RIWAYA: ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron
WIVU….huwezi kutambua kama una ugonjwa huo mpaka pale utakapoanza kukushambulia, wivu hushambulia katika namna ya kipekee, wivu ambao ni kidonda na wahenga walisema ukiushiriki utakonda, haswaa!! Ilikuwa hivyo maradhi ya wivu huishambulia akili vyema, huifanya isifanye kazi ya kufikiri mambo mengine na badala yake kufikiria juu ya kitu kimoja tu. Wivu ukishaimaliza akili huuvamia mwili na kuupunguza kilo katika namna ya kustaajabisha isiyosimulika kwa namna yoyote ile, kisha wivu humfanya mgonjwa kuwa mwewndawazimu wa jambo Fulani, kwa mtazamo wa haraka haraka mtu mwenye wivu na mwendawazimu hawana tofauti kubwa. Maana mwenye wivu yupo tayari kukimbizana na magari barabarani akiamini anaweza kuyafikia, mwenye wivu yupo tayari kujifanya yeye ni mpelelezi japokuwa hajasomea. Na mara nyingine mgonjwa wa wivu huwa bingwa wa kutukana na kupigana.
Ubaya wa gonjwa hili, hukomaa kimya kimya bila mtu kujua kama tayari limejipandikiza katika mwili wake.
Wivu hauchagui jinsia wala umri, wivu huja wakati usiotegemea ilimradi tu kukuonyesha kuwa una jambo katika mwili wako.
Gonjwa hili huchukiwa na wengi, lakini afadhali basi wanaoyatambua madhara ya wivu wanaweza kujiongoza wanapougua lakini vipi kwa Joyce Kidoti ambaye hakuwahi kujua vyema wivu ni ugonjwa wa aina gani.
Ile hali ya kujisikkia vibaya Isaya asipompigia simu nd’o alitafsiri kama wivu.
Hakika! Alikuwa sawa lakini huo ulikuwa ni wivu mdogo usokuwa na madhara.
Siku alipoupokea ujumbe matata kutoka kwa Isaya ndipo lile gonjwa rasmi la wivu likajitangaza kuwa limo katika damu yake. Limekaa katika akili na muda si mrefu litatapakaa na kuanza kuutafuna mwili wake.
Joyce aliketi kitandani vyema na kujiuliza ni msichana gani huyu ambaye Isaya anamuita mpenzi wake. Shida ya kwanza kabisa akataka amjue ni wa aina gani ili kabla hajamsikitikia Isaya ajisikitikie mwenyewe.
Sifa za kwamba yu mrembo wa kutisha zilimfanya awe na kiburi bila kujijua, aliamini hata Isaya alidatishwa na urembo wake.
Sasa kwa huyo mwingine amedata na nini? Alijiuliza…..
Mawazo lukuki na ndoto kufifia vyote vilimuandama. Wakati alikuwa akitarajia kwa kupitia Isaya anaweza kujipenyeza na kuingia rasmi katika siasa ambayo inaweza kumfanya awe kiongozi siku moja katika kisiwa cha Ukala na kuleta mabadiliko, sasa huyu Isaya hataki kutumiwa ujumbe hovyo.
Kunani??? Alijiuliza. Nani angempa jibu….
Hakuna!!
Alitakiwa kulitafuta jibu. Jibu ambalo litampa mwongozo wa nini kinafuata iwapo mwanaume ambaye ametokea kumpenda anajihusisha na mwanamke mwingine.
Akajilazimisha kulala bila mafanikio ya upesi hadi majira ya saa nane alipofanikiwa kupotea katika lindi la usingizi.
Asubuhi akamka akiamini kuwa ile ilikuwa ndoto, akaichukua simu yake akafungua na kukutana na ujumbe wa Isaya.
Akafadhaika!!
Siku hiyo mapema wivu ukamdanganya kuwa yeye ni mpelelezi wa kimataifa na mpiganaji mzuri sana iwapo itabidi. Akaingia chuo akiwa na lengo moja tu kumjua mpinzani wake. Huku akijilaghai kuwa huenda Isaya alikuwa anampima imani….
