SIMULIZI FUPI: USIKU USIO NA JINA
MTUNZI: FARIDAH KHALFAN
MAHALI: MOROGORO
SIMU: 0656 317970
NDEGE wa angani pekee nd’o walikuwa wakiendelea kulipa uhai anga lililotanda kwa giza nene huku nyota zikishindwa kufua dafu katika kuileta nuru. Anga lilipoanza kutoa miale mikali inayong’ara, ndege walivikumbuka viota vyao na makundi kwa makundi walitoweka anga ikabaki katika hali ya upweke, miale mikali pekee nd’o uhai mdogo uliosalia.
Miale hiyo haikuishia kuleta uhai katka anga pekee, bali ulimurika pia katika chumba kimoja ambacho kilikuwa kimekaliwa na mwanamke. Alikuwa amevaa nguo za kulalia, macho yake yakiwa makavu. Taa ilikuwa imezimwa hivyo ule mwanga ukaibua undugu kati ya macho na sasa.
Ilikuwa yapata saa tisa usiku. Yule bwana aliyemuoa kwa mbwembwe zote na mapenzi miaka miwili iliyopita alikuwa hajarejea nyumbani bado.
Ni kweli alikuwa ameanza tabia za kuchelewa nyumbani lakini siku hii alipitiliza.
Mwanamke akakunja uso wake kwa uchungu mkuu, akajiziba na viganja vya mikono yake. Akatambua kuwa amebanwa na donge la hasira kooni na hawezi kulihimili mpaka atoe kilio. Hapo akaamua kutimua mbio kuelekea chumbani kwake. Akafika akaduwa chumbani kwake huku akitiririkwa na machozi. Akaliendea kabati la nguo ili aweze kuchukua kitambaa atumie kukabiliana na machozi yale.
Mara paah! Kikaanguka kitu kikilia mfano wa sarafu, akainama kutazama ni kitu gani. Hofu ikazidi kutanda.
Ilikuwa pete ya ndoa, pete ambayo kwa mikono yake alimvisha mume wake wakati wanaamuriwa kuwa mume na mke. Pete hiyo imetolewa kidoleni sasa na kufichwa kabatini. Hapa uvumilivu ukamshinda akakimbilia kitandani, akajirusha na kuanza kugalagala huku akilia kilio cha uchungu mkubwa, lakini alijitahidi sana kuizuia sauti ile isipenye na kukifikia chumba kilichokuwa kinafuata, kwani hakutaka huyo mtu katika chumba kile aweze kutambua kuwa alikuwa katika kulia.
Kilio hiki kilikuwa na mengi ndani yake, alijiuliza iwapo huo nd’o ulikuwa uhitimisho wa safari ya ndoa yake, alijiuliza kama hiyo ni talaka alikuwa ameandaliwa kwa vitendo. Kama sio kwanini aitupe pete yangu humu, kwanini anachelewa kurejea nyumbani? Alijiuliza bila kupata majibu.
Mawazo tele aliyokuwanayo yalimfanya asisikie mchakato wowote wa mtu kutembea katika korido kisha kukifikia chumba na kugonga mlango. Mlango ulipogongwa kwa mara ya pili ndipo akili zikamkaa sawa. Akajifuta machozi kwa kutumia shuka, kisha akaenda kufungua bila kuuliza aliyekuwa mlangoni ni nani.
Alitambua tu kuwa lazima atakuwa mumewe na hakika ilikuwa hivyo, mwanamke huyu alimtazama mumewe kidoleni akidhani atakutana na pete na kujitoa mawazo kuwa huenda aliifananisha tu ile iliyodondoka.
Kapa!! Hakuona kitu.
“We Felista…..” mumewe aliita huku harufu ya pombe ikitambaa mle chumbani.
Mungu wangu ameniita jina langu!!
Mwanamke yule alitahamaki, haikuwa kawaida hata kidogo kwa mume wake kumuita kwa jina hilo na badala yake alizoea kumuita mpenzi, mahabuba na majina mengineyo yanayotangaza huba.
Leo hii anamuita Felista!!! Tena we Felista!!
Kama mbwa vile!!!! Mshikemshike.
