RIWAYA:ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA SABA
Yule mwenye kidoti akageuka, macho yao yakagongana. Waliachana umbali wa mita kadhaa.
“Betiiiiiiiiiii!!!!” Kidoti akapiga kelele ya nguvu na kubwa kupita zote alizowahi kupiga hapo kabla.
“Joyceeeee jamaniiiiiiii” mrembo mwingine aliyekaribia kuanguka baada ya kusukumwa akajibu kwa kupaza sauti iliyosindikizwa na mikwaruzo ya kutaka kulia…..
Kimya kikatanda kila aliyekuwa na shughulia akaiacha na kuwatazama wawili wale. Wakakimbilia na kukumbatiana kwa nguvu.
Ilistaajabisha, Kidoti akawa wa kwanza kupoteza fahamu kwa mshtuko kisha msichana asiyekuwa na jina naye akaanguka chini na kupoteza fahamu, naye pia kwa mshtuko na mengine yoyote yale ambayo atayasema yeye akizinduka. Mimi kama wewe tu sijui nini kilitokea.
Lakini kwa kuwa wewe haukuwepo basi tulia nitakuhadithia!!!!
Lakini wale mapacha wasitoka tumbo moja.
BETTY (Msichana asiye na jina) na JOYCE (Kidoti) walikuwq wamekutana tena……wote wakiwa hai….
Lakini kwa mara nyingine tena ni katika wajihi tofauti.
Wawili hawa hawakuhitaji kukimbizwa hospitali ili waweze kurejewa na fahamu. Baada tu ya kupungiwa upepo wa haja na marafiki pamoja na kumwagiwa maji kiasi fahamu ziliwarudia. Wakaachwa watulie kidogo na kumbukumbu zao zikawakaa sawasawa.
Hapa sasa hawakuhitaji kujibu swali lolote kutoka kwa mtu yeyote yule, walihitaji kupumzika. Lakini sio katika chumba cha hapo chuoni, Joyce Keto Kidoti alichukua taksi akamuamuru dereva akawapeleka maeneo ya River Side Ubungo, huko wakachukua chumba katika hoteli ya kisasa.
Usiku huu ukawa wa aina yake!!
Ulikuwa usiku ambao kila sentensi kutoka kwa aidha Joyce ama Betty ilichangamsha ubongo na kuulazimisha kufikiri kwa uyakinifu.
Zilikuwa ni kumbukumbu za miaka sita iliyopita. Kumbukumbu za Makambako, kumbukumbu zilizotatanisha haswa. Na kisha ukazuka mtihani wa aina yake!! Mtihani ulioufanya usiku huu kuwa wa kukumbukwa tena!!!
Mazungumzo ya awali kabisa Betty alimuuliza Joyce Keto, kisa cha kuwa amekasirika vile usiku ule na inakuwa vipi anakuwa na wapambe wengi vile.
******
WANAUME wanaume wanaume aaargh!!! Alianza kulalamika Joyce. Betty akawa msikilizaji.
Joyce alielezea juu ya kushiriki kwake mashindano ya urembo chuoni na kisha kuzua kizaazaa baada ya mshindi kutajwa mwingine wakati kila mmoja akitegemea kuwa Joyce Keto ama maarufu kama Kidoti atanyakua taji hilo. Mtafaruku huo ukampa jina kubwa pale chuoni, na akapata marafiki wengi japo sitakosea nikiwaita wapambe. Ni hawa waliokuwa kama walinzi wake, wakimfuata hovyo kila mahali. Huku wakijisahau kuwa wote ni wanafunzi tu wa pale chuoni.
Joyce akamaliza kwa ufupi kisha akahamia tukio la jioni ile.
Hili alilielezea kwa ghadhabu.
Kama ambavyo hakutegemea kuwa mpotezaji wa vitu vile kuwa katika hali ya majivuno na ulimbukeni ulo’kubuhu kiasi kile, basi nd’o ambavyo hakutegemea kuwa yatazuka mambo ya ziada.
Joyce alituliza akili yake wakati wale vijana wanne wanajongea katika kimbweta alichokuwa ameketi, aliwatazama kwa jicho la kuibiaibia akawaona jinsi walivyokusudia kuvuta macho ya watu kuwatazama.
“Karibuni.” Aliwakaribisha. Wakaketi wote baada ya kumpa salamu kwa kumshika mkono. Joyce alitamani kuwaomba watoke abaki na mmoja lakini aliona hilo kama haliwezekani, halafu mbaya zaidi walipofika na kumtambua ni yeye wakaongeza majisifu. Kijana aliyekuwa mbele yake kwa kudhamiria kabisa akalegeza vishikizo vya shati lake.