“Yaani kama ananipima imani itakuwa nafuu maana dah….” Alijipa moyo wa imani.
ALIPOKIFIKIA chuo akitokea maeneo anayoishi katika chumba cha kupanga, macho baadhi ya watu waliokuwa wakimfahamu yalimtazama kwa mashaka na huruma kiasi Fulani.
Hakufanikiwa kuona matukio hayo maana alikuwa akiwaza mengi sana.
Usiombe kukwazwa na jambo ewe mtu mzima kisha mtu akwambie neno pole. Hili neno huonekana kuwa la kistaarabu lakini kwa mpokeaji huhisi linamaanisha hakuna kinachowezekana tena, ni sawasawa na mfiwa kupewa pole. Marehemu hataamka kamwe.
Joyce alikutana na maneno haya kutoka kwa marafiki zake. Baada ya kumweleza mengi kuhusiana na Isaya.
“Yaani yule ni kawaida yake, tulijua tu maskini ona hata nywele umesahau kuziweka vyema.” Rafiki yake mmoja alimweleza huku akimweka sawa nywele zake kichwani.
“Ujue Isaya atajuta sidhani kama atadumu na yule msichana, au ule urembo nd’o umemvutia labda…” rafiki mwingine alisema. Neno ‘urembo’ likamvuruga akili Joyce. Akastaajabu kuwa kumbe Isaya amepata msichana mrembo zaidi.
Maneno yakaendelea na pole zikifululiza. Hapo sasa Joyce Keto akakosa uvumilivu, chozi likajiviringisha katika jicho lake la kuume na kisha kuchuruzika katika mashavu yake.
Wivu ulikuwa unamsulubu!! Hakuweza kusema neno lolote lile.
Marafiki zake walimwondoa katika mgahawa na kumpeleka chini ya mti huku wakiendelea kumfariji.
ILIBAKI kidogo tu Joyce aridhike na matokeo na kukubali kuwa Isaya hakuwa chaguo sahihi kwake, nafsi ilipingana naye lakini hakuwa na jingine la kujifariji.
Lakini siku hiyohiyo kwa maksudi ya kila namna Isaya na weapambe wake wakaitafuta namna ya kumwonyesha Joyce kuwa hawamnyenyekei.
Ni siku hii iligeuza kila kitu katika historia ya maisha yake ya chuo kikuu. Ni siku hii alipogundua kuwa kuna tofauti kati ya mapenzi na urafiki.
Ni siku hii alipobaini kuwa Betty yule rafiki yake wa dhati ndiye alikuwa katika mahusiano na Isaya Akunaay. Betty yule muathirika wa gonjwa hatari la Ukimwi ambaye anausambaza maksudi kwa nia moja tu ya kupata pesa.
Joyce alitamani kusema neno lakini akasita akakumbuka kuwa aliweka kiapo cha moja kwa moja kuwa kamwe hatafungua kinywa chake kusema juu ya tatizo la Betty.
Lakini alipokuwa amegusa Betty ni pabaya sasa, alikuwa amegusa mahali ambapo Joyce amekufa na kuoza kimahaba.
Akili ya Joyce isingeweza kulala zaidi, akamtafuta rafiki na mpambe halisi wa Isaya, akamchimba maswali mawili matatu. Akapata jibu kuu alilokuwa akilihitaji.
Isaya hakuwahi kufanya mapenzi na Betty katika hizo siku tatu.
Hakika! Joyce akafumba macho na kukumbuka kuwa Betty alikuwa katika siku zake kwa kipindi hicho.,joy akafanya ishara ya msalaba kama ishara ya kushukuru kuwa Isaya bado anayo nafasi ya kuishi.
Shughuli ikawa kile kiapo alichoweka mbele ya Betty siku ya kwanza kiapo cha milele. Alitaka kukipuuzia kisa Isaya ni hapo alipokumbuka jinsi Betty alivyoukwaa Ukimwi kwa sababu yake yeye Joy aweze kusoma. Kwa maana hiyo bila Joy hata hapo alipo asingekuwepo na bila yeye kuhitaji elimu bila shaka Betty asingeukwaa Ukimwi.
