NSSF yaandaa chakula cha mchana kwa wastaafu Dar

 

 
Picture
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) leo limejumuika pamoja kwa kula chakula cha machana na baadhi ya wastaafu wanaohudumiwa na mfuko huo hadi sasa baada ya kustaafu kazini wakiwa wanachama wa mfuko huo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema tukio hilo la kukutana na wastaafu wanaonufaika na mafao ya uzeeni na kula chakula cha pamoja ni la kawaida kila mwaka na ufanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Magori alisema mbali na kujumuika katika chakula wastaafu hao wanufaika na mafao ya uzeeni hupata fursa ya kukutana na wafanyakazi wa shirika hilo na kubadilishana mawazo ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza na kujua wanavyoendelea katika maisha yao ya kustaafu.

Alisema mbali na zoezi hilo lililowakutanisha mamia ya wastaafu muda mwingine wafanyakazi wa NSSF huwatembelea baadhi ya wastaafu maeneo wanaoishi ili kujua maendeleo yao, ikiwa ni pamoja na kupata maoni yao juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.

"Leo tumekutana na wastaafu tunazungumza nao na kuwasikiliza hoja zao...na si hivyo tu sisi ni kawaida yetu mstaafu endapo tunabaini kuwa hajafika kwa miezi kadhaa mwenyewe kuchukua malipo yake pale Posta basi lazima tumtembelee na kujua nini kimetokea, kwa hiyo jambo kama hili la kukutana na wanufaika wa huduma zetu mara kwa mara ni utaratibu wetu," alisema Magori.

Naye mgeni rasmi wa hafla hiyo, Naibu waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga  aliipongeza NSSF kwa kuwa na utaratibu wa kuwakumbuka waliokuwa wanachama wao ambao kwa sasa wananufaika na mafao ya uzeeni na kuongeza kuwa utaratibu huo ni wa kuigwa na mifuko mingine.

"Binafsi nimependa utaratibu huu wa kujumuika pamoja na wastaafu, maana ingekuwa ni wengine wasingeliwakumbuka tena ukizingatia nyie (wastaafu) sasa haichangii tena zaidi ya kulipwa...lakini NSSF bado wanawakumbuka na kuwajali hili ni jambo jema," alisema Dk. Mahanga.

Aidha alishauri mikutano ya kukutana na wastaafu hao mara nyingine iwe na muda mrefu zaidi ili wazee wapewe muda wa kutosha kutoa maoni, kuuliza maswali na kujibiwa juu ya masuala mbalimbali ya huduma za NSSF. 

Baadhi ya wastaafu hao pia waliusifia utaratibu huo na kuushukuru uongozi wa NSSF kwa kuwakumbuka hivyo kushauri utaratibu kama huo uendelee kwani ni mahali pekee ambapo wao hupata muda wa kutoa maoni yao juu ya huduma anuai za NSSF.

~Imeandaliwa na www.thehabari.com

Post a Comment

أحدث أقدم