WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imetakiwa kuacha siasa na malumbano
na badala yake isambaze dawa za maralia aina ya ALu kutokana na vituo
vya kutolea huduma vya umma kuna na uhaba mkubwa wa dawa hizo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari,Mkurugenzi Mtendai wa
Sikika, Irenei Kiria alisema wameshangazwa na taarifa iliyotolewa
na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwamba kuna dawa za kutosha aina
ya ALu hapa nchini wakati si kweli.
Alisema kuwa, Taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo Februari mosi mwaka huu, na kuchapishwa kwenye baadhi ya vyombo
vya habari ilikuwa ikikanusha tamko lilitolewa na Sikika kwenye vyombo
vya habari kuhusu uhaba wa dawa mseto (ALu) kwenye vituo 1300 sawa na
asilimia 26 vya umma vya huduma za afya nchini.
Kiria alisema kuwa, pamoja na Wizara ya Afya kutumia nguvu na muda
mwingi kukanusha uhalisia wa taarifa za uhaba wa dawa za ALu nchini,
hali halisi bado inaonyesha kuwepo ukosefu wa dawa hizo kwenye baadhi
ya vituo hadi Februari 10 mwaka huu.
Alisema kuwa, taarifa ambazo zinapatikana kutoka katika mtandao wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia mfumo wa kielektroniki
ujulikanao kama ‘SMS for life’, zinaonesha kwamba hadi kufikia leo,
asilimia 25 (vituo 1,280) ya vituo vya afya vya umma nchini bado
havina dawa zozote aina ya ALu.
Mfumo huo pia ulionesha kwamba mikoa iliyoripotiwa na Sikika kuwa na
ukosefu wa dawa (ALU na Quinine) uliokithiri hapo Januari 28, 2013
bado ilikuwa haijafikishiwa dawa zinazodaiwa kuwepo nchini. Mikoa hiyo
na asilimia ya idadi ya vituo ambavyo havina dawa hizo (ALU na
Quinine) katika mabano ni; Mwanza asilimia 59, Ruvuma asilimia 49 ,
Shinyanga asilimia 44, Tabora asilimia 40, Mara asilimia 38 na
Kigoma asilimia 38.
Alisema kuwa, taarifa ya Wizara ilidai kwamba mfumo wake wa
kielektoniki (SMS for life), unahusika na dawa za kutibu malaria aina
mbili tu ambazo ni Alu na Quinine na sio dawa nyingine za kutibu
Malaria.
“Sikika inapenda kukumbusha umma kwamba tangu mwaka 2006, Tanzania
imekuwa ikifuata mwongozo wa matibabu ya malaria uliotolewa na Shirika
la Afya Duniani (WHO), unaotumia dawa ya ALu kutibu malaria ya
kawaida na Quinine kwa malaria sugu huku SP ikitumika kwa akinamama
wajawazito” alisema
Alisema kuwa, badala ya kuendeleza malumbano, Sikika inatoa rai kwa
Wizara ya Afya kuutumia vyema mfumo wake wa SMS for life kwa kujipanga
ili kuhakikisha afya za Watanzania zinalindwa na kwamba uhaba wa mara
kwa mara wa dawa za Alu pamoja na zingine kwenye vituo vya huduma za
afya, hautokei tena.
Post a Comment