HUYU NDIYE MSAUZI MWEUSI ALIYE JITANGAZA YEYE NI YESU

 

WIKI mbili baada ya Alan John Miller, raia wa Australia kutangaza kwamba  yeye ni Yesu na mkewe ndiye Maria Magdalena, nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’ raia wa nchi hiyo, Moses Hlongwane naye ametangaza hadharani kwamba yeye ni Yesu Kristo wa Nazareti.
Alan mwenye miaka 50, ambaye ni mstaafu wa utaalamu wa kompyuta, alisema yeye na mkewe walikuja duniani miaka 2000 iliyopita, jina lake likiwa Yeshua Yusuf au Yesu wa kwenye Biblia, mtoto wa Mariam na Yusuf.
Alisema Mariam Magdalena wa kwenye Biblia ndiye mke wake na ndiye mtu wa kwanza aliyemtokea baada ya kufufuka. Maneno hayo ameyaandika kwenye tovuti yake pamoja na DVD zake zikimuonesha akijibu maswali kutoka watu mbalimbali.
Kwa upande wa Moses wa Sauzi, licha ya Yesu ‘orijino’ kujulikana alikuwa mweupe na alishapita,  tayari amezoa mamia ya wafuasi ambao wamekuwa wakimchangia fedha kwa ajili ya kuhakikisha ujumbe wake unaenea dunia nzima.
Moses, mkazi wa Kwazulu-Natal amekuwa akitumia muda mwingi nyikani kama ilivyokuwa kwa Yesu na kusema kwamba yeye ni mwana wa Mungu aliye hai.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha E News cha nchini humo, Moses alisema:
“Nimepambana na shetani kwa miaka ishirini na mbili na nimemshinda, sitakufa tena, najiandaa kufukua makaburi ili wafu wafufuke na kuwaponya walemavu.”
Mfuasi mmoja wa Moses, Paul Sibiya (84) alisema ameamua kutoa fedha zote za kiinua mgongo chake kwa mtumishi huyo akiamini ni mwana wa Mungu.
Mke wa mfuasi huyo, Alfin alisema mumewe anaamini kwa kufanya hivyo anatoa moyo wake kama sadaka.
Watu mbalimbali ambao wamekuwa wakizungumzia habari za akina Yesu hao huwa wananukuu mstari ndani ya Biblia, Kitabu cha Mathayo 24:5, usemao watatokea wengi wakisema wao ndiyo Kristo, wasisikilizwe.

Post a Comment

أحدث أقدم