Bado kidogo mabilionea wa ‘cocaine’ watatuchagulia rais!


Makala Tafakuri Jadidi
Bado kidogo mabilionea wa ‘cocaine’ watatuchagulia rais!
Johnson