Felista hakuitika lakini yule mwanaume mlangoni hakujali akapiga hatua moja mbele, hakika alikuwa amelewa na alitaka kukosa muhimili, kama lisingekuwa kabati basi angepiga mweleka na kusalimiana na ile marumaru pale chumbani.
Akiwa ameegemea kabati mwanaume yule ambaye ni kwa mara ya kwanza alirudi nyumbani akiwa amelewa alianza kubwabwaja maneno machafu sana kwa mkewe, maneno ambayo hata Malaya na hawara pia akiambiwa yanaweza kumkera, lakini maneno haya aliambiwa mwanamke wa ndoa iliyobarikiwa kabisa.
Maneno yakazidi mwanamke naye akazidi kukasirika, mwanzoni alipuuzia lakini ikamtoka yule mwanaume kauli mbaya sana ambayo ilibadili usiku ule na kuwa usiku wa kukumbukwa.
Usiku wa sintofahamu na huenda usiku mrefu kupita yote katika maisha yao.
Usiku usio na jina!!!
*****
URAFIKI wao ulianzia ufukweni mwa bahari, Felista na rafiki zake waliokuwa wanasoma shule moja walipokuwa wakicheza na mchanga wa bahari, mara warushiane mchanga mara wamwagiane maji. Mchezo ukiwa umewanogea mara Felista akamponda mwenzake na kiatu chake chepesi, bahati mbaya kusudio lake likashindikana baada ya kiatu kile kukwepwa na mlengwa kisha kikamfikia mwanaume mmoja aliyekuwa ufukweni pia.
Bila kufikiria mara mbili mwanaume yule ambaye labda kwa sababu zake binafsi alikuwa akingoja litokee jambo ili aweze kuwakabili wasichana wale ambao mmoja wao tayari alikuwa amemjibu vibaya alipojaribu kumweleza juu ya mapenzi. Mbio mbio mwanaume yule akaenda kumkabili Felista ambaye alikuwa ameduwaa akiwa amejiziba midomo yake kwa mshangao mkubwa.
Mwanaume yule akamfikia Felista na kuanza kumkaripia pasi na kumpa nafasi ya kuomba msamaha ama kujieleza vyovyote vile. Felista aliyekuwa anatetemeka alimuona mwanaume mwingine akijongea mahali pale.
“Frank, acha hasira kaka. Mtoto wa kike huyu halafu si unaona watu wanavyokushangaa…..jifanye hakijatokea kitu. Halafu na wewe binti waambie wenzako kama michezo mkafanyie mbali, si unaona hapa watu wamekaa sawa eeh!” sauti ilisihi. Yule kijana aliyekuwa anazidi kupandwa za jazba akapiga kite cha hasira kisha akakubaliana na yule rafiki aliyemsihi.
Felista na rafiki zake wakatafuta eneo jingine, si kwa minajiri ya kucheza tena la! Kila mmoja kuvaa nguo na kutoweka. Ufukwe ushakuwa gundu tena.
Wakati wanaondoka pale, Felista alimwona yule kijana aliyewasuluhisha baada ya yule kijana mjeruhiwa wa ajali ya kiatu kumkabili.
“Asante kaka.” Alimwambia baada ya kumkaribia.
Wakazungumza kidogo kisha wakati wanaagana kwa kushikana mikono akasikia kama kuna kitu anapewa mkononi, akaufunga mkono vyema kisha akaondoka na rafiki zake.
Alipoufungua mkono baada ya kufika mbali alikutana na kadi ya biashara ikiwa na namba za simu na eneo la ofisi zinapopatikana.
Bahati nzuri ofisi za huyu msuluhishi zilikuwa zinahusika na jambo ambalo Felista alikuwa akisomea katika masomo yake chuo kikuu cha Dodoma. Hivyo alimtafuta kwa lengo la kuulizia kama ataweza kupata nafasi ya kufanya mazoezi yake kwa vitendo katika ofisi hizo. Huo ukawa mwanzo wa mazoea yao, kisha urafiki na baada ya kumaliza chuo walikuwa wachumba.
“Nakupenda Gervas.”
“Nakupenda Felista”
Maneno haya waliambizana kwa mara ya kwanza mjini Dodoma. Yakadumu hadi walipofanikiwa kufunga ndoa.
