Mbowe alitoa
kauli hiyo bungeni mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la
nyongeza ambapo alisema wapo watu ambao wanateseka na kukaa gerezani kwa
muda mrefu kwa sababu tu ya kushindwa kufikishwa mahakamani.
“Mahabusu
katika gereza la Kalanda katika eneo la manispaa ya Moshi hupelekwa
kwenye kesi zao wilaya ya Hai mara moja kwa wiki, na ikitokea kwa bahati
mbaya au nzuri wiki hiyo hakimu akawa hayupo watasubiri hadi wiki
nyingine tena alhamisi na kuendelea kukaa mahabusu bila sababu.
“Kwa nini
tunawaadhibu watu wasio na hatia? Namtaka waziri kwa niaba ya serikali
atuambie tatizo hilo litakoma lini na kuacha kuwaadhibu watu bila
sababu!” alisema Mbowe.
Awali katika
swali la msingi mbunge wa Viti Maalumu Clara Mwatuka (CUF), aliihoji
serikali sababu za msingi zinazosababisha kesi zisizohitaji uchunguzi au
ambazo uchunguzi wake umekamilika kutolewa uamuzi kwa haraka.
Akijibu
maswali hayo kwa pamoja Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah
Kairuki, alisema jukumu la kusafirisha mahabusu hapa nchini ni la jeshi
la polisi wakati kwa mkoa wa Dar es Salaam ni jukumu la jeshi la
magereza.
Alisema
licha ya kazi kubwa na nzuri inayofanywa na jeshi hilo, linakabiliwa na
tatizo kubwa la ukosefu wa mafuta na uhaba wa magari na tayari Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi ameanza kuzungumza na wafadhili mbalimbali
pamoja na Wizara ya Fedha ili kupata fedha za kununua magari na mafuta
ili kumaliza tatizo.
Pamoja na
hilo alisema kuna mradi wa programu ya sekta ya sheria na wamekuwa
wakinunua magari na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali.
Akijibu
swali la msingi alisema kesi zote za jinai zinazopelekwa katika mahakama
hapa nchini lazima zifanyiwe upelelezi wa kina kabla hazijafunguliwa
mahakamani.
Naibu waziri
huyo alisema kesi zikishafunguliwa mahakamani sheria na kununi zilizopo
za uendeshaji wa kesi zinataka kesi isikilizwe na kutolewa uamuzi
mapema ila kama kuna sababu ya msingi inayosababisha kuchelewesha
uamuzi.
Alifafanua kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zinasababisha ucheleweshwaji wa maamuzi kwa kesi ambazo upelelezi wake umekamilika.
Alizitaja
sababu hizo kuwa ni pamoja na wingi wa kesi zinazofunguliwa na idadi
ndogo ya watumishi waliopo; sababu za kiufundi za kisheria
zinazosababisha mapingamizi ya kisheria na hivyo kukwamisha kwa muda
ukamilishaji wa maamuzi /uamuzi mapema.
Nyingine ni
ufinyu wa bajeti, vikao vya kusikiliza kesi za mahakama kuu kutofanyika
mara kwa mara, upungufu wa vitendea kazi kwa upande wa mahakama za nchi
na wadau wake, kutopatikana kwa fedha za kuwalipa mashahidi.
Aidha
kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati na kusababisha kesi kuahirishwa
mara kwa mara, mahabusu kutofikishwa mahakamani siku za kusikiliza kesi
zao, dharura kwa watendaji/pande muhimu kwenye kesi mahakamani-hakimu
mwendesha mashtaka, wakili wa utetezi, mshtakiwa na wazee wa baraza.
Nyingine ni
uhamisho wa mahakimu unaosababisha kesi isiendelee hadi atakapopatikana
hakimu mwingine wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo au kuanza upya kwa
kadiri sheria itakavyohitaji kwa kesi husika.
إرسال تعليق