Online link open kwa kuombea mkopo wa Bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu


 
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu pamoja na wanafunzi wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kuanzia Mei Mosi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa bodi hiyo, Cosmas Mwaisobwa alisema maombi ya mikopo yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia anuani yahttp://olas.heslb.go.tz

Alisema vipeperushi maalumu vyenye maelezo ya jinsi ya kuomba mkopo kwa njia ya mtandao vinapatikana kwenye vyuo vya elimu ya juu, ofisi za elimu za wilaya, watoa huduma ya intaneti, Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo na ofisi za Bodi ya Mikopo za kanda.

Aidha, alisema maelezo ya mikopo yanapatikana kwenye tovuti ya bodi ambayo ni www.heslb.go.tz

Alisema waombaji wapya wanatakiwa kulipa ada ya maombi ya sh 30,000 huku wanafunzi walio katika mwaka wa masomo wa tano au wa sita wataendelea kulipa ada ya maombi ya sh 10,000.

"Wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na nne ambao walilipa ada ya maombi ya sh 30,000 katika miaka ya masomo ya 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 hawatakiwi kulipa tena ada hiyo," alisema.

Mwaisobwa alisema mwombaji anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, kudahiliwa katika chuo cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya kugharamia elimu ya juu, kufaulu mitihani ya mwaka uliotangulia kwa waombaji wanaoendelea na masomo pamoja na kuwa mhitaji.

"Bodi inasisitiza kwamba waombaji wa mikopo wazingatie muda uliopangwa na pia kufuata kwa umakini taratibu zote zilizoainishwa katika uombaji wa mikopo," alisema na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya muda uliopangwa kupita. Mwisho wa kupokea maombi hayo ya mikopo ni Juni 30.

---

Post a Comment

Previous Post Next Post