Zanzibar yaridhia masharti ya ubakaji


BARAZA la Mapinduzi Zanzibar limetoa uamuzi kuhusu suala la ubakaji kisiwani Zanzibar kwa kuyakubali masharti yaliotolewa na nchi za Maziwa Makuu katika mkutano wake uliofanyika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mwaka jana .

Maazimio hayo yaliyopitishwa na nchi hizo, yamekubaliwa na Baraza la Mapinduzi yakiwemo ya kuanzishwa kwa Mahakama maalumu ya kesi za udhalilishaji, kuzifanya kesi hizo kuwa ni kesi maalumu, kuipa madaraka Mahakama ya kufika katika tukio la udhalilishaji, kesi hizo kutozidi miezi sita na kila nchi kulaani jambo hilo kwa kutoa matangazo mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mawasiliano.


Hayo yalisemwa jana kwenye Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakari Khamis Bakari wakati alipokuwa akitoa majumuisho kwenye bajeti ya Wizara.

Bakari alisema kinachofuata baada ya uamuzi huo ni kwa wizara yake hivi sasa kuwa katika mchakato wa kuazisha sheria hiyo ambayo itafanyiwa kazi mara baada ya kupitishwa na kutiwa saini.

Alisema katika sheria hiyo mbali na hayo yatakayokuwemo pia ni pamoja na kumuweka kizuizini mtuhumiwa wa ubakaji hadi kesi hiyo imalizike, ili kuhofia kupoteza ushahidi. Lingine ni kufungwa miaka mingi mhusika wa ubakaji ili iwe fundisho na kukomesha suala hilo.

Masuala mengine yatakayokuwemo katika sheria hiyo ni kuorodhesha majina ya vyuo vyote vya Quran na kuvipa usajili, kwani inadaiwa baadhi ya walimu wa vyuo vya Quran nao ni sehemu ya ubakaji watoto wadogo.

Mengine ni kumuwekea kizuizi mtoto wakati atapokuwa akitoa ushahidi ili aaminike kwa vile atakuwa hana wasiwasi ya kile anachokizungumza akiwa hamuoni mtuhumiwa. Aidha alisema pia suala jingine ni kuwashajihisha masheha, wanajamii na wazazi ili kuwa sehemu ya ushahidi pamoja na kukitumia kifaa cha DNA kitakapokuwepo badaye.

Naye Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Watoto, Zainab Omar Mohamed akitoa majumuisho ya Wizara hiyo alisema alikuwa akisikitishwa sana juu ya uamuzi wa kesi hizo na kusema kwa vile sasa Wizara ya Sheria tayari inaandaa utaratibu mzuri kuna siku tatizo la udhalilishaji litakwisha.

--Habari Leo

Post a Comment

Previous Post Next Post