
KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa amesema
siku za chama tawala kukaa madarakani zinahesabika, hatishwi na
wanaomsema kuhusu imani yake na kwamba mchumba wake Josephine Mushumbuzi
ni mwanamke imara.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na Raia Mwema wiki hii, Makao Makuu ya CHADEMA,
Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema CHADEMA kimedhamiria kwa dhati
kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa kuanzia ili
kujisambaza hadi waliko wapiga kura, kimeamua kwamba katika kila kaya 30
za familia kutakuwa na balozi, wakati katika kila nyumba 10 kutakuwa na
kiongozi wa shina, ambalo katika mfumo mpya wa uongozi, litaitwa ngazi
ya msingi.
Aidha, Dk.
Slaa katika mahojiano hayo yaliyochapishwa katika kurasa za 12 na 13, za
toleo hili, na yatakayoendelea wiki ijayo, amesema katika kutekeleza
mkakati wao wa kukipeleka CHADEMA chini kabisa kwa wananchi vijijini,
sasa oparesheni za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) hazitakuwa za mkoa kwa
mkoa tena, kama zilivyokuwa zikiratibiwa, bali zitakuwa zikifanyika kwa
wakati mmoja na kwa mara kwa mara katika vijijini vyote vya Bara na
Visiwani.
Anasema
kuanzishwa kwa utaratibu huo mpya wa mfumo wa uongozi na oparesheni za
M4C, kunalenga kuhakikisha kwamba hadi kufikia Septemba mwaka huu,
CHADEMA inavifikia vijiji zaidi ya 18,000 nchini, kazi itakayokwenda
sambamba na uzinduzi na ufunguzi wa matawi 18,000 ya CHADEMA na zaidi ya
mashina ya msingi 50,000.
Kwa mujibu
wa Dk. Slaa mikakati yote hiyo, inalenga pia kuhakikisha kwamba chama
hicho kinachukua madaraka ya utawala wa Serikali za Mitaa katika
uchaguzi wa 2014, kabla ya kukamata madaraka ya Serikali Kuu mwaka 2015.
Mfumo wa
uongozi katika ngazi ya balozi wa nyumba kumi, ni mfumo ambao hadi sasa
ulikuwa unatumiwa na CCM pekee kati ya vyama vyote vya siasa nchini,
hali ambayo wachambuzi wa mambo wanasema mfumo huo ndio mara nyingi
umekuwa ukikihakikishia ushindi chama hicho katika kila chaguzi za
kisiasa zinazoshirikisha vyama vingi. Dk Slaa alisema viongozi wao nao
katika ngazi hiyo, wataitwa jina hilo hilo la balozi kutokana na kile
alichokiita ‘historia ya jina hilo.’
Akizungumzia
mkakati huo wa kukizamisha chama chake hicho vijijini kuliko na watu
wengi, uamuzi uliotokana na maazimio ya kikao cha Baraza Kuu
kilichokutana hivi karibuni, na ambao unatakiwa kuanza rasmi Aprili
mwaka huu, Dk Slaa alisema:
“M4C sasa
inakwenda kuimarisha misingi ya chama vijijini. Katika kila kaya 30 za
familia, CHADEMA tutakuwa na balozi wetu kama alivyo balozi wa nyumba
kumi wa CCM. Na katika kila nyumba 10, tutakuwa na shina, ambalo tutaita
ngazi ya msingi ya uongozi. Kwa nini na sisi tumeamua kiongozi wetu
aitwe balozi, ni suala la historia tu. Baada ya hapo tunakuwa na
waratibu wa M4C kwenye ngazi ya kijiji, ngazi ya kata, ngazi ya jimbo,
ngazi ya wilaya, mkoa na ngazi ya kanda.
“Ofisi ya
Katibu Mkuu Taifa ndiyo iliyokuwa inaratibu oparesheni zote za M4C. Sasa
ofisi imekasimisha kazi hiyo ya kuratibu oparesheni za M4C kwa Waratibu
wa Kanda. Hawa watachaguliwa na wanachama wetu huko huko kwenye ngazi
ya kanda, kazi yetu sisi wa Makao Makuu, kupitia vikao vyetu vya chama
itakuwa ni kuwathibitisha wale waliochaguliwa kuwa Waratibu.
“Tofauti na
Oparesheni Sangara ambayo ilikuwa inakwenda mkoa kwa mkoa, oparesheni ya
M4C itakuwa inafanyika kwa wakati mmoja katika vijiji vyote vya
Tanzania, Bara na Visiwani. Kwa hiyo, unaweza ukapima mwenyewe aina ya
kishindo kitakachotokana na oparesheni hiyo.
“Tunataka,
kufikia Septemba mwaka huu tuwe tumevifikia vijiji vyote takriban 18,000
vya nchi hii. Tumewekeana malengo kitimu, ni vijiji vingapi vifikiwe na
oparesheni ya M4C, na kwa maana hiyo hiyo, hadi kufikia Septemba
CHADEMA tutakuwa tumefungua matawi ya ofisi za chama chetu vijijini
zaidi ya 18,000 na mashina ya msingi (chini ya balozi) kiasi cha mara
tatu ya idadi hiyo ya matawi.”
Katika
mahojiano hayo, Dk Slaa alizungumzia pia wale wote wanaomshangaa Mchumba
wake, Josephine Mshumbusi, kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika
siasa za CHADEMA, pamoja na wote wanaohusisha upadiri na ukatoliki wake
katika mbio zake za urais.
Akiwazungumzia
wanaomshangaa Mchumba wake Josephine kushiriki moja kwa moja siasa za
CHADEMA, Dk Slaa anasema: “ Kama kuna Watanzania wanashangaa kuniona
nikiwa na Josephine kwenye siasa za CHADEMA, basi hao sijui bado
wanaishi karne gani katika dunia hii. Ina maana watu hao hawajamwona
Michelle akiwa na Obama?
