Nani zaidi leo Kombe la Mabara, Neymar, Suarez? Hispania, Italia kesho


 
RIO DE JANEIRO, Brazil
WASHAMBULIAJI Neymar wa timu ya taifa ya Brazil na Luis Suarez wa Uruguay ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuwa kivutio leo wakati mataifa hayo hasimu kisoka yatakapokutana katika mechi yao ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea nchini Brazil.
Brazil ambao ni wenyeji wa michuano hiyo, walitinga nusu fainali kwa kishindo, wakiwafunga Japan na Mexico bila kuruhusu lango lao na kisha kuishindilia Italia magoli 4-2 katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi.
Uruguay walifuzu kwa hatua ya nusu fainali baada ya kulala 2-1 mbele ya Italia na kisha kushinda mechi nyingine zilizofuata za hatua ya makundi dhidi ya Nigeria na Tahiti.
Hadi sasa, timu zote zimeonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao na mechi yao leo inaweza kuwa miongoni mwa mechi za kusisimua zaidi katika michuano hiyo.
Mbali na Neymar aliyetua Barcelona hivi karibuni, Brazil inatarajiwa pia kuwategemea nyota wake waliong'ara zaidi kwenye michuano hiyo hadi sasa ambao ni pamoja na Marcelo wa Real Madrid, Paulinho wa Corinthians anayewaniwa na Tottenham Hotspur, Oscar wa Chelsea, Thiago Silva wa PSG na Fred.
Kwenye kikosi cha Uruguay, Suarez ambaye ni nyota wa kutumainiwa pia wa klabu ya Liverpool anatarajiwa kuwasumbua mabeki wa Brazil akishirikiana na nyota wenzake Edinson Cavani wa Napoli na Diego Forlan wa Inter Milan.
Neymar ana rekodi nzuri ya kuifungia Brazil magoli 24 katika mechi 35 huku Suarez  akiandika historia kwa kuwa kinara wa muda wote wa upachikaji mabao katika timu ya taifa ya Uruguay baada ya kufunga magoli mawili waliposhinda 8-0 dhidi ya Tahiti na kufikisha magoli 36.

LEO, Jumatano
Nusu fainali ya kwanza
Brazil v Uruguay (saa 4:00 usiku)

KESHO, Alhamisi
Nusu fainali ya pili
Hispania v Italia (saa 4:00 usiku)

Post a Comment

أحدث أقدم