Mongela (M/Wilaya) atengua uamuzi wa Lema (Mb) wa kuifunga shule

Saa kadhaa baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kufika katika Shule ya Sekondari Korona iliyopo katika Kata ya Engutoto jijini  Januari 23 mwaka huu na kuamuru shule hiyo ifungwe kwa madai kwamba inaendeshwa kinyume na taratibu za elimu, ikiwemo kupokea wanafunzi kabla miundombinu ya shule kukamilika; Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela ameamuru wanafunzi wa Shue ya Sekondari Korona iliyopo Njiro jijini Arusha, warudi shuleni na kuendelea na masomo.

Shule hiyo iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, mwaka 2011, inao wanafunzi 478 lakini waliobakia wameandikishwa  shuleni hapo ni 118 na kati ya hao, 30 tu ndiyo waliopo shuleni hapo.

Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama na waandishi wa habari waliofika shuleni hapo, Mongela alisema Lema hana mamlaka ya kufunga shule hiyo wala kanuni za ufungaji shule za mwaka 1978 na 1995 hazimtambui mbunge mwenye kutunga sheria na kanuni kuchukua uamuzi.

Alisema kanuni zinamtambua Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi, Ofisa Elimu, walinzi wa amani au Waziri mwenye mamlaka na si Mbunge. Alisema kama Lema alibaini shule hiyo ina upungufu, angeweza kufikisha upungufu huo kwa viongozi na kufanyia kazi na si kuibuka na utaratibu wa kuwachukua baadhi ya viongozi na kwenda nao eneo la tukio kufunga shule.
Mbunge hana mamlaka ya kuifunga shule lazima viongozi tujue sheria na kanuni za kuamua tunayotaka na suala hili lisigeuzwe la kisiasa...  Hapa nikiri kuna upungufu lakini Lema anatoka eneo hili na huu upungufu anaujua, kwa nini asije tuongee na kutatua? Badala yake anaamuru shule ifungwe. Hivi hawa wanafunzi waliokosa masomo yao juzi na jana gharama yake nani atakayeilipa? Nasema Jumatatu ijayo wanafunzi warudi shuleni na shule haijafungwa, pia namvua madaraka Mwalimu Mkuu huyu aliyekuwepo hapa shuleni.
Mwalimu aliyevuliwa madaraka ni John Mbise kutokana na kushindwa kusimamia shule hiyo na kukosekana kwa Bodi ya Shule.

Awali, Lema alifikia uamuzi huo katika kikao cha pamoja cha mashauriano shuleni hapo na Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Eusebi Maeda, kilichohudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni Ofisa Utumishi, Eliphas Mollel na Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza.

Lema alisema kuwa aliifunga shule hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo mengi yaliyosababisha wanafunzi kushindwa kusoma tangu ifunguliwe Januari 14, mwaka huu.
  • Shule hiyo haina huduma ya maji safi baada ya bomba lililokuwepo kukatwa na mamlaka ya maji kutokana na deni la sh 340,000. Pia, pamoja na walimu watano waliopo, mkuu wa shule na msaidizi wake hawaonekani.
  • Baadhi ya wanafunzi wanaishi umbali mrefu zaidi ya kilometa 6.5 na wakati mwingine hulazimika kukodisha gari na kulipa 1,000 kila mmoja. Wakifika shuleni hapo, hukubaliana na waalimu kupumzika kwa saa moja na inadaiwa baadhi ya wanafunzi huingia shuleni hapo saa sita na kupumzika hadi saa saba na saa nane wanarudi majumbani mwao, hivyo kuwa na muda mfupi wa masomo.

Lema aliwaagiza wanafunzi hao wafike ofisini kwake na wazazi wao kesho, huku akimtaka Diwani wa kata hiyo, Anthony Male, kwa kushirikiana na ofisa Elimu kuwahamishia kwa mafungu wanafunzi hao katika shule nyingine zilizomo ndani ya Jiji la Arusha.

Mbunge huyo aliahidi kutoa pampu ya kuvutia maji, vifaa vya kuzalisha umeme wa jua pamoja na matofali 3,000 na kwamba atashirikiana na mkuu wa wilaya na mkoa kuhakikisha shule hiyo inaboreshwa ndani ya miezi mitatu ili kutoa fursa ya kuchukua wanafunzi wa bweni.

Naye Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza, alijitetea kuwa yeye angeomba kwanza afuate  taratibu za kuandika barua kwa Ofisa Elimu Kiongozi ambaye ana mamlaka ya kufunga shule, jambo ambalo Lema alisema aendelee na taratibu zake wakati wanafunzi hao wakiendelea na masomo katika shule nyingine.

Aidha katika utetezi wake juu ya changamoto za shule hiyo, Ofisa Elimu huyo alisema alikwishawahi kupeleka mapendekezo katika vikao vya baraza la jiji vya kununua magari ya wanafunzi lakini yakapingwa na kusema hata hivyo wengi wa wanafunzi waliopelekwa katika shule hiyo wanatoka shule za mchepuo wa Kiingereza, ndiyo maana hawaripoti shuleni hapo.

Kaimu Mkurugenzi alimuomba Lema asubiri kiitishwe kikao cha dharura cha baraza la madiwani wa jiji, alichodai huenda kitatoka na suluhisho zuri zaidi kuhusiana na shule hiyo.

Post a Comment

أحدث أقدم