RIWAYA: ROHO MKONONI 12


RIWAYA: ROHO MKONONI

MTUNZI: George Iron

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

Nafsi ikamsuta akajiona mjinga sana anayeenda kujichumia dhambi ambayo anaweza kuiepuka.
Joy akaikumbuka ahadi ya Betty kuwa usiku huo ndio usiku wa kumpa zawadi Isaya. Zawadi ya kifo.
Kauli hii ikamsisimua na kumtoa katika pumbazo Joyce. Nguvu ya mapenzi ikamtekenya, ni kweli alikuwa anampenda sana Isaya, na sasa alikuwa anabariki mauaji haya ya maksudi.
Upendo gani wa kushindwa kutetea ukipendacho…
UTATA….
JOYCE akaamua kufanya jambo. Jambo ambalo badala ya kuwa utatuzi wa tatizo, jambo likazua jambo. Roho mkononi zikamzidia uzito, tamaa ya kuzishikilia zote tatu kwa pamoja ikamvuruga akili.

HEKAHEKA

CHUMBA kikubwa chenye hadhi ya kuitwa cha ‘kisasa’ kiliwapokea kwa manukato ya aina yake. Isaya alitabasamu huku akiuzungusha mkono wake katika kiuno cha Betty ambaye sasa alikuwa akimfahamu kwa majina yote mawili, Isaya kama jina la ubatizo na Joram jina maarufu alilopewa na babu yake kipindi cha utoto.
Betty naye aliuchanua uso wake kujibu tabasamu la Isaya. Mlango ukafungwa na Isaya, kisha wakakumbatiana na kupeana mabusu mashavuni na kisha katika papi za mdomo.
Wakaketi kitandani, kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita na kisha kuanza kupongezana huku wakipeana michapo ya hapa na pale iliyokuwa inatokea ukumbini wakati wa sherehe.
Mvinyo waliokuwa wamekunywa ulikuwa umewachangamsha haswaa. Na kila mmoja alikuwa muongeaji. Mvinyo huu ukawafikisha hatua ya kutamaniana, kwa Isaya hii ilikuwa nafasi hadimu aliyokuwa anaisubiri. Lakini kwa Betty ilikuwa hadimu zaidi maana alikuwa anaendeleza safari yake ya kuwakomesha wanaume na kisha kujinufaisha yeye kwa ajili ya kisiwa alichozaliwa.
“Tukaoge kwanza…” Betty alimwambia Isaya ambaye alikuwa ameanza kumzongazonga akimvuta kitandani. Isaya akacheka kidogo baada ya kugundua kuwa Betty ametambua nini kinachotaka kuendelea.
Isaya akaondosha baadhi ya nguo zake kisha akamsaidia Betty pia, kisha wakajongea katika bafu kubwa lililozungukwa na marumaru inayovutia machoni.
Waliingia bafuni bila kuufunga mlango, hii iliwasaidia kuweza kuisikia simu ya Isaya ilivyokuwa inaita.
Kwa jinsi Isaya alivyoweka milio yake kwa ajili ya watu maalum basi hakuhangaika kujua kuwa ni mzee wake anapiga.
“Mzee huyo, hapa hatachelewa kuanza kutoa semina zake za mara tuwe makini sijui nini dah! Wazee wa zamani oooh!!” alilalama Isaya wakiwa hawajaanza kuoga.
“Kapokee simu mpenzi.” Betty alimchombeza.
Isaya akaondoka huku Betty akimtazama mwanaume yule ambaye yupo njia ya kuzimu akisubiri usafiri wa kwenda huko.
“Eeeh unasema….nini?......Haiwezek…..sasa kwa hiyooo!!” alisikika Isaya akibwatuka katika simu bila utulivu, Betty akajisogeza hadi mlangoni na kumtazama mpenzi wake yule ambaye walikuwa wamevishana pete muda mchache uliopita.
Isaya hakurejea bafuni tena, alimsisitiza Betty naye avae waondoke eneo lile. Hakuweza kujieleza zaidi nini kinatokea lakini alionyesha kupagawa sana.
Betty akatii alichoambiwa, akasimama na kuvaa nguo zake upesiupesi kisha wakatoka huku wakitoa taarifa kuwa watarejea.
Walivyoondoka hawakurejea tena katiuka hoteli ile.
Huu ukawa mwanzo wa hekaheka!