Ewalaa!! Mkufu wa dhahabu ukaonekana, laiti kama angekuwa msichana mwingine angeanza kuuvaa mkenge lakini Joyce Keto hakuwa msichana wa kawaida, huo aliuona ni ushamba. Akataka kusonya lakini akajikuta akiguna, akataka kuangalia kwa jicho baya lakini badala yake akajikuta akirembua jicho lake.
Joyce hakujua kuuvaa uhusika wa kukasirika, suluhu yake ni kuvimbisha mashavu kisha anatokwa machozi. Mwisho wa mchezo.
Joyce akapuuzia yote yaliyokuwa anaendelea. Akataka kuanza kujieleza jambo alilolifahamu, mara mmoja kati yao akatoa simu aina ya Nokia yenye kamera, ambayo kwa wakati ule ilikuwa katika chati. Hapa Joyce akashusha pumzi kwa nguvu bila kusema lolote.
‘Hivi wanadhani mimi wa bei rahisi hivyo!...pole yao maskini dah!’ aliwaza haya huku akijitahidi asizungumze kwa hasira.
Hatimaye walianza maongezi, Joyce akaanza kujieleza lakini akakatwa kauli na mmoja wao.
“Aaah! Sorry sister, yo know hatujafahamia bado walau majina something which is not good at all.” Mtumwa mmoja wa maisha ya kighaibuni akasema.
“Naitwa Joyce” akawahi kujitambulisha kwa karaha.
“Ben”
“Simon”
“George”
“Isaya” alimalizia mwanaume wa mwisho ambaye kama ni mashindano ya ujivuni alikuwa anaongoza, ni kweli alikuwa amependeza lakini ujivuni ulimfanya aonekane mpuuzi tena.
“Nafurahi kuwafahamu.” Alisema kwa kujilazimisha Joyce, kisha akaendelea na alichokusudia kuwaeleza, akawaelezea kwa pamoja ni kitu gani anafahamu kuhusu kompyuta iliyopotea, alishangazwa sana na umakini wao. Hawakuwa makini kabisa kumsikiliza alichokuwa akiwaeleza, labda kidogo Isaya alikuwa anasikiliza kitu japo naye kila mara alikwenda kupokea simu bila kuomba radhi.
“Basi ni hivyo nijuavyo, kama bado haijatoka nje ya chuo basi ni mtu huyo niliyemshuhudia akitoweka nayo maktaba.” Alimaliza.
Baada ya maswali mawili matatu yasiyokuwa na uzito ndipo wanaume hawa walipohamisha mada na kuibua mada iliyomkera waziwazi Joyce. Haikuwa mada mbaya, ilikuwa mada ya kuhusu mapenzi….na hapakuwa na ubaya mtu kuzungumza mapenzi, lakini walichofanya wanaume hawa ni kumtongoza kwa pamoja.
Walimfanya kama changudoa mzoefu. Mara huyu amwambie hivi mara yule aseme hiki. Kwa akili zao waliamini kuwa Joyce atazenguka na ufajari wao. Kitendo cha kutongozwa na wanaume wanne ilikuwa ni dharau iliyopitiliza kabisa. Dharau iso’kuwa stahiki yake. Ni hapa Joyce alipoamua kuwatumia ujumbe marafiki zake wa kike ambao ni mcharuko haswaa. Wakati anawatumia ujumbe walimjibu kuwa walikuwa mahali wanapata juisi, akawasihi waende alipo wakamweleza kuwa wanaenda huku wakimtumia ujumbe wa ziada kuwa wamekutana na pacha wake kwa urembo.
Walipofika wakatumia mbinu zao kumtoa Joyce katikati ya kundi lile, hapa ukazuka mtafaruku mwingine baada ya wanaume wale kudai kuwa kwa sababu rafiki zake Joy wametimia wanne na wao wapo wanne basi wagawane.
Hapa ukazuka mcharuko wa ajabu kutoka kwa rafiki zake Joy. Mcharuko ambao uliwafanya wafike hosteli huku wakitukana matusi yote wayajuayo na Joyce akiwa kimya tu.
Marafiki/wapambe hawa ni walewale wapashkuna na washakunaku waliokuwa wameketi jirani na Betty wakiujadili urembo wake huku wakiulinganisha na wa Kidoti Joyce Keto.
Ni huku walipokutana tena mapacha hawa na kubadilisha simulizi ya usiku ule!!!!
Joyce kidoti alimaliza ngwe ya kwanza ya simulizi. Betty alikuwa anatabasamu tu…
“Ila umekuwa mrembo sana Betty jamani…” alimsogelea rafiki yake na kuanza kujidekeza katika mapaja yake kama mtoto mdogo. Kisha akaanza kulia akimlalamikia kwa nini aliondoka bila kuaga.
