RIWAYA: ROHO MKONONI 8

RIWAYA: ROHO MKONONI


MTUNZI: George Iron

SMS: 0655 72 73 25

SEHEMU YA NANE

JOYCE alikosa cha kujibu kwa usiku ule, akatamani kumshauri Betty walale kwanza huku akifikiria nini cha kujibu lakini akajikanya kuwa huyu Betty hakufikiria mara mbilimbili wakati anaamua kufanya mapenzi na mwalimu Japhari ili aweze kupata pesa kwa ajili yake. Kumbukumbu hii ikampa ujasiri..akakifungua kinywa chake.
“Betty, nadhani unafahamu kuwa sina uwezo wa kusema hapana kwako, nadhani unajua kuwa wewe ni zaidi ya mwandani wangu, sina kipingamizi, kama ambavyo sikunyanyua kinywa changu kumshirikisha mtu yeyote juu ya mahusiano yako na mwalimu, basi hivyo hivyo sitapoteza hata sekunde moja kumshirikisha mtu yeyote juu yako. Kwa hili NAAPA!!” Alisema Joyce kwa ujasiri huku akimtazama Betty machoni moja kwa moja akimaanisha kuwa kile ambacho anakiongea anamaanisha na wala hatanii. Betty akavutiwa na jibu hilo, alitegemea elimu ya Joyce itakuwa imeanza kumbadili lakini la haikuwa hivyo. Joyce alikuwa yuleyule.
“Ehe na wewe nambie uliunga unga vipi hadi kufika huku maana sikuamini siku nilipoona jiba lako katika mtandao kuwa unajiunga na chuo hiki, hakika nilistaajabu. Sikuwa tu na mtu yeyote kule Lilongwe ambaye alikuwa anakufahamu hivyo sikuwa na wa kumweleza kuwa pacha wangu amefikia elimu ya chuo kikuu.” Aliuliza kwa shauku, Betty.
“Mhhh! Kwanza nimalizie wewe ulipoteaje pale Makambako jamani watu wakaanza kusema umekufa, wee nililia sana, mara Dulla naye akajinyonga yaani nd’o nikachanganyikiwa mimi.”
Hapa Betty alitabasamu kidogo kisha akajisemea mwenyewe, “Mwanaume pekee niliyemuua kimakosa ni Dulla waliosalia wote ni haki yao, watajuta kuzaliwa wanaume na tamaa zao” Baada ya kujisemea akaendelea kuzungumza tena na Joyce, akaipandisha sauti juu kidogo.
“Hofu, aibu, mawazo, na uoga wa kifo humfanya mgonjwa wa Ukimwi kujihisi anakufa kesho yake, hapa sasa hujikuta akiteswa na hivyo vitu vitatu hasahasa mawazo na uoga wa kifo. Hapa sasa mgonjwa huonekana kama aliyezidiwa tayari na anakufa muda wowote.” Ni hivyo daktari aliwaeleza ndugu zangu wa kule Makambako. Kisha wakawasihi wanipeleke mbali kabisa na Makambako ambapo nitapotelewa na ‘aibu’ kwa sababu hatakuwepo mtu anayenitambua, pia mawazo yatapungua kutokana na mazingira mapya.

