Wapiga kura waliojitokeza kumchagua Rais mpya wa Mali
REUTERS/Joe Penney
|
Na Flora Martin Mwano
Zoezi la kuhesabu Kura nchini Mali limeendelea baada ya kutamatika kwa
upigaji kura za Uraisi. Mamilioni ya wananchi walijitokeza kushiriki
zoezi hilo siku ya jumapili na kutupilia mbali vitisho vya uvunjifu wa
amani vilivyotolewa na kundi la wapiganaji wa eneo la kaskazini mwa nchi
hiyo MUJAO.
Waangalizi wa kimataifa wamesifu idadi kubwa ya wapiga kura
waliojitokeza huku kukiwa na ulinzi mkali katika vituo mbali mbali
nchini humo, kuanzia katika mji mkuu Bamako.
Mpaka asubuhi ya jumatatu hakukuwa na uvunjifu wa amani ulioripotiwa
kujitokeza dhidi ya wapiga kura wala wasimamizi wa zoezi hilo.
Raia wa Mali walitakiwa kumchagua raisi wao miongoni mwa wagombea 27
walioidhinishwa na tume ya uchaguzi na mshindi wa kinyang'anyiro hicho
ndiye atakayefanikisha uundwaji wa serikali ya muungano wa kitaifa.
Taarifa toka nchini humo zinadokeza kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Taifa
hilo Ibrahim Boubacar Keita anaongoza katika matokeo ya awali
yaliyokwishahesabiwa katika baadhi ya vituo.
Aidha Waziri Modibe Sidibe ambaye naye ni Waziri Mkuu wa zamani na
Soumaila Cisse ambaye ni Waziri wa zamani wa fedha wanaonyesha dalili za
kupata uungwaji mkono katika kura hizo.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa na wizara ya mambo ya ndani siku ya jumanne.
Endapo hakutakuwa na mgombea aliyeibuka na kura nyingi zaidi basi duru
la pili la uchaguzi huo litafanyika tarehe 11 ya mwezi Agosti na
kuwashirisha wagombea waliopata zaidi ya asilimia 50.
Chanzo - kiswahili.rfi.fr
إرسال تعليق