Na Elias Msuya
Juni 26 mwaka huu ilikuwa ni siku ya
maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani. Maadhimisho
hayo yalifanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na
wadau wa janga hilo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
aliyemwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema wafanyabiashara wa
dawa za kulevya ni watu hatari na kwamba, wanaweza kuingilia misingi ya
kiutawala, hivyo Watanzania hawana budi kuipiga vita kwa nguvu zote.
Alisema iwapo biashara hiyo haitadhibitiwa
kikamilifu na kuachwa ikaendelea moja ya athari zitakazojitokeza ni
kuingiliwa kwa misingi ya utawala na ongezeko kubwa la rushwa.
Kauli hii inaonyesha kuwa Serikali imekata tamaa
katika mapambano ya dawa za kulevya nchini. Tulitarajia Serikali
ingetangaza mafanikio ya mapambano hayo, siyo takwimu tu za tatizo. Kwa
mfano kama Lukuvi anakiri kwamba biashara hiyo inawagusa watendaji wa
Serikali, basi watajwe na wachukuliwe hatua hadharani.
Hali hiyo inajitokeza wakati kukiwa na ongezeko la Watanzania wanaokamatwa kwa kujihusisha na biashara hiyo.
Kwa mfano katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012,
watuhumiwa 10,799 walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na biashara hiyo
nchini, huku Watanzania 240 wakikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan
na Afrika Kusini na baadhi wamefungwa.
Taarifa ya Serikali inaonyesha pia kuongezeka kwa
tatizo hilo hadi ilipofika mwaka 2010 ambapo kilo 914 za dawa za kulevya
aina ya heroin, zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia uharamia nchini.
Tumeshuhudia pia viashiria vya matumizi ya dawa za
kulevya nchini hasa kwa wasanii wa muziki na michezo mingine. Ni hivi
karibuni tu kulikuwa na kifo cha utata cha msanii Albert Mangwair
aliyefia nchini Afrika Kusini huku ikidaiwa kuwa alikuwa na ‘mzigo’
tumboni.
Kifo chake kilifuatiwa na msanii mwingine wa muziki wa kizazi kipya, Langa Kileo ambaye naye aliathirika na dawa hizo.
Msanii mwingine aliyeathirika na dawa za kulevya
na sasa anapatiwa matibabu kwa ufadhili wa Rais Jakaya Kikwete ni Rehema
Chalamila.
Kama hiyo haitoshi, tumeshuhudia hukumu ya miaka
15 aliyopewa mwanamichezo wa ndondi, Petro Mtagwa na watu wengine watatu
waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroin nchini Mauritius.
Hao pamoja na wengine wengi wanaonyesha kuwa janga
hili ni kubwa mno. Hata hivyo nina wasiwasi na hatua zinazochukuliwa na
Serikali yetu.
Mwananchi
Mwananchi
إرسال تعليق