Ndoa iliyobarikiwa na pande zote mbili bila kinyongo chochote kile. Kila mmoja akiwa amemuelezea mwenzake juu ya siri zake na historia za miaka ya nyuma bila kificho.
Maisha ya ndoa yakaanza rasmi!
Upande wa mawifi palikuwa shwari kabisa na hata mashemeji walimpenda Felista naye alijitahidi kuwapenda pia.
MIAKA miwili ikakatika upendo ukaanza kupooza, ulipooza kwa sababu Felista alikuwa hajaongeza zao lolote katika ukoo wa Gervas wala katika nyumba waliyokuwa wanaishi jijini Dar es salaam.
Gervas aliahidi kuwa atavumilia mpaka mwisho, neno hilo lilimpa faraja sana Felista, akajipa imani kuwa akipata upendo wa mumewe basi hawa wengine wanabaki kuwa wa ziada tu. Hakuumiza kichwa kuhusu wao.
Lakini alitilia maanani ule usemi usemao, ‘damu nzito kuliko maji!!’ na hapo akakumbuka kuwa mume wake si ndugu yake wa damu na hakuna damu yoyote ambayo inawaunganisha. Akajiwekea tahadhari hii kichwani.
HAKIKA baada ya mwaka mwingine, mume wake akaanza kubadilika, akawa anawasikiliza dada zake sana, kuna maneno fulani hivi ambayo japo Felista hakuwa anayafahamu lakini aliamini maneno hayo ndiyo chanzo cha kila kitu kuwa shaghalabaghala. Akajaribu kujiimarisha ili aweze kuwa kinara katika nyumba lakini haikuwezekana kabisa tayari wale wana’damu’ moja walikuwa kitu kimoja.
Alitamani kuikimbia nyumba lakini asingeweza kurudi nyumbani bila kupewa talaka, akatamani kuiomba talaka yake lakini kibaya zaidi mume wake hakuwa amewahi kumtamkia kuhusu talaka hata siku moja. Hili kwake likawa tatizo, akawa anaishi utumwa katika nyumba yake.
Ugeni wa mawifi ukawa haukatika nyumbani kwake, wakifika wanagawana jiko mawifi hawataki chakula cha mama mwenye nyumba. Wanajipikia wao wenyewe, salamu wanajibu kwa kujilazimisha tu na maisha yanaendelea.
Felista alipomuuliza mumewe akajibiwa kuwa ajitahidi kuwazoea mawifi zake. Hilo nd’o lilikuwa jibu pekee aliloweza kutoa mume, tena katika namna ya kupuuzia tu.
Mawifi wote waliopita walikuwa micharuko na wasumbufu lakini wifi aitwaye Sarah huyu alikuwa wa aina yake alionyesha ushirikiano wa hali ya juu kwa Felista, alimsaidia kazi za ndani na kuna wakati walipika wote jikoni. Alimpa moyo kuwa hiyo anayopitia ni mitihani tu kutoka kwa mwenyezi Mungu na ipo siku itapita na maisha yataendelea.
Wifi huyu wa ajabu, kila walipokuja mawifi wakorofi yeye alikuwa akijiondokea kabla hawajafika. Jambo hili lilimshangaza sana Felista lakini moyoni akaamini amepata shujaa wa kweli wa kumpigania, aliamini kuwa wifi yule anawachukia na kuilaani tabia wanayofanya wadogo zake. Hata ambapo wifi yule hakuwa ndani ya nyumba yake, alikuwa akimpigia simu usiku na wakati wowote ule kwa lengo la kumfariji, alimueleza kila kitu kilichokuwa kinatokea. Alijaribu kumsihi aongee na kaka yake ili aweze kuwa kama zamani, wifi Sarah akakubaliana na Felista na kumwahidi kuwa ataongea na kaka yake vizuriu kwa kina juu ya hilo.
Hakika siku iliyofuata Felista alipokea ujumbe kutoka kwa Wifi Sarah kuwa mambo yanaenda vizuri amemsema kaka yake kwa kirefu na bila shaka amemuelewa.
Juma lililofuata furaha kiasi ilirejea ndani ya nyumba. Felista akakiri kuwa wifi Sarah ni wifi wa kweli kabisa.
