Kwani Mheshimiwa Makinda, Ndugai ni zaidi ya Watanzania?

  
TUMESIKIA vitisho vya kila aina kutoka kwa wakubwa wenye mamlaka ya ulinzi, wakisema kuwa watawachukulia hatua wale wote waliowatumia ujumbe wa matusi Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.
Hatua ya viongozi hao kutumiwa ujumbe mfupi (sms) na kupigiwa simu ilitokana na wananchi kupewa namba hizo kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wiki iliyopita.
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA,  Mhe. Zitto Kabwe
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Kabwe Zitto, aliwataka wananchi wawatumie ujumbe na kuwapigia simu viongozi hao kadiri wawezavyo na wawaeleze jinsi wasivyoridhishwa na namna wanavyoliongoza Bunge.
Tangu kutangazwa kwa namba hizo, tumesikia taarifa nyingi kuwahusu viongozi hao ambazo zinadai kuwa wamekuwa wakitumiwa ujumbe wenye matusi na vitisho, ambapo sasa wale waliotuma ujumbe huo wamehadharishwa kuwa wakae chonjo kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Kwamba vyombo vya dola kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) wanabaini namba hizo zilizotumika kutuma ujumbe wa matusi na vitisho ili kuwachukulia hatua wahusika.
Hatukubaliani kwa namna yoyote na wale wote waliotuma ujumbe au kupiga simu na kuwatukana viongozi hao wa Bunge. Isipokuwa tunawaunga mkono wale waliofikisha ujumbe sahihi na kueleza hisia zao.
Tunasema hivyo kwa sababu nia ya Zitto na wenzake kuwataka wananchi wawatumie ujumbe viongozi hao ilikuwa ni kutaka walengwa wajue kuwa wananchi hawakubaliani na jinsi wanavyoliendesha Bunge.
Makinda na Ndugai ni sawa na Watanzania wengine. Hivyo wanapokosea ni lazima waelezwe makosa yao, lakini kwa sitaha, si kwa kutukanwa matusi ya nguoni kama wanavyolalamika kufanyiwa.
Laiti vyombo vyetu vya ulinzi hususan Jeshi la Polisi na TCRA wangekuwa wanawathamini wananchi wote kama ilivyo kwa Makinda na Ndugai, bila shaka wangekuwa wamewanasa matapeli wanaowaibia watu mamilioni ya fedha kila siku.

Post a Comment

أحدث أقدم