hiyo maalumu iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alifanya hivyo kutokana na idhini ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba, timu hiyo itakuwa ikifanya kazi zake kwa siri.
Hata hivyo, katika msisitizo wake bungeni mwaka jana,  Zitto Kabwe, alidai kuwa na orodha ya majina 10 ya vigogo serikalini na wastaafu ambao ndio wamiliki wa fedha hizo.
Miongoni mwao anatajwa kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge hadi sasa, na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Zitto, katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna Watanzania lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia halali za kupata orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara wakubwa wana akaunti katika benki za Uswisi.
source: Raia Mwema

Post a Comment

أحدث أقدم