Muda ukazidi kusogea na tabia ikawa ileile, wakija mawifi wakorofi na mama mkwe basi Sara anajiondokea. Na maisha yakaendelea.
Baada ya miezi kadhaa wifi sarah alishika ujauzito. Hakumficha Felista alimueleza ukweli kabisa juu ya jambo hilo. Felista alimpongeza huku moyoni akiumia sana na kutamani ile mimba ingekuwa ya kwake, wifi Sarah akaanza kuwa mkorofi, uvivu ukamtawala na akawa mtu wa kulala tu kutwa nzima.
Mimba bwana!!!........ Felista alijisemea huku akitabasamu, aliamini kuwa ni mimba imemfanya kuwa vile wifi yake mkarimu kabisa. Hakutaka kumkera na kila lililokuwa likitokea kwake aliisingizia mimba ya wifi yake.
Mara usumbufu wa mimba ukaongezewa na usumbufu wa mumewe, akaanza tena kuwa mkorofi ndani ya nyumba. Zile tabia zake za zamani zisizotabirika zikaanza kujirudia. Mara akapitiliza zaidi na kuanza kulala sebuleni siku nyingine.
Mara akilala chumbani hataki kuguswa na mkewe, Felista alilia sana lakini nd’o lilikuwa tatizo tayari. Mshauri mkuu alikuwa ni wifi yake lakini huyu naye mimba ilikuwa imemfanya awe mtukutu na msumbufu. Hivyo mchezo ukawa hivi.
Kutwa ni usumbufu na vimbwanga vya wifi na usiku ni karaha za mume wa ndoa. Hapa sasa Felista alikonda barabara. Wazazi wake na ndugu zake wengi walikuwa mkoani Kagera hivyo hakuwa na pa kupumulia, akijaribu sana kuitafuta furaha basi ni siku ambayo alikuwa akienda kutengeneza nywele saluni. Huku aliweza kuburudisha akili yake kwa kusikia maneno ya wanawake wenzao wakipigana vijembe wao kwa wao.
Baada ya kurejea nyumbani zilikuwa karaha tupu.
Hadi miezi tisa ije kumaliziaka nitakuwa nimebakia kama sindano!! Felista alijisemea kwa masikitiko makuu.
Mzigo wa ndoa ulikuwa unamuelemea, afadhali basi angekuwa anafanya kazi mahali walau shilingi mbili tatu zingekuwa katika hifadhi yake lakini hakuwa kazini, mume alikuwa hajamruhusu kufanya kazi bado kwa kauli ya kwamba bado haijapatikana kazi ambayo inamfaa. Mume amesema mke angebisha nini?
Maisha magumu yakaendelea kuishi katika nyumba ya Felista.
MWANZONI Gervas alikuwa anafanya vimbwanga vyote lakini katu hawezi kulala nje ya nyumba yake bila taarifa. Lakini hili nalo likaibuka kutokea pasipofahamika.
Baada ya yule wifi mtukutu kutoweka pale nyumbani na kuonekana kuwa walau nyumba itakuwa na amani kidogo, jambo jingine likazuka. Gervas naye akaanza kuchelewa kurudi nyumbani.
“Afadhali Wifi angekuwepo maana alikuwa anamkaripia akichelewa kurudi….ona sasa” alilalamika mwenyewe huku akiitazama saa ya ukutani. Ilionyesha kuwa ule ulikuwa usiku wa saa nne. Akaendelea kungoja hadi akapitiwa na usingizi.
Siku hiyo alillalasebuleni na mumewe hakurejea kabisa.
Aliporejea siku iliyofuata Felista alijiandaa kumkabili na kupambana naye amweleze alilala wapi. Bahati ikawa mbaya upande wake, mumewe hakumjibu kitu. Alivua nguo zake alizokuja nazo akajitupa kitandani na kusinzia hoi!!
Kizungumkuti hakika!!
Ina maana hatambui tena umuhimu wangu!! Ina maana hakumbuki kama aliwahi kusema atanipenda milele….alijiuliza Felista biula kuupata muafaka.
Mienendo mibovu ikaendelea kuchukua hatamu, ikafikia kipindi Felista akaiomba talaka yake.