Betty alisimulia jinsi alivyosafirishwa hadi Malawi kwa mganga wa tiba za asili. Akapewa tiba za kiasili kwa juma moja akinyweshwa madawa makali makali asiyoyajua majina yake. Madawa ambayo yalimsaidia haswa. Kisha akasafirishwa hadi Lilongwe mji mkuu wa Malawi, huku ndipo akaanza huduma za kisasa. Ushauri wa daktari ulipozingatiwa Betty akanawiri tena. Alitamani sana kusoma lakini ilimlazimu kuanza upya tena jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya, basi akabaki kuwa msaidizi tu nyumbani kwa huyo aliyeambiwa kuwa ni ndugu yake.
Maisha yalikuwa ya wastani na familia ilikuwa na furaha tele, lakini Betty hakuridhika kabisa kuishi na kufia utumwani, hapo likamjia wazo la kutoroka. Alikutana na mwanaume kutoka Tukuyu Mbeya, katika orodha huyu ndiye wa kwanza. Akampamba Betty kwa maneno matamu. Betty akaomba kitu kimoja tu, awezeshwe kufika Tukuyu ama Mbeya mjini iwapo itawezekana.
Mnyakyusa akaingia mtegoni. Betty akatoroka nyumbani, akiwa na fikra moja tu kichwani mwake, fikra ya kufia nyumbani na si ugenini kiasi kile hata kama alikuwa akipendwa vipi, bado aliamini kuwa yeye ni marehemu wa wakati wowote. Basi kwa kitendo cha mwalimu Japhari kumpa pesa baada ya kumwambukiza Ukimwi basi alihitaji ‘ka-mchezo’ kaendelee.
Ule Ukimwi aliopewa na mwalimu yeye akaamua kuufanya kitega uchumi. Betty akaamua kuuza Ukimwi kwa manufaa ya kisiwa cha Ukala.
Kutokea Tukuyu, baada ya mnyakyusa kulipia pesa nyingi ule Ukimwi ambao alipewa katika nyumba za kulala wageni mjini Mbeya. Betty akaamua kusafiri kwenda Dar.
Alifanya hivi akiamini kuwa pesa na kila wanaume punguani waliovurugwa na pesa wapo jijini Dar es salaam.
Sasa yupo Dar, yupo na Joy na amemweleza kila kitu na amekubaliwa.

Joyce akashusha pumzi baada ya Betty kusimulia.
Kwa upande wake hapaukuwa na longolongo nyingi, alifaulu kwa kiwango cha juu kidato cha nne, mkuu wa shule akaitisha mkutano wa wazazi na wanakijiji wengine, harambee ikapitishwa kwa Joyce na wanafunzi wengine wawili waliofaulu kujiunga na kidato cha tano. Pesa ikapatikana ya kutosha wakaingia shuleni bila mashaka yoyote.
Hata safari ya kwenda chuo kikuu haikuwa ngumu, serikali ilikuwa inatoa mikopo. Na bado mkuu wa shule aliendelea kuhitisha mikutano mara kwa mara hadi Joyce pekee akiwa kati ya wanafunzi watatu kutoka Makambako waliofaulu kidato cha sita na kuingia ngazi ya chuo kikuu.
Wakati Joyce anamaliza kusimulia Betty alikuwa amesinzia tayari, bila shaka hakusisimuliwa na maelezo yale ama la! Alichoka. Hivyo Betty hakupata nafasi ya kusikia juu ya Joy kugombea ‘urembo’ wa chuo, jinsi wanafunzi walivyomtunuku pesa kuonyesha kuwa wanapingana na matokeo yaliyotajwa, akajitokeza mdau mwingine na kuahidi kisha kumnunulia Joyce Kidoti ‘laptop’…..

****

MACHO ya wasichana walimbwende haswa kutoka chuoni yalikuwa yakistaajabishwa na hali ya sintofahamu iliyokuwa inaendelea kati ya mwanafunzi aliyekuwa na pesa na pia majivuno huenda kuliko wanafunzi wote wa chuo hicho kikuu na msichana aliyesadikika kuwa ni mrembo aliyeshinda taji lakini akachakachuliwa na wajanja. Kwa ufupi ilikuwa ni sintofahamu kati ya watu maarufu chuoni hapo.
Walikuwa waeneo ya Mabibo Hostel, eneo maarufu kabisa kwa wapendanao ‘Block G’.
Kwa mtazamo wa macho ilionyesha kabisa kuwa msichana alikuwa akipingana na yule mvulana, mtoto wa mbunge wa Geita. Isaya Akunaay, hali ile iliwatia hasira wasichana ambao walitamani sana kuwa katika mahusiano na watu maarufu na wenye pesa zao.
Kila msichana wa kisasa angeweza kutamani kuwa na Isaya Akunaay, si tu kwa sababu alikuwa na pesa la! Alikuwa mtanashati pia, jamari wa sura ana umbo.
Vipi kuhusu Joyce? Mbona kama hana dalili za kushawishika!!! Hiyo ikawa sintofahamu kuu.

