Na Adnan Hussein, Mogadishu
Serikali ya Somalia itaanzisha mpango mpya hapo Aprili wa kuwalipa
waajiriwa wake kupitia mfumo wa automatiki unaodhibitiwa na Benki Kuu ya
Somalia.
Waziri wa Fedha na Mipango Mohamud Hassan Suleiman aliiambia Sabahi kuwa
programu hiyo ni moja miongoni mwa mipango kadhaa yenye lengo la
kuufanya mfumo wa fedha nchini kuwa wa kisasa, kutoa uwiano wa bajeti na
kuzuia ufisadi wa kitawala na kifedha.
Waajiriwa wa serikali kwa sasa wanalipwa fedha taslimu na wahasibu
waliopangiwa katika wizara zao husika baada ya fedha kulipwa na Benki
Kuu. Wahasibu ndio wenye dhamana ya kukusanya fedah na kumlipa kila
mwajiriwa baada ya kutia saini risiti ya karatasi kama njia ya
uthibitisho.
Mchakato huu, ambao unahusisha kutoa na kusafirisha kiwango kikubwa cha
fedha na kujaza fomu za karatasi, mara nyingi hupelekea kuchelewa kwa
mishahara na kupotea kwa fedha, Suleiman alisema.
Waziri alisema kuwa mfumo huo mpya utazuia kuchelewa huko na kupelekea
uwajibikaji mzuri zaidi na uwazi katika udhibiti wa fedha za umma.
Kukiwa na mfumo wa malipo ambao ni automatiki, kila mwajiriwa wa umma
atapewa akaunti yake binafsi katika Benki Kuu ambako mishahara yao
itakuwa inawekwa kwenye akaunti hizo na kupatikana kwa kutumia kadi ya
beki mwanzoni mwa kila mwezi.
Serikali pia inapanga kutoza kodi katika kampuni zinazotoa pesa taslimu,
kampuni za mawasiliano ya simu, mirungi, sigara, na kwa wauzaji kwenye
masoko ya maeneo, alisema. Kodi zitatozwa pia kwa bidhaa zinazoingia
kupitia bandari za Mogadishu, Kismayo, Bosaso na Berbera.
"Tutapambana na ufisadi wa kiutawala na kifedha na tutaanzisha mipango
ambayo itaturuhusu kukiusanya kodi zaidi na kutimiza ahadi zetu za
kuwatumikia watu wa Somalia," Suleiman aliiambia Sabahi.
Shirika la Transparency International, asasi ya kiraia ya kimataifa
inayopambana na ufisadi, ilizipa daraja Somalia, Afghanistani na Korea
ya Kaskazini kuwa ndizo nchi fisadi zaidi miongoni mwa nchi 176 katika
orodha yake ya 2012.
Msukosuko wa hali ya soko
Serikali lazima ichukue hatua zaidi za kudhibiti fedha za umma katika
juhudi zake za kutuliza uchumi, wachambuzi waliiambia Sabahi.
Mwanauchumi Bashir Mardadi Salah alisema kuwa sheria lazima ziwekwe ili
kuhakikisha kuwa mishahara ya watumishi wa umma inalipwa kwa shilingi ya
Somalia ili kuimarisha thamani yake dhidi ya sarafu za kigeni. Hivi
sasa, akiba ya fedha za kigeni katika Benki Kuu inakadiriwa kufikia dola
milioni 17 na inapungua kwa kiwango cha kutisha, aliiambia Sabahi.
Salah alisema kuwa serikali inapaswa kuhifadhi fedha yoyote ya kigeni
iliyo nayo ili kujenga akiba yake ili kuleta mzunguko mwingi wa shilingi
ya Somalia ambazo zilipangwa kuchapishwa wakati wa serikali ya mpito
lakini bado hazijatolewa.
Mwanauchumi Hiba Abdi Khalif alisema kuwa kuimarisha nafasi ya Benki Kuu
pia itasaidia kusitisha ghiliba katika ubadilishaji wa fedha za kigeni
na wafanyabiashara huru ambao hawawekewi sheria.
Ingawa Benki Kuu ya Somalia ilifunguliwa upya mwaka 2009,
wafanyabiashara huru ndio wanaodhibiti viwango vya ubadilishaji fedha na
wanaweza kulighilibu soko. Kwa miaka mingi, alisema, wafanyabiashara
wamekuwa wakitumia fursa ya msukosuko wa uchumi ulioanzishwa na kukosena
kwa sheria na upungufu wa shilingi ya Somalia iliyopo kwa ajili ya
mzunguko na kughilibu viwango vya ubadilishaji fedha kwa kujipendelea
wao.
Khalif alitahadharisha dhidi ya kushindwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango
kuwakamata watu waliohusika na kughilibu viwango vya ubadilishaji
fedha, ambacho kimeathiri familia za Wasomali wengi ambazo zinategemea
fedha kutoka nje.
Hapo tarehe 17 Januari, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alimteua
mwanauchumi Abdisalam Omer kuwa gavana mpya wa Benki Kuu ya Somalia.
Omer amefanya kazi katika Benki ya Dunia na ana digirii za uzamifu
katika utawala wa umma kutoka Chuo Kikuu cha Tennessee, Marekani.
Via sabahionline.com
إرسال تعليق