****

MPANGO wa ujambazi kisha mauaji ya kutisha hii ndiyo ilikuwa habari iliyozungumzwa katika simu ya bwana Akunaay Zingo kwenda kwa watu wake wa karibu. Wakati huo akiwa ameanza na yule wa karibu zaidi.
Usingizi uligoma kabisa kushirikiana naye kitandani. Alijiuliza ni nani hawa wa kutaka kumvuruga akili yake kwa kushiriki katika kumvamia mwanaye. Kitu cha kwanza alichojiuliza na kuhisi ni usahihi mtupu ni juu ya zawadi ambazo Isaya na mwenzake walipewa na wageni waalikwa.
Aliamini kuwa hili liliwavuta sana vibaka ama majambazi na kutaka kugawana na mwanaye zawadi hizo. Jambo ambalo hakuwa tayari kuona likitokea.
Haraka akachukua simu yake na kubonyeza namba za maaskari fulani ambao walikuwa wanamuheshimu sana. Akataka kupiga namba zao lakini akajiona mpuuzi wa kwanza kabisa kupata kutokea.
Yaani awaelekeze polisi kwenda kuulinda uhai wa mtoto wake mkubwa? Wakati na wao wanalinda uhai wao….
Hapana! Akapingana na shauri hili, akajikita katika mtazamo wa mzazi ndiye awezaye kumlinda mtoto wake kwa moyo wote na si askari ambaye ataleta habari ya tulirushiana risasi wakatushinda tumeua mmoja lakini mtoto wako alipigwa risasi.
Hii itakuwa na maana gani kwake sasa. Isaya atakuwa marehemu wakati taarifa hii ikitolewa.
Ghafla akabadili maamuzi na kuamua kumpigia Isaya moja kwa moja na kuzungumza naye kama mtoto mdogo anayehitaji uangalizi wa karibu.
Isaya alipokea simu yake akianza na utani kwenda kwa baba yake. Bahati mbaya hakujibiwa chochote badala yake mzee Zingo alikuwa ametaharuki na alitoa taarifa ya mapema sana na iliyotakiwa kufanyiwa kazi mara moja.
“Ondoka katika hoteli hiyo, sasa hivi, unajua maana ya sasa hivi…nasema toka hapo upesi kijana wangu, kuna mambo ya hatari yamepangwa juu yako. Fanya hima mtoto. Usiwaeleze chochote hao wahudumu wa hapo, ondoka Isaya ondoka sasa hivi” Mzee alisihi sana huku akijisahau kuwa Isaya hayuko peke yake bali yupo pamoja na msichana wake ambaye ametoka kumvalisha pete.
Ni simu hii iliyozua hekaheka katika chumba alichokuwa ametegemea kulala Isaya pamoja na Betty.

Wakatoweka upesi wawili hawa bila kuwaeleza wale wahudumu wa hoteli ile juu ya taarifa ya hatari waliyopewa.

****

KADRI muda ulivyozidi kwenda ndivyo Joy alizidi kuumia, aliamini kuwa hakuna alichofanya kwa ajili ya kumsaidia Isaya wake. Akajigalagaza kitandani huku akiugulia maumivu makali ya nafsi, machozi yakaunda unyevuunyevu katika shuka lake huku yakiacha michirizi mashavuni lakini kubwa zaidi yakiweka maumivu moyoni. Maumivu yasiyostahimilika katu!
Alipoitazama saa yake ulikuwa ni usiku mnene haswaa.
Mara akashtuliwa na simu yake. Nani wa kumpigia simu usiku huo.
Alipoitazama aliona namba mpya!!
Mtego!! Akahisi lakini akajikosoa baada ya kukumbuka kuwa namba yake hiyo hakuitumia hapo kabla katika kufanya jaribio.
Akaipokea simu bila kusema chochote.
“Joy mama mbona makubwa huku, yaani ni hatari roho zetu mkononi kuna watu wanazisaka jamani mwee! Nakuja nyumbani kwa kweli mi staki mjadala hapa.”
“Kuna nini lakini?” aliuliza Joyce katika namna yua mshangao.
“Nakuja Joy mamangu nakuja nitakusimulia bora nifie mikononi mwako mwenzangu.” Alijibu Betty kisha akakata simu.
Joyce akajikuta akiunda tabasamu hafifu kidogo, ujio wa Betty kidogo ungeweza kumrejeshea faraja na pia kujikuta yu katika mapambano hai.
Aliamini fika kuwa iwapo Betty hakufanikiwa siku hiyo basi amempatia muda wa kujipanga upya. Na kupambana naye kwa kila hatua.
Baada ya saa zima Betty alifika akiwa amepagawa.
Hata kabla ya salamu akamsimulia Joyce juu ya simu ambayo alipigiwa Isaya. Simu iliyotoa ujumbe hatari unaokaribia kumaanisha kifo.
Joyce alifanya igizo la kusikitika, kisha akamliwaza rafiki yake huyo apumzike watazungumza asubuhi.
Baada ya Betty kusinzia, Joy alifanya tabasamu jingine. Kisha akajipongeza kwa uamuzi wake aliofikia dakika za mwisho kabisa kumpigia simu baba yake Isaya kwa namba tofauti kabisa na ile ambayo walibadilishana siku ambayo alionana naye mara ya kwanza nje ya ukumbi wa Nkrumah.
Simu hii ilibeba ujumbe mfupi lakini ulionyooka, ulikuwa ni uongo uliotungwa ukatungika na mzee Akunaay Zingo akauvaa mkenge.
Karata aliyocheza Joyce ikawa karata sahihi kabisa ya kumwokoa Isaya.
Mpambano huu wa kwanza Joyce akaibuka kidedea, japo alizua hofu baina ya nafsi kadha wa kadha lakini ni heri hofu kuliko uhai kupotea kirahisi. Uhai wa mwanaume ambaye anampenda kwa dhati.
Kuanzia usiku huu Joyce akajiapia kwamba ameanzisha vita ya kimya kimya dhidi ya mahusiano ya Betty na Isaya.
Joyce alikuwa na nia moja tu katika mapambano haya, alihitaji kumlinda Isaya asiukwae Ukimwi na kisha baada ya miezi mitatu akiwa amemaliza mitihani yake aweze kumtamkia bayana kuwa alikuwa akimpenda nab ado anampenda haswa.
Kwa wakati uliokuwepo alihofia kuchanganya mambo, iwapo tu Isaya atamjibu vibaya basi atavurugika kiakili na kuyumba kimasomo. Joy hakuwa tayari kwa anguko hili. Hivyo akapendekeza kuwa akimaliza mitihani yake ya mwisho utakuwa wakati muafaka wa kumweleza Isaya jambo kuu kama lile.
Usiku huu ukamalizika huku nafsi ikiwa katika amani.