“Isaya…unanirudisha hostel ama nikapande daladala.” Alihoji Joyce huku akirusha mikono huku na kule.
“Nisikilize kwanza nd’o nitakurudisha kama hunisiki…”
“Kaka, sitapanda gari yako nimeghairi, nitapanda daladala. Naomba niende tafadhali.” Sauti ya Joy ilishuka chini sana, hii hutokea akiwa amekasirika sana.
Isaya alidhani Joyce alikuwa anatania, mara yule msichana akasimama wima….
“We Kidoti…Kido….” Hakumalizia kauli yake, binti akarusha mikono hewani kumaanisha kuwa hataki kusikia lolote kisha kwa mwendo wake uleule wa kilimbwende akatoweka machoni.
Isaya akabaki ameduwaa, hakika aliduwaa na ilikuwa mara yake ya kwanza.
Mara ya kwanza kudhalilishwa kama ambavyo angeweza kusema yeye iwapo angeulizwa.

Wapambe wake waliokuwa ndani ya gari la Isaya walilitazama tukio lile katika hali ya mshtuko pia, hawakutarajia kuona walichokiona. Wakapigwa na bumbuwazi na hata Isaya alipoingia ndani ya gari hakuna aliyemuuliza kitu.
Mpambe akawasha gari.
“Nipeleke room.” Aliamrisha. Gari ikatoweka.
Kichwa kilimuuma Isaya.

HAIKUISHIA hapo, mara ya pili walikuwa maktaba wakijisomea, wapambe wakamtonya Isaya kuwa Kidoti alikuwa humo.
Isaya akajibebesha mkoba wake wenye laptop akaingia maktaba. Huko akamfuata tena Joyce katika namna ya kutaka kuendeleza na ombi lake la kumtaka kimapenzi.
Pasipo kutarajia baada ya kuongea maneno mengi sana kwa sauti ya kunong’ona, sasa ulikuwa wakati wa Joyce kujibu. Likatokea jingine ambalo lilimlaza Isaya hoi kitandani siku hiyo bila ugonjwa wowote kichwani.
Joyce akaandika katika kikaratasi na kukisukuma kwa Isaya Akunaay. Mtoto wa mbunge anayejihisi kuwa nay eye ni mbunge.
“DON’T MAKE NOISE IN THE LIBRARY…..haukusoma pale mlangoni??” maandishi yalisomeka hivyo. Isaya akabaki na kile kikaratasi huku akitazama kama kuna mtu yeyote ameona wakati akisukumiwa, akakikunja kunja. Akataka kusema neno lakini Joyce hakuonekana kuwa tayari kusikiliza chochote kile.
Karata hii nayo ikagonga mwamba!! Isaya akazidi kuchanganyikiwa, mapema akalala fofofo mchana, kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya chuo.

Jaribio la tatu lilikuwa shukrani alizopeleka kwa Joyce kwa kumsaidia kuipata ‘laptop’ iliyokuwa imepotea maktaba. Isaya aliamini shukrani pekee ni pesa, akamtumia Joyce kiasi cha shilingi laki mbili kama shukrani.
Hapa napo mambo yakawa yaleyale na akili yake ikazidi kuduwaa. Pesa ilirudishwa bila kupungua hata noti moja.
“Amesema haukutangaza dau lolote kwa atakayefanikisha kupatikana kwa laptop nd’o maana aliamua kwa moyo wake tu!!” kauli hii ikamchanganya Isaya japo alikiri kuwa Joyce alisema ukweli kabisa. Akazipokea pesa zake kinyonge.

