Na Bosire Boniface, Nairobi
Vikosi vya usalama vya Kenya vimetuma askari wengi zaidi katika mpaka wake na Somalia baada ya shambulio katika vituo viwili vya polisi mwishoni mwa wiki kuwafanya maafisa wa serikali kupendekeza zaidi ya idadi mara mbili ya watu wa usalama kupelekwa katika mkoa wa kaskazini mashariki.
Timu ya kutathmini usalama inayoongozwa na Manaibu Inspekta Wakuu Grace Kaindi na Samuel Arachi hapo Jumapili (tarehe 26 Mei) kutembelea kambi za polisi za Abdi Sugow na Damajaley katika Kata ya Garissa, ambako shambulio liliua kiasi cha watu watano, akiwemo mvulana mwenye umri wa miaka 15, na kujeruhi wawili wengine.
Al-Shabaab walidai kuhusika na mashambulizi hayo, na kuongeza kwamba wanamgambo wake waliwateka nyara maafisa wawili wa polisi wakati wa uvamizi huo. "Pamoja na ngawira (ya silaha na vifaa), wapiganaji waliwaburuza Makafiri wawili wa Kenya kama Wafungwa wa Vita na sasa wamo katika mikono imara ya Mujahidina," al-Shabaab walisema katika Twitter.
Tishio la wanamgambo linataka wawepo wanajeshi na polisi kiasi cha mara mbili ili kulinda vijiji vilivyoko mpakani, pamoja na fedha ya ziada na vifaa, Kaindi alisema.
"Mashambulizi haya ni wito wa kupelekwa haraka kwa vikosi zaidi vya usalama, na zana bora zaidi ni muhimu kwa kujibu haraka vitisho vyao," aliiambia Sabahi. "Mafunzo bora zaidi na kuchukua hatua kwa haraka kutoka kwa vitengo vya dharura kutazuia mauaji haya ya kijinga."
Alisema kuwa ulinzi kwa kutumia satelaiti ni muhimu katika kufuatilia shughuli na mienendo ya watu mpakani.
Pamoja na mvulana wa miaka 15, maafisa wawili wa polisi, afisa wa Msalaba Mwekundu na mwalimu waliuawa siku ya Jumamosi, Afisa Wilaya ya Dadaab Bernard ole Kipury alisema.
Msako unaendelea wa maafisa wa polisi waliopotea
Kipury alithibitisha kutekwa nyara kwa maafisa wawili wa polisi, lakini akakataa kwamba wanapaswa kuchukuliwa kama wafungwa wa vita kama ambavyo al-Shabaab walieleza kwa sababu hawakutekwa katika uwanja wa vita. Alitoa wito wa kuwaachwa huru haraka.
"Maafisa wawili wa polisi walitekwa nyara na watu wawili, akiwemo afisa wa polisi, walijeruhiwa katika uvamizi huo," aliiambia Sabahi. "[waliojeruhiwa] wametibiwa na kuruhusiwa na hali zao zinaridhisha."
Kipury alisema kuwa wafanyakazi zaidi wa usalama wametumwa katika vijiji vilivyoathirika na vijiji vyote vya mpakani vimewekwa katika hali ya tahadhari kubwa.
Majina ya maafisa waliopotea ni Fredrick Chirchir na Joseph Wambugu, Kaindi aliiambia Sabahi.
Alisema kuwa vikosi vyote vya usalama vya Kenya vinahusika katika operesheni ya utafutaji wao huku wakiwa na maelekezo ya wazi ya kuwa na tahadhari kubwa sana ili wasihatarishe maisha yao kwa maafisa waliotekwa nyara. Alikataa, hata hivyo, kutoa maelezo zaidi juu ya operesheni hiyo, kwa kusema kwamba kufafanua chochote katika hali hii ni kuhatarisha misheni hiyo.
"Baada ya shambulio la Jumamosi, wawili wa maafisa wetu bado wamepotea na juhudi za kuwatafuta ziko njiani," alisema Inspekta Mkuu wa Polisi David Kimaiyo baada ya mkutano wake na viongozi kutoka Wajir, Mandera na Garissa siku ya Jumatatu. "Tunafanya kila kinachowezekana ili kuwapata. Jeshi pia linasaidia katika utafutaji mpakani."
"Pia tutaomba msaada kutoka kwa wazee wa upande wa pili wa Somalia," alisema, kwa mujibu wa Capital FM ya Kenya.
Wananchi katika tahadhari
Mkuu wa Damajaley, Omar Khalif, ambaye alipatwa na jeraha la risasi mguuni kwake wakati wa shambulio, alisema kuwa watu wenye silaha wa al-Shabaab walikuwa wameweka uzio kwa zaidi ya masaa manne, kuanzia saa 12 mchana.
"Hali ingekuwa mbaya zaidi kama isingekuwa kwa ushujaa uliooneshwa na maafisa wapiganaji," aliiambia Sabahi. "Maafisa katika kambi ya Damajaley walijitolea kila kitu, yakiwemo maisha yao, ili kuvilinda vijiji, lakini walizidiwa nguvu na kikundi ambacho kilikuwa na zaidi ya watu ishirini."
Vikosi vya usalama huko Liboi, ilioko umbali wa kilomita 15, vilichelewa kuitikia shambulio kwa sababu wanamgambo walikuwa wamekata mawasiliano, alisema.
Khalif alisema kuwa tukio hilo linapaswa kuwatahadharisha wakazi wawe na tahadhari juu ya wale wanaowakaribisha. "[Wanamgambo] lazima watakuwa wamehifadhiwa na mtu kijijini ili kuwapa muda wa kuvichunguza vituo vya polisi kabla ya kufanya shambulio," alisema.
Gavana wa Kata ya Garissa Nathif Jama Adam alisema kuwa hali ya kutokuwepo kwa usalama kunaweza kuwa na athari hasi kwa maendeleo na uchumi wa kata, licha ya ukweli kwamba shambulio hili limekuja baada ya mwezi mzima wa utulivu kabisa.
"Wakati kata nyingine zinafanya mikutano ya uwekezaji, Kata ya Garissa inajishughulisha na mikutano ya kutafuta njia za kukomesha ghasia," aliiambia Sabahi. "Wakazi wanapaswa kuungana na serikali ili kutokomeza tishio la ghasia."
"Tunavitaka vyombo vyote vya usalama kufanya kazi kwa kuratibu pamoja na mashirikiano na jamii ili kumaliza vurugu hizi," alisema.
Source; sabahionline.com
إرسال تعليق