“Yaani Betty jamani….nd’o ukaniacha pekee ukaniacha vile kweli Betty mimi mwenyewe huko….mi s’taki…..s’taki….” akazidi kudeka huku machozi mepesi yakimtoka. Betty akambembeleza huku akimfuta machozi, walikuwa wamekuwa wadada watu wazima lakini ule urafiki wao wa tangu utotoni uliwafanya waendelee kuwa watoto.
Betty aliifahamu tiba ya kumfanya Joyce atabasamu tena, baada ya kuonekana kuzidiwa na majonzi, na aliihitaji sana furaha yake ili na yeye aweze kumhadithia jambo zito.
Akasimama akimwacha Joy kitandani. Akasogea hadi katikati ya chumba. Joy alidhani anaenda uani, akajilaza kifudi fudi.
Mara…………………
“Ukutiii ukutiiiii……wa mnaziii…..wa mnaziiiiiiiiii……..mwenzetu….mw enzetu……..kagongwa ……kagongwa……na nini na nini….
Na gaaari na gaari……..”
Joyce akakurupuka kutoka kule kitandani, alikuwa na kanga iliyofunika kiguo kifupi cha kulalia, kanga ikaanguka hakujihangaisha kuiokota……akafika kwa fujo mahali alipokuwa Betty akiimba kipweke kabisa, akaunganisha mikono yao upesi kisha akendelea kwa sauti kuu yenye furaha..huku wakirukaruka.
“…Tumpeleke hosibitali asije kusema kwa mama yake….yesayesayesa yaaah…..bado kidogo….yeasayesayesa yaah!! Baaado kidogo ….yesayesayesa yaah!!”
Hakika Betty alikuwa amemkamata Joyce haswaa, waliruka ruka wakabadili kila aina ya nyimbo za utotoni na zile ambazo waliimba wakiwa wanakua. Furaha ikakipamba kile chumba.
Kisha kwa furaha wakakumbatiana huku wakilia, zile nyimbo ziliwakumbusha mbali. Enzi hizo Joyce ni mwembamba na kidoti chake kikiwa sio biashara hadimu. Betty naye akiwa ‘kimbaumbau’.
WAKATI wawili hawa wakikumbushia enzi zao kwa nyimbo za kitoto, upande mwingine wa maisha wanaume wanne ambao waliita kile kitendo cha Joyce kuondoka kinguvu na wale wasichana ambao ni rafiki zake kilikuwa ni utovu wa nidhamu. Wanaume wale waliamini hapakuwa na msichana hata mmoja ambaye ana uwezo wa kuwakatalia kimapenzi, walikuwa na kila kitu ambacho msichana wa wakati ule alikuwa anatamani kukifahamu aghalabu kama si kukipata kabisa.
“Mara ya mwisho mi kukataliwa na demu ilikuwa mwaka juzi, tena tulikuwa ikulu nd’o kitoto cha prezidaa kikanitolea nje, tena ni vile sikukaza uzi tu na alishajua kuwa nilikuwa natoka na mtoto wa waziri, hiki kishamba kutoka wapi nd’o kinisumbue. Sasa hapa naweka kando mambo yangu kwa muda. Lakini tupinge nawapa wiki mbili tu huyo Kidoti sijui nakuja kumtambulisha mbele yenu” alijiganba Isaya. Wale wanaume wengine wakapiga kelele za shangwe kumpamba Isaya.
Walizungumza mengi huku yule mtoto wa mbunge wa wilaya ya Geita (kwa sasa mkoa wa Geita) ambaye alionekana kudhamiria waziwazi kuhusiana na Joyce akiweka kiapo.
Safari zake za kwenda Marekani na uingereza mara mbili tatu akiambatana na mzee Akunaay Zingo ambaye ni baba yake mzazi na pia mbunge, zilikuwa zimempagawisha sana na kujikuta akitamani kuishi maisha ya kimagharibi katika nchi ya Tanzania.
Alijipa kiburi kuwa kwa safari zake hizo na pesa aliyokuwa nayo basi angeweza kufanya kila kitu na kila mtu akakubali.
Ni heri asingeweka kiapo kile maana alikuwa anajiingiza katika safari asiyoijua mwisho wake wala mwanzo wake!!!
Ni basi tu wanadamu hatukupewa jicho la kujua yatakayojiri wakati ujaoo…….
***
Kabla ya kulala Betty naye alisema machache kuhusu yeye.
“Joyce Kidoti.” Aliita kwa utani, Joyce akacheka.