Mbaya zaidfi akakumbuka kuwa bila Betty huenda angeibwia sumu ya panya baada ya kulazimishwa kuolewa. Betty akamzuia na kumwahidi kumpigania……hakika alimpigania haswaa.
Mapenzi kitu gani? Alijiuliza baada ya kugundua mapenzi yanataka kuyumbisha msimamo wake kimaamuzi.
Joyce Keto Kidoti alipogundua kuwa hawezi kumsaliti Betty na kuitoa siri yake ili kumwokoa Isaya ni hapo pia alipogundua kuwa hawezi kushiriki dhambi ya kumtazama kijana ambaye anampenda kwa dhati ateketee kwa kuukwaa Ukimwi kisa tu analipiza kisasi cha kutopendwa na Joyce.
Ni hapa ndipo Joyce alipoinama na kuitazama mikono yake miwili akakutana na maajabu, alikuwa amebeba roho za watu wawili, roho moja kila upande, huku ya Isaya na huku ya Betty. Ni roho ipi ina thamani kwa wakati ule, ni roho ipi aikamate imara ili asijedhurika na usemi wa mshika mbili moja humponyoka.
Ama!! Hazikuwa mbili tena, Joy akakumbuka pia kuwa ana masomo kichwani mwake, hiyo ilikuwa roho nyingine, kwani kwa kufeli masomo yake basi kila kitu kingeharibika.
Je aitunze siri ya Betty ili Isaya afe, ama amwokoe Isaya kwa kuitaja siri ya Betty ili Betty aabike na uwe mwisho wa urafiki wao, ama ashikilie masomo huku yatakayoendelea yatajulikana mbele kwa mbele.
Hili la kuendelea kusoma bila kujihusisha na wawili hawa likawa mbinde sana, asingeweza kusoma katika hali ile.
Maamuzi yakawa magumu sana kufikiwa. Roho tatu katika mikono miwili. Kila roho na thamani yake ya kipekee.
Kichwa kikamuu haswa.
Akajikongoja akachukua taksi ikamrudisha nyumbani kwake.
Huku akakutana na uso wa Betty ukiwa umechanua kwa furaha.
“Shosti…mtoto wa mbunge kiganjani kwangu pumbavu zake…atanikomaje?” Betty alimweleza Joy huku akirusha mikono yake juu.
Kichwa ni kama kilitaka kupasuka na kujiondokea kabisa, Joy alihitimisha kile alichokiona na kukisikia.
Macho yalikuwa mekundu sana, akasingizia kuwa anaumwa kichwa, Betty akamtafutia dawa na kumpatia anywe, Joy akazipokea na kuzimeza. Kisha akakirukia kitandani, kizunguzungu kikiwa kimemwandama.
Kitanda kikaonekana kama kinazunguka kwa kasi katika namna yua kukera, joto likaizidi maarifa feni iliyokuwa inapuliza pale ndani, Joy akaondoa nguo zake na kujifunika na kanga pekee.
Akajilazimisha kulia machozi hayakutoka lakini kuna donge lilikuwa limemkaba kooni.
Ama kwa hakika Joyce alikuwa amefikwa.
Uzito wa roho kadhaa mkononi mapema kabisa ulionekana kumzidia. Ili apate ahueni alitakiwa kuchagua nini cha kutupa na kipi cha kubaki nacho. Joyce alitakiwa kufanya maamuzi ya kuokoa roho mojawapo. Ili asishindane na ule usemi ambao mchumia janga hula na wakwao.
Joy akabaki kuwa mfa maji asiyeisha kutapatapa….
***HATIMAYE JOYCE ana ROHO MKONONI……..roho tatu tofauti……je aiokoe ipi??/
***BETTY hajafanya mapenzi na Isaya lakini tayari ni wapenzi…..
***USIKOSE TENA ….
LIKES, SHARES, NA COMMENTS………kama ilivyo ada….
Post a Comment