“Ni lini
walimuona Obama katika kipindi chake chote cha kampeni akiwa mpweke bila
kuwa na Michelle? Kuna mazingira fulani, yalimlazimu Obama kuwa na
familia yake nzima kwa maana ya mke wake na watoto wake wale wawili.
Karne hii, mtu anamshangaa mgombea urais kuwa na mke wake. Anamshangaa
katibu mkuu wa chama cha siasa kikubwa kama hiki kumtanguliza mbele mke
wake katika shughuli za umma? Ni maajabu kweli kweli!
“Inawezekana
wanaohoji hayo yote, hawamjui Josephine ni nani, ametokea wapi.
Wanadhani ni kibaka tu niliyemuokota mitaani yupo kwa ajili ya
kunichuna? Wamekosea. Kabla ya kuwa na mimi, huyu alikuwa ndiye mtaalam
pekee wa IT (Teknolojia ya Mawasiliano), Mwakilishi wa UNHCR Kanda ya
Afrika. Josephine ni international figure…mimi nimeishi na kufanya kazi Ulaya, najua aina ya mke wa hadhi yangu.
“Watu
wanakimbilia majungu, hawataki hata kufikiri wafanye utafiti hata kidogo
juu ya maisha ya mtu. Yeyote ambaye angefanya utafiti kidogo tu kuhusdu
maisha ya Josephine; yeye ni nani na ametoka wapi, asingeweza kushangaa
anapomuona akishiriki siasa za moja kwa moja na CHADEMA…huyu kwa asili
yake ni ‘activist’ (mwanaharakati)…nambie ni kwa jinsi gani naweza
kuzuia uana harakati wake eti kwa sababu tu ni first lady mtarajiwa?”
Kwa upande
wa wale wanaosema kutokana na upadiri wake hafai kuwa Rais wa Tanzania
kama ilivyotokea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dk. Slaa
anasema: “Upadiri na Ukatoliki wangu wanaujua zaidi wananchi wa Karatu.
Hawa ndio walioandaa na kushuhudia sherehe zangu za kusimikwa upadiri
mwaka 1977, na ndio ambao wamefurahia huduma yangu kama mbunge wao kwa
miaka 15 hadi naondoka mwaka 2010. Jimbo la Karatu, kama yalivyo majimbo
mengine yote, kuna wakristo na waislamu hivyo hao ndio wanaweza kuhoji
kama katika utumishi wangu kwao, nilionyesha dalili yoyote ya kuwabagua
kwa misingi ya dini.
“Wakati wa
kampeni mwaka 2010, wapo waliosema nimetumwa na Kanisa Katoliki kugombea
urais. Wengine wakasema nautaka urais ili nikatekeleze matakwa ya
Kanisa. Lakini hao hao, ndio waliokuwa wakieneza taarifa kwamba mimi
nilifukuzwa upadri. Yaani Kanisa linifukuze kazi ya upadri, halafu hilo
hilo linitume kazi ya urais. Hao ni wale ambao mara nyingi nawaita watu
wenye ufupi wa akili ya kufikiri!
“Wenye akili
timamu walipaswa kujiuliza Dk. Slaa alitokaje kwenye upadri, kwa maana
Kanisa Katoliki lina utaratibu wake wa kuwaondoa kazini mapadri. Kuna
wanaoondoka kwa kufukuzwa, kuna wanaoondoka kwa kutoroka wenyewe, lakini
kuna wanaoondoka kwa utaratibu kama wa kwangu wa kuandika barua kwa
Papa ya kuomba, barua inapokewa na kujadili sababu zake, na
wakishajiridhisha wanakupatia kile tunachokiita (kwa Kanisa Katoliki)
Laicization, kwa maana ya kurudishwa kwenye kuwa muumini wa kawaida.
“Hata hivyo,
tofauti ya muumini wa kawaida, na tofauti ya padri aliyefukuzwa au
kuacha kazi kwa utoro, mimi nikiwa na wewe safarini tukapata ajali,
ninayo ruhusa ya Papa na Kanisa ya kutoa sakramenti ya upako wa mwisho
kwa mtu anayekata roho na sakramenti hiyo ikapokewa kwa Mungu mbinguni.
Kama wakati inatokea ajali hiyo ninayo Komunyo, naruhusiwa pia kuitoa.
Padiri aliyefukuzwa na au kotoroka hana ruhusa hii.
“Kwa hiyo,
ni watu wale wavivu wa kufikiri, wavivu wa kufanya utafiti wanaoweza
kuihusisha taasisi ya urais na upadiri wangu au ukatoliki wangu kwa
sababu hawataki kujishughulisha kujua taasisi ya urais inafanyaje kazi,
inaendeshaje nchi. Mimi niliondoka salama kwenye upadri. Sina ugomvi na
mapadri wala maaskofu wangu. Labda kwa kuwakumbusha tu Watanzania,
nilipokuwa Katibu Mkuu wa TEC, mimi Dk. Slaa ndiye niliyesimamia
kupeleka mradi wa kwanza kabisa wa maji Kojani, Zanzibar, na hadi leo
maji yale yapo yanatumiwa na jamii ya Kojani, ambao sidhani kama ndani
yake kuna Mkristo hata mmoja.
“Watanzania
turejee kwenye misingi yetu ya asili kama Taifa ambayo ilituwezesha
kuishi kama ndugu moja na Taifa moja. Tuache kuingiza dini kwenye siasa.
Dini ni ya watu na Mungu wao. Dini si suala la nchi. Ufisadi, rushwa na
matumizi mabaya ya rasilimali za nchi yetu, mambo haya hayana dini!
Raia mwema
إرسال تعليق