Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika Mji wa Timbuktu baada ya kuuchukua kutoka kwa Makundi ya Kiislam
REUTERS/Arnaud Roine/ECPAD/Handout
|
Mkutano wa Kimataifa uliowaleta pamoja Viongozi wa nchi za
Afrika na Maofisa wa Kimataifa umefanikiwa kukusanya jumla ya dola
milioni 600 kwa ajili kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali.
Wafadhili mbalimbali wamechangia fedha kwa ajili ya kuendeleza vita
iliyopewa jina Vita ya Kupambana na Ugaidi Kaskazini mwa Mali lengo
likiwa ni kuyasambaratisha Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala kwa
miezi zaidi ya tisa.
Mkutano huo umefanyika nchini Ethiopia ambapo mataifa hayo
yameahidi pia kuchangia kijeshi ili kufanikisha kukabiliana na vitendo
vya kigaidi ambavyo vyanzo vyake vimekuwa vikitanjwa kuwa nchini Mali.
Japan imechangia dola milioni 120 huku Marekani ikitoa kitita cha
dola milioni 96 kati ya dola milioni 600 ambazo zimeahidiwa kutoka kwa
nchi ambazo zimehudhuria mkutano huo maalum wa kuchangisha fedha.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa UN,
Umoja wa Ulaya EU na China ambao wote wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya
kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi.
Rais wa Mali Dioncounda Traore ameishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa
mchango ambao wameutoa kwa nchi hiyo katika na kuahidi watakuwa tayari
kutoa ushirikiano wa hali na mali.
Umoja wa Afrika AU umeahidi kutoa dola milioni 50 kusaidia operesheni
hiyo ya kijeshi huko Kaskazini mwa Mali ambayo imekadiriwa kugharimu
dola milioni 460 ili iweze kukamilika.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika AU Nkosazana Dlamini-Zuma
amesema wanafahamu kitovu cha mgogoro kwa hiyo ushirikiano ambao
wanaupata kutoka Jumuiya ya Kimataifa utasaidia kupata jibu.
Mkutano huo wa kuchangisha fedha kusaidia vita nchini Mali umekuja
kipindi hiki ambacho majeshi ya Ufaransa na Mali yakifanikiwa kuweka
kwenye himaya yao Mji wa Timbuktu.
Post a Comment