Kuanzia hapa hakufanya papara tena, akajifanya hana haja na Joyce tena. Lakini moyoni akikiri kuwa wale wasichana wote aliowapata zamani kwa kutumia jeuri ya pesa zake hawakuwa na ladha na hawakumkaa akilini kabisa, alifanya nao mapenzi na kuwaacha mara moja. Wengine walimlilia lakini hakujali, lakini sasa akakitambua kilio chao kilivyokuwa na maana kubwa na kikiwaachia jeraha la aina yake.
Jeraha la hisia!!
Sasa jeraha hili likaanza kumtambaa nay eye pia, akajikuta akimuhitaji sana Joyce kuliko yule mtoto wa raisi wan chi ambaye alimkataa kimapenzi.
“Kumbe pesa sio kila kitu eeeh!!” aliwaza Isaya kisha akamalizia, “Kipi sasa ni kitu zaidi ya pesa jamani.” Hakuwepo wa kumjibu.
Tabia ya Isaya ikabadilika, akawa mtu wakulala tu, kila alilolifanya aliona haliendi sawa iwapo kuna msichana alimuhitaji na hakumpata.
Mara akaanza kudhoofika. Hili likawashtua rafiki zake nay eye mwenyewe pia. Alidhoofika kwa sababu ya kuwaza juu ya jeuri ya Joyce , alijiuliza nani anayempa kiburi.
Msako ukaanza ili amjue mwanaume ambaye anampa kiburi Joyce, akishampata ndipo atajua nini cha kumfanya ama uamuzi gani wa kuchukua.

*****

WAKATI huu Joyce alikuwa amehamia chumba chake mwenyewe nje na chuo, huku alikuwa akiendelea kuishi na Betty ambaye alikuwa kazini katika namna ya kipekee, kama alivyosema awali. Hataki mwanaume njaa anayetegemea mkopo wa serikalini utoke ndipo aanze mbwembwe zake chuoni, ama mwanaume shida anayetegemea wazazi wapate mishahara yao midogo wamtumie pesa za matumizi.
Betty alikuwa anahitaji wale wanaojiita watoto wa ‘misheni tauni’. Wenye pesaa zao bila kujalisha ni wapi walipozitoa. Cha msingi wasiwe na mikono ya birika, wajue kuhonga. Na kwake yeye ilikuwa lazima wahonge, hakuwa msichana wa kutongozeka kikawaida kawaida.
Alikuwa kikazi zaidi, na katika kazi yake hiyo alikuwa makini mno.
“Vipi jamaa keshaacha kukusumbua siku hizi…maana kimyaa au ndo tayari na wewe…ushadata.” Betty alimchokoza Joy wakiwa kitandani.
“Aaargh asingeweza kunipata kirahisi, ameuchuna siku hizi aibu kwake…ananitishia mimi pesa ananitishia majivuno.” Alijibu Joy kwa jeuri huku akiibetua midomo yake.
“Na hicho kidoti wanakomaje!!!”
Wakacheka kwa pamoja!!!
Mara simu ya Betty ikaita akaipokewa, alikuwa bwana mmoja mfanyakazi wa benki.
“Mi natoka shoga!!.” Alimuaga Joyce wakati anajiandaa kwenda kwa bwana mwingine.
“Huyu ananipa laki tano leo, nakaribia kufikisha milioni nne dah safi sana. Na roho saba zipo rehani tayari pumbavu zao.” Alibwabwaja huku akitangaza chuki ya waziwazi.
Akaondoka zake!!!

***ISAYA AKUNAAY ameamua kumkabili Joyce Kidoti Keto katika namna nyingine….JE KWELI YUPO MWANAUME anayempagawisha JOYCE….nini kitajiri …..

***BETTY yupo kazini na hana utani….je atatimiza azma kabla UKIMWI haujammaliza…..

ITAENDELEA KESHO.

NB: Kwa mara nyingine kompyuta imeanza kuzingua……

Post a Comment

Previous Post Next Post