Askari polisi wa Manyoni mkoani Singida apandishwa kizimbani kwa tuhuma za kujaribu kuiba shilingi milioni 11.7.


mahakama
Na Nathaniel Limu
Askari polisi wilaya ya Manyoni mkoani Singida PC G.4121 Steven Sweya Peter (24) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida, akikabiliwa na tuhuma ya kutenda makosa mawili likiwemo la jaribio la kutaka kuiba zaidi ya shilingi milioni 11.7 mali ya mwajiri wake.
Mwendesha mashitaka Sajenti wa polisi Godwl Lawrance, amedai mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, kuwa mnamo Mei 30 mwaka huu kwa nyakati tofauti, mshitakiwa aligushi hati nne za malipo (pv) kwa lengo la kumwibia mwajiri wake jeshi la polisi zaidi ya shilingi 11.7 milioni.
Amesema mshitakiwa alitenda makosa hayo huku akijua wazi kwamba anatenda kinyume na sheria zilizowekwa.
Lawrance ametaja hati za malipo hayo kuwa ni Pv, E.010600, E.010589, E.010586 na E.010595, ambazo zilikuwa zilipwe kupitia akaunti 2011000015 iliyopo kwenye benki ya NMB tawi la Manyoni mjini.
Mshitakiwa amekana mashitaka yote na yupo nje kwa dhamana ya wadhamini watatu wenye mali isiyohamishika.
Kesi yake itatajwa tena agosti 15 mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoa wa Singida, zimedai kuwa polisi huyo kijana amekwisha fukuzwa kazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post