Neno hili likamshtua Gervas, hakuwahi kulitegemea. Wakati Felista alidhani kuwa itakuwa kazi rahisi lakini Gervas hakuwa tayari. Akaahidi kubadilika kabisa, akasingizia msongo wa mawazo unamsumbua.
Lakini wakati wote huu kuna jambo ambalo Felista alikuwa akiliona machoni mwa mumewe.
Aliuona uongo waziwazi…uongo usiopingika kuwa kuna kitu anaficha lakini hana mapenzi tena. Hakumpenda Felista.
Hakumpenda kwa sababu alikuwa tasa.
Felista akarudisha moyo nyuma akampokea tena Gervas.
*****
BAADA ya miezi kadhaa, Felista bila kujua kwanini amepata wazo hilo alijikuta tu akifunga safari ya kwenda hospitali kwa mara nyingine kuangalia tatizo lilikuwa nini hadi hapati mtoto. Hakumweleza mumewe kama ataenda hospitali siku hiyo.
Aliuacha funguo mahali ambapo wote wawili wanafahamu kuwa huwa wanahifadhi. Akaenda zake hospitali.
Akaongea kwa kirefu na daktari, akamweleza hata yasiyomuhusu juu ya namna anavyodharauliwa na fdamilia ya mume wake. Daktari akamchukua vipimo na kuingia maabara. Baada ya hapo akaketi na kumweleza kila kitu juu ya kizazi chake, majibu haya alikuwa akiambiwa kila siku iendayo kwa Mungu na madaktari tofauti tofauti. Lakini huyu kuna moja la ziada alimweleza Felista. Lilimtingisha kidogo Felista lakini alilipokea kwa tabasamu hafifu kana kwamba alilitambua hapo kabla.
Alizungumza sana na daktari. Kisha wakaagana.
Alipofika nyumbani alikuta nyumba ikiwa na uhai, kulikuwa kuna kilio cha mtoto mchanga. Akiwa anastaajabu alipokelewa na tabasamu kali la wifi Sarah. Felista akastaajabu, kumbe ilikuwa imepita miezi lukuki tangu waonane, sasa Sarah alikuwa na kichanga.
Hakuwa mkorofi tena. Hakuwa na tabia zake za kununa. Felista akakiri kuwa ni mimba tu iliyokuwa inamsumbua wifi yake mzuri.
Wakakumbatiana na kubusiana mashavuni. Ilikuwa furaha tena katika familia ile.
Felista alitaka kumshirikisha Sarah juu ya kilichojiri hospitali, lakini akaona ni mapema sana kumweleza mzazi huyu aliyejikita katika kukilea kichanga chake.
FELISTA akafikia maamuzi ya kumweleza mume wake na liwalo na liwe.
Hapa ndipo ukafika ule usiku usiosahaulika kamwe, usiku wa kizaazaa. Ule usiku ambao haukuwa na jina.
Ilikuwa saa tisa usiku ambapo mlango ulifunguliwa, mume wake aliyekuwa amelewa kwa mara ya kwanza akaingia ndani huku akiyumba yumba.
“We Felista wewe….mpuuzi mpuuzi malaya usiyekuwa na nidhamu….ni wewe uliyeniomba talaka yako sio….sasa nasema andika hiyo talaka tasa mkubwa wewe mimi nitaweka sahihi. Andika naachwa kwa sababu sizai, kwa sababu ya umalaya wangu andika upesi wewe changudoa mzoefu….” Alibwabwaja Gervas. Felista akapokea kama pigo kali maneno yale. Hakuamini kama yanatoka kwa mume wake. Akatamani kulia kwa nguvu lakini kifua kilikuwa kinambana.
“…Tena ikiwezekana uondoke usiku huu umwachie mwanamke anayeweza kuzaa nyumba yake hayawani wewe, mwenzako mbona amezaa upesi tu…wewe unanikalishia makalio humu ndani unamaliza sofa zangu kunguru usiyefugika wewe…rudi kwa mama yako mwambie umalaya wako umekuponza na sikutaki tena….hiyo pete yako vua nitamvalisha mwingine.”
