G.20 yakaribishwa kuwekeza katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

EAC heads of state

Viongozi wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakiimba Wimbo wa Mataifa hayo kabla ya kuanza kwa Mkutano

Mataifa yanayoendelea kupiga hatua za haraka za Kiuchumi Ulimwenguni ya G. 20 yameshauriwa kuwekeza ndani ya Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Mataifa hayo.


Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.

Rais Museveni amesema Mataifa hayo yenye muelekeo mzuri wa Kiuchumi yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya Miundo mbinu ya Barabara ,Mawasiliano na hata Sekta binafsi.

Baadhi ya Mawaziri wa SMT na SMZ walioshiriki Mkutano wa Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 

Amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya Wananchi wake kwa kuimarisha Sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa Serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa Vijana bado ni mdogo.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ametolea mfano Taifa lake la Uganda ambalo limejizatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo yao ambao hubaki wakizurura bila ya utaratibu wa kufanya kazi.

Akiwahutubia Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar pamoja na Watendaji wao Rais Museveni amempongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya.



Mwenyekiti wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni aliyeshika Kofia akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wenzake wa jumuiya hiyo mara baada ya kumaliza Mkutano wao wa 11 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ngurdoto Mkoani Arusha. Kushoto kwa Rais Museveni ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Sheni. Kulia kwa Rais Museveni ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien Habumuryemi pamoja na Rais wa Burundi Bw. Pierre Nkurunziza.(Picha na Hassan Issa OMPR – ZNZ).

Chanzo:Moblog

Post a Comment

Previous Post Next Post