“Najua una maswali mengi ya kutaka kuniuliza, lakini baadhi nayajibu katika maelezo yangu, kwanza unajiuliza Dar nipo tangu lini na nimekuja kwa nani….Joy mpendwa mguu huu kutoka huko nitokapo ni mguu wa kuja kwako wewe.” Akasita na kumtazama machoni rafiki yake.
“Nimekuja kwako wewe ukiwa ndugu yangu wa karibu sana na mwandani wa kuzifahamu siri zangu na matatizo yangu hata kama ni makubwa vipi. Nimekuja hapa nikihitaji msaada wa vitu viwili kwako, yaani vitu viwili tu! Na kama vikiongezeka nitakueleza…” Joy akamkatisha, “Betty hutakiwi kuhesabu kitu chochote kwangu Joy ni yuleyule na nitafanya kila kitu kwa ajili yako hata kama ni vitu elfu moja.” Alisema kwa hisia, Betty akaipokea kwa kutikisa kichwa juu na chini. Kisha akaendelea. “Kitu cha kwanza ni hifadhi, sina hifadhi katika jiji hili na kubwa zaidi ni mara yangu ya kwanza kufika jijini hapa. Kitu kingine ambacho nahitaji unisaidie ni kunitunzia siri yangu, Joyce Ukimwi ….ukimwi hauponi hata asikudanganye mtu, mimi na afya yangu yote hii bado unaishi nami ugonjwa huo mbaya.” Hapa Joyce akatikisa kichwa kwa masikitiko.
“Usiumie Joyce hiyo ilibidi itokee iuli wewe ufike hapa kisha urejee Ukala kama shujaa wangu, shujaa wa kijiji chetu. Na katika huo ushujaa ukilitaja jina langu kichwani mwako nitafarijika sana. Maana kitu ninachokiamini mimi katika vita hata wale ambao huteteketea na kupoteza uhai wao wakiligombania taifa na wao huitwa mashujaa pia. Hivyo mimi nimekufa katika harakati, ningeweza vipi kukuacha Joy uolewe…nigekuacha vipi uolewe na wale watu wazima ambao huenda wana Ukimwi wakakuambukize. Joy imekuwa heri punda afe mzigo ufike na sasa imekuwa heri Betty afe JHoyce akikomboe kisiwa cha Ukala, kisiwa kilichowameza wazazi wetu, kikawatafuna waalimu wetu kwa sababu ya kukosa huduma za kiafya. Kisiwa kilichosahaulika kabisa. Ni furaha yangu nimekukuta ukiwa hapa na utanieleza ulifikafika vipi hapo baadaye maana tupo pamoja tena…..Joy msaada huo wa kuitunza siri hiyo kwa upendo ni kwa manufaa yetu pia, najua mzigo wa kuipigania Ukala ni mkubwa sana, nilitamani tushirikiane kimasomo hadi huku lakini haikuwezekana, lakini nikaipata njia mbadala huko Lilongwe Malawi nilipokuwa naishi kwa kipindi kirefu. Nimekuja nikiwa na nia moja tu, nahitaji pesa. Pesa kwa ajili ya kijiji chetu, pesa kwa ajili ya maisha yetu. Mara ya kwanza nilivua nguo nikapata pesa, sasa ni mawili KISASI na PESA…wataumia hao walio na tamaa watambuao kuwa sisi ni vyombo vya starehe, na wataumizwa na tamaa zao, sitajiuza Joy sitamtega mwanaume kwa maksudi ili aninase lakini nasema OLE WAO wajilengeshe na kujifanya wanajua kupenda na wanayo pesa……moyo wangu umebakiza nafasi ndogo sana ya upendo, na huu ni kwa ajili yako tu Joy, sihitaji kumpenda mtu mwingine kabisa. Namaanisha ninayoyasema.
Nd’o maana nikahitaji hifadhi za aina mbili, kwanza mimi kama mimi kisha hifadhi na siri yangu hiyo nzito. Huku ukijua wazi ndugu yako sina upendo zaidi ya kwako wewe na nd’o maana ninakupa siri na mipango yangu ya sasa” alimaliza na kuweka kituo Betty kisha akamtazama tena Joyce. Joyce alikuwa ana wasiwasi mkubwa sana.
Alishangaza sana kumtazama.
****BETTY ndani ya jiji, hana urafiki wala huruma…..jilete akufyatue..
***JOYCE amebebeshwa siri hiyo…si alisema yupo tayari kwa lolote…HAPO VIPI??
***ISAYA na kiapo chake….atambeba JOYCE KIDOTI…
TOA MAONI YAKO KUHUSU RIWAYA HII…..
##ITAENDELEA
إرسال تعليق