AKILI hapa ikamchemka Felista, yaani ina maana wifi Sara amezaa na mume wangu? Alijiuliza.
Halafu ananiita mimi malaya wakati ameniambukiza UKIMWI huyu mwanaharamu!!! Alilaani Felista huku akikumbuka majibu aliyopewa na daktari hospitalini. Hapa sasa ujasiri ukamshinda akataka kuuliza lakini mume akaendelea kuropoka.
“Sara wewe ndiye mke wangu asante kwa bebi boi uliyeniletea…asante sana kwa zawadi hiyo…nakupenda Sara wee…mwaaaah!!” alizidi kubwabwaja kilevilevi.
Felista akalipata jibu kuwa kumbe kuna sintofahamu katikati. Akatazama kushoto akakutana na chupa ya soda. Alairukia kwa hasira akaitwaa na kuituliza katika kichwa cha mume wake, mlevi yule akalainika na kutua sakafuni.
Haikutosha akaendelea kumtwanga nayo hadi akahakikisha mikono imechoka. Kisha mbio mbio akakimbilia jikoni akatwaa kisu.
Akakimbilia chumbani kwa wifi Sara.
“Sara wewe ni nani katika nyumba hii.” Akamuuliza kwa ghadhabu, huku akiwa amekificha kisu chake kwa nyuma.
“Mama mwenye nyumba kwani vipi?” akajibu kwa dharau na hili likawa kosa kubwa sana, laiti angejua angejitetea kuliko kujibu jeuri.
Felista akamvamia na kuzamisha kisu chote mb avuni kwa ujasiri akakichomoa tena na kukizamisha katika chemba ya moyo.
Wifi feki Sarah kimya!!!
Akakitazama kile kitoto kilichokuwa kimesinzia akataka kukimalizia lakini huruma ikamwingia. Akatimua mbio chumbani kwake akakuta Gervas ametulia vile vile.
Akahaha bila kujua ni kipi anafanya pale chumbani. Akajigonga huku na kule kisha akafanikiwa kutuliza akili akachukua pesa katika mifuko ya mumewe, akaongezea na ya kwake kisha akatoweka.
ASUBUHI alikuwa safarini kuelekea Mwanza, akili ilikuwa haijatulia kabisa kutokana na kilichotokea.
Safari nzima aligubikwa na mkasa mzito sana ambao aliamini akimshirikisha mama yake anaweza kupata afueni. Mkasa wa kumfuga mke mwenza akidhani ni wifi yake...
Hakika alifika Mwanza, na kumsimulia mama yake kila kitu. Hakujua na wala hakusema kama alikusudiia kuua.
SIKU MBILI baadaye wakatangaza tukio la mauaji ya kutisha jijini Dar es salaam.
Mwanaume kwa kupondwa pondwa kichwani na chupa, mwanamke kwa kuchomwa kisu na mtoto mdogo kwa kukosa chakula.
Ni taarifa hii iliyoondoka na akili za Felista na kumfanya mwendawazimu milele…..taarifa ya kuhusika katika mauaji ya watu watatu
Mama yake mzazi pekee nd’o aliweza kusimulia mkasa ulivyokuwa kabka mwanaye hajawa na wazimu kichwani, wazimu wa kuvua nguo na kukimbiza watu hovyo. Hapakuwa na la kumshtaki kichaa huyu. Simulizi ya mama yake ikabakia kuwa simulizi inayogusa jamii, hasahasa wanandoa zenye utata na vijana ambao walikuwa hawajaingia katika ndoa bado.
Ikapita miezi kadhaa, yule kichaa Felista akabeba mimba mtaani, hakujulikana aliyembebesha mimba ile. Kilio kikazuka upya na watu wakaanza kujiuliza je? Tatizo alikuwa mumewe ama???
Nani angejibu iwapo mume ni marehemu na mke ni kichaa?? Yule aliyemjaza mimba pekee ndiye ajuaye na ule UKIMWI aliojiambukiza ndio utakaomuumbua...
MWISHO
NB: Toa maoni yako kuhusu simulizi hii, je umejifunza kitu?? sema lolote kumshauri mwandishi huyu....
Usisite KU SHARE yaweza kuwa funzo kwa wengine
إرسال تعليق