Wizara yaanzisha matumizi ya Teknolojia ya UBM nchini.


IMG_1100

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Lt. Kanali Juma Sipe akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Teknolojia mpya ya Ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu (UBM) ambao ni mradi unaotekelezwa na SUMA JKT, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ujenzi wa wizara hiyo Bw. Nathan Alute.
IMG_1108
Kamishna Msaidizi wa Ujenzi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bw. Nathan Alute akitoa ufafanuzi Teknolojia mpya ya Ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu(UBM), kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kulia ni Msemaji wa Wizara hiyo Lt. Kanali Juma Sipe.
IMG_1110
Meneja Mradi wa UBM Raphael Bandiho (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari Kuhusu ubora wa nyumba zinazotokana na teknolojia hiyo, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo ukumbi wa Idara ya Habari kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.(PICHA ZOTE NA HASSAN SILAYO).
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeanzisha matumizi ya teknolojia mpya ya ujenzi ijulikanayo kama “Ultimate Building Machine (UBM)”, inayowezesha ujenzi kufanyika haraka na katika hali yoyote ya maumbile ya nchi.
Teknolojia ya UBM ilianza kutumika nchini kwa majaribio katika kambi za Jeshi Mgulani, Dar es Salaam. Hatimaye Wizara iliridhia teknolojia hiyo kutumika katika ujenzi mkubwa wa Shule ya Mafunzo ya Awali, Kihangaiko (Msata), Mkoani Pwani katika mwaka wa Fedha 2012/13. Pamoja na ufinyu mkubwa wa fedha kutoka Serikalini, UBM imewezesha hatua kubwa kupigwa katika ujenzi huo muhimu.
UBM ni mtambo wa ujenzi unaotembezwa juu ya gari maalumu. Mtambo huu ambao hutumia kompyuta unaweza kuendeshwa kwa urahisi na kwa ufanisi, husafirishwa moja kwa moja hadi eneo la ujenzi kwa kutumia lori maalumu au ndege ya mizigo ili kuwezesha ujenzi wa haraka wakati wa majanga.
Faida za teknolojia ya UBM ni pamoja na kuwezesha ujenzi wa haraka (Rapidity) kutokana na uwezo wa mtambo kutengeneza/ kuzalisha maumbo mbali mbali ya mabati katika mitindo tofauti tofauti pale pale kwenye eneo la ujenzi, urahisi na uharaka wa uunganishaji wa maumbo kiasi cha kuwezesha watu 10-12 kukamilisha jengo moja lenye futi za mraba 10,000 ndani ya siku moja (endapo msingi wake uko tayari) na kupunguza muda wa ujenzi kwa kuwa teknolojia hii haihitaji nguzo za kushikiza (columns), vishikio (Screws, panels, beams, trusses, nuts, bolts, fasteners), misumari (screws), wala gundi maalumu ya kuzuia kuvuja (sealants).
Faida nyingine ni kupatikana kwa “thamani ya fedha” (Cost-Effectiveness) kwani gharama za ujenzi ni kati ya asilimia 40 na 60 ya ujenzi wa kawaida au teknolojia ya “prefabricated” kutokana na kupunguza idadi ya wajenzi na usimamizi wa wahandisi wanaohitajika kwa teknolojia ya kawaida. Aidha, teknolojia inarahisisha pia usafirishaji wa Mtambo na Vifaa kwani matumizi ya “Galvanized, Pre-painted Steel Coil” yanapunguza hadi asilimia 80 ya mahitaji ya vifaa.
Mjenzi anaweza kunufaika pia na ujenzi wa maumbo mbali mbali (Flexible designs) kutokana na mtambo wa UBM kuwa na uwezo wa kuzalisha maumbo mbali mbali ya mabati katika mitindo tofauti tofauti kulingana na hitajio la mwenye nyumba. Umbo, muonekano, kimo na upana wa jengo pia hutofautiana kulingana na mahitaji, na bado jengo likabaki na uwezekano wa kupanuliwa siku za usoni.
Majengo ya teknolojia ya UBM yana faida pia ya maisha marefu na gharama ndogo za matengenezo (Durable and Low Maintenance cost) kutokana na umadhubuti wa mabati yanayotumika na uwezo wake wa kuhimili mikikimikiki ya kimbunga, tetemeko la ardhi, moto na upepo mkali.
Tafiti duniani zinaonesha kuwa teknologia ya UBM inakubalika kuwa ya kiwango cha juu kiusalama kimataifa ikiwemo kukidhi viwango vya Jumuiya ya Ulaya (European CE compliance). Teknolojia ya UBM imethibitika pia kuwa si kwa ajili ya ujenzi wa haraka wakati wa majanga tu, bali inaweza kulisaidia Taifa kukamilisha ujenzi wa aina mbali mbali kwa haraka na kwa gharama nafuu ili kuleta manufaa haraka.
Kuridhia kwa Serikali na Taasisi binafsi kutumia teknolojia hii kutaifanya UBM kuwa mkombozi katika ujenzi wa maabara na mabweni mashuleni, ujenzi wa maghala ya mazao katika maeneo mbali mbali ya uzalishaji nchini, pamoja na aina yoyoye nyingine ya ujenzi wa haraka kwa kadri mmiliki wa jengo atakavyohitaji na watakavyokubaliana na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi na JKT.
Teknolojia ya Ultimate Building Machine (UBM) iliyoasisiwa na Kampuni ya MIC Industries, Inc. ya nchini Marekani na baadae kuenea hadi barani Ulaya na Asia. SUMAJKT wamepewa dhamana ya kutumia teknolojia hiyo nchini.
Imeandaliwa na kutolewa na Luteni Kanali Juma Nkangaa Sipe,
Msemaji, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Post a Comment

أحدث أقدم