Msemaji
wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Lt. Kanali Juma Sipe
akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Teknolojia mpya ya Ujenzi wa
nyumba zenye gharama nafuu (UBM) ambao ni mradi unaotekelezwa na SUMA
JKT, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa
Idara ya Habari Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ujenzi wa wizara hiyo
Bw. Nathan Alute.
Kamishna
Msaidizi wa Ujenzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bw.
Nathan Alute akitoa ufafanuzi Teknolojia mpya ya Ujenzi wa nyumba zenye
gharama nafuu(UBM), kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
leo ukumbi wa Idara ya Habari kulia ni Msemaji wa Wizara hiyo Lt. Kanali
Juma Sipe.
Meneja
Mradi wa UBM Raphael Bandiho (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa
Habari Kuhusu ubora wa nyumba zinazotokana na teknolojia hiyo, kwenye
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari
kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi
Kawawa.(PICHA ZOTE NA HASSAN SILAYO).
Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeanzisha matumizi ya teknolojia mpya
ya ujenzi ijulikanayo kama “Ultimate Building Machine (UBM)”,
inayowezesha ujenzi kufanyika haraka na katika hali yoyote ya maumbile
ya nchi.
Teknolojia
ya UBM ilianza kutumika nchini kwa majaribio katika kambi za Jeshi
Mgulani, Dar es Salaam. Hatimaye Wizara iliridhia teknolojia hiyo
kutumika katika ujenzi mkubwa wa Shule ya Mafunzo ya Awali, Kihangaiko
(Msata), Mkoani Pwani katika mwaka wa Fedha 2012/13. Pamoja na ufinyu
mkubwa wa fedha kutoka Serikalini, UBM imewezesha hatua kubwa kupigwa
katika ujenzi huo muhimu.
UBM ni
mtambo wa ujenzi unaotembezwa juu ya gari maalumu. Mtambo huu ambao
hutumia kompyuta unaweza kuendeshwa kwa urahisi na kwa ufanisi,
husafirishwa moja kwa moja hadi eneo la ujenzi kwa kutumia lori maalumu
au ndege ya mizigo ili kuwezesha ujenzi wa haraka wakati wa majanga.
Faida za
teknolojia ya UBM ni pamoja na kuwezesha ujenzi wa haraka (Rapidity)
kutokana na uwezo wa mtambo kutengeneza/ kuzalisha maumbo mbali mbali ya
mabati katika mitindo tofauti tofauti pale pale kwenye eneo la ujenzi,
urahisi na uharaka wa uunganishaji wa maumbo kiasi cha kuwezesha watu
10-12 kukamilisha jengo moja lenye futi za mraba 10,000 ndani ya siku
moja (endapo msingi wake uko tayari) na kupunguza muda wa ujenzi kwa
kuwa teknolojia hii haihitaji nguzo za kushikiza (columns), vishikio
(Screws, panels, beams, trusses, nuts, bolts, fasteners), misumari
(screws), wala gundi maalumu ya kuzuia kuvuja (sealants).
Faida
nyingine ni kupatikana kwa “thamani ya fedha” (Cost-Effectiveness) kwani
gharama za ujenzi ni kati ya asilimia 40 na 60 ya ujenzi wa kawaida au
teknolojia ya “prefabricated” kutokana na kupunguza idadi ya wajenzi na
usimamizi wa wahandisi wanaohitajika kwa teknolojia ya kawaida. Aidha,
teknolojia inarahisisha pia usafirishaji wa Mtambo na Vifaa kwani
matumizi ya “Galvanized, Pre-painted Steel Coil” yanapunguza hadi
asilimia 80 ya mahitaji ya vifaa.
Mjenzi
anaweza kunufaika pia na ujenzi wa maumbo mbali mbali (Flexible designs)
kutokana na mtambo wa UBM kuwa na uwezo wa kuzalisha maumbo mbali mbali
ya mabati katika mitindo tofauti tofauti kulingana na hitajio la mwenye
nyumba. Umbo, muonekano, kimo na upana wa jengo pia hutofautiana
kulingana na mahitaji, na bado jengo likabaki na uwezekano wa kupanuliwa
siku za usoni.
Majengo ya
teknolojia ya UBM yana faida pia ya maisha marefu na gharama ndogo za
matengenezo (Durable and Low Maintenance cost) kutokana na umadhubuti wa
mabati yanayotumika na uwezo wake wa kuhimili mikikimikiki ya kimbunga,
tetemeko la ardhi, moto na upepo mkali.
Tafiti
duniani zinaonesha kuwa teknologia ya UBM inakubalika kuwa ya kiwango
cha juu kiusalama kimataifa ikiwemo kukidhi viwango vya Jumuiya ya Ulaya
(European CE compliance). Teknolojia ya UBM imethibitika pia
kuwa si kwa ajili ya ujenzi wa haraka wakati wa majanga tu, bali inaweza
kulisaidia Taifa kukamilisha ujenzi wa aina mbali mbali kwa haraka na
kwa gharama nafuu ili kuleta manufaa haraka.
Kuridhia
kwa Serikali na Taasisi binafsi kutumia teknolojia hii kutaifanya UBM
kuwa mkombozi katika ujenzi wa maabara na mabweni mashuleni, ujenzi wa
maghala ya mazao katika maeneo mbali mbali ya uzalishaji nchini, pamoja
na aina yoyoye nyingine ya ujenzi wa haraka kwa kadri mmiliki wa jengo
atakavyohitaji na watakavyokubaliana na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na
JKT.
Teknolojia ya Ultimate Building Machine (UBM) iliyoasisiwa na Kampuni ya MIC Industries, Inc. ya nchini Marekani na baadae kuenea hadi barani Ulaya na Asia. SUMAJKT wamepewa dhamana ya kutumia teknolojia hiyo nchini.
Imeandaliwa na kutolewa na Luteni Kanali Juma Nkangaa Sipe,
Msemaji, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Post a Comment