Mbowe akerwa na watuhumiwa kusota mahabusu

MBUNGE wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA), ameitaka serikali kutoa tamko na kueleza ni lini itakomesha tabia ya watu kukaa mahabusu kwa muda mrefu kutokana na kucheleweshwa kwa hukumu za kesi zao.
Mbowe alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza ambapo alisema wapo watu ambao wanateseka na kukaa gerezani kwa muda mrefu kwa sababu tu ya kushindwa kufikishwa mahakamani.
“Mahabusu katika gereza la Kalanda katika eneo la manispaa ya Moshi hupelekwa kwenye kesi zao wilaya ya Hai mara moja kwa wiki, na ikitokea kwa bahati mbaya au nzuri wiki hiyo hakimu akawa hayupo watasubiri hadi wiki nyingine tena alhamisi na kuendelea kukaa mahabusu bila sababu.
“Kwa nini tunawaadhibu watu wasio na hatia? Namtaka waziri kwa niaba ya serikali atuambie tatizo hilo litakoma lini na kuacha kuwaadhibu watu bila sababu!” alisema Mbowe.
Awali katika swali la msingi mbunge wa Viti Maalumu Clara Mwatuka (CUF), aliihoji serikali sababu za msingi zinazosababisha kesi zisizohitaji uchunguzi au ambazo uchunguzi wake umekamilika kutolewa uamuzi kwa haraka.
Akijibu maswali hayo kwa pamoja Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki, alisema jukumu la kusafirisha mahabusu hapa nchini ni la jeshi la polisi wakati kwa mkoa wa Dar es Salaam ni jukumu la jeshi la magereza.
Alisema licha ya kazi kubwa na nzuri inayofanywa na jeshi hilo, linakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa mafuta na uhaba wa magari na tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameanza kuzungumza na wafadhili mbalimbali pamoja na Wizara ya Fedha ili kupata fedha za kununua magari na mafuta ili kumaliza tatizo.
Pamoja na hilo alisema kuna mradi wa programu ya sekta ya sheria na wamekuwa wakinunua magari na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali.
Akijibu swali la msingi alisema kesi zote za jinai zinazopelekwa katika mahakama hapa nchini lazima zifanyiwe upelelezi wa kina kabla hazijafunguliwa mahakamani.
Naibu waziri huyo alisema kesi zikishafunguliwa mahakamani sheria na kununi zilizopo za uendeshaji wa kesi zinataka kesi isikilizwe na kutolewa uamuzi mapema ila kama kuna sababu ya msingi inayosababisha kuchelewesha uamuzi.
Alifafanua kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zinasababisha ucheleweshwaji wa maamuzi kwa kesi ambazo upelelezi wake umekamilika.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na wingi wa kesi zinazofunguliwa na idadi ndogo ya watumishi waliopo; sababu za kiufundi za kisheria zinazosababisha mapingamizi ya kisheria na hivyo kukwamisha kwa muda ukamilishaji wa maamuzi /uamuzi mapema.
Nyingine ni ufinyu wa bajeti, vikao vya kusikiliza kesi za mahakama kuu kutofanyika mara kwa mara, upungufu wa vitendea kazi kwa upande wa mahakama za nchi na wadau wake, kutopatikana kwa fedha za kuwalipa mashahidi.
Aidha kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati na kusababisha kesi kuahirishwa mara kwa mara, mahabusu kutofikishwa mahakamani siku za kusikiliza kesi zao, dharura kwa watendaji/pande muhimu kwenye kesi mahakamani-hakimu mwendesha mashtaka, wakili wa utetezi, mshtakiwa na wazee wa baraza.
Nyingine ni uhamisho wa mahakimu unaosababisha kesi isiendelee hadi atakapopatikana hakimu mwingine wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo au kuanza upya kwa kadiri sheria itakavyohitaji kwa kesi husika.

Post a Comment

Previous Post Next Post