ASUBUHI ambayo ilianzisha siku nyingine, Joyce alianza kujiweka karibu sana na Betty huku akitaka kujua mambo yake mengi kuhusiana na Isaya. Alifanya hivi ili aweze kuzijua vyema ratiba za wawili hawa kila zinapotokea.
Joyce alifurahia sana ile hali ya Betty kutojichanganya na wanafunzi wa chuo, hii ilimsaidia kumweka mbali juu ya ufahamu wa Joyce kujihusisha na Isaya kabla hajaamia kwa Betty. Wanachuo wengi walilijua hili lakini wangeanza vipi kumweleza Betty iwapo hana mazoea nao na ilikuwa nadra sana kuonana naye?

****

ZILIPITA siku tano bila Betty kuonana na Isaya japo waliwasiliana mara kwa mara kwa njia ya simu. Betty hakuwa akilala nyumbani na kupumzika kama alivyodhani Isaya na badala yake alikuwa akiongeza mtaji wake kwa vibopa wengine wenye pesa zao.
Siku ikawadia ya Betty kuonana tena na Isaya. Bila kujua Joy ni adui yake ndani ya nafsi kwa sababu ya Isaya alimweleza kila jambo lilivyo, muda na mahali ambapo watakutana na Isaya.
“Yaani huyu mkaka anaulilia ujira wake hadi namwonea huruma ati.” Alisema Betty huku akifanya maandalizi ya mwishomwisho kwa ajili ya kwenda kukutana na Isaya.
Joy alijilazimisha kutabasamu bila kusema neno lolote lile. Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi tena. Alikuwa anaingia tena katika vita ya aina yake, safari hii alikuwa hajajipanga kabisa japo awali pia hakuwa amejipanga kwa shambulizi lile.
Betty akaaga huku akimweleza Joy kuwa atakuwa akiwasiliana naye mara kwa mara kwa kila hatua atakayokuwa amefikia.
Joy alibaki nyuma akiumiza akili yake ni kitu gani anaweza kufanya ili aweze kumwokoa tena Isaya na janga hilo lililokuwa likielekea kumkabili.
Akili ilizunguka sana bila kupata suluhisho, hofu nayo ikazidi kumwandama.
Joy akatamani kumweleza Betty hata kwa njia ya simu juu ya utaabani wake juu ya penzi la Isaya, alitamani na angeweza kufanya hivyo lakini alijionya mengi sana ambayo yakakifanya kichwa chake kiume haswa.
Alikosa maamuzi!!
Mara akaamua jambo moja ambalo lilikuwa zito kukubaliana nalo kama litaweza kufanya kazi lakini aliamua kujiaminisha

***ISAYA na BETTY tena…..je watanusurika safari hii…
***JOYCE anakosa maamuzi…maamuzi sahihi ya kujitoa katika mpambano huu wa aina yake…..je atafanya nini…
***BETTY hajui nini kitakachotokea…..

ITAENDELEA 

Post a Comment

Previous Post Next Post