Afya ya Kibanda yazidi kuimarika

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu (wa kwanza kushoto) Mhariri Mtendaji wa Free Media, Ansbert Ngurumo (aliyesimama kushoto( na Katibu Mkuu Jukwaa la Wahariri, Nevil Meena (Kulia).

Hali ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, imeanza kuimarika baada ya kuanza mazoezi mepesi ya kusimama, kutembea, kuweza kukaa kwa muda na kushiriki mazungumzo.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa TEF, Neville Meena, imesema kuwa Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), hali yake inatia moyo na kuomba Watanzania waendelee kumuombea ili apone haraka.

Meena na wahariri watendaji wengine wa magazeti ya NIPASHE, Jesse Kwayu na Free Media, Ansbert Ngurumo, wapo nchini Afrika Kusini, jijini Johannesburg katika hospitali ya Milpark, alikolazwa Kibanda, kumjulia hali wakati akiendelea kupata matibabu kutokana na tukio la kushambuliwa.

“Jana (Ijumaa) kutwa tulishinda naye hosipitalini na kwa ujumla hali yake inaendelea kuimarika vizuri. Kama tulivyowaarifu tangu juzi, ameanza mazoezi mepesi ya kusimama na kutembea na anaweza kukaa kwa muda na kushiriki mazungumzo. Kwa hakika amechangamka na anatia moyo,” ilisema taarifa ya Neville.

“Hata hivyo, bado mwenyekiti wetu ataendelea kubakia hospitalini kwa matibabu zaidi kama wanavyoshauri madaktari wake. Jambo la msingi tuendelee kumwombea katika sala zetu na wale ambao watapata fursa wafike kumjulia hali na kumtia moyo,” iliongeza taarifa hiyo.  

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Post a Comment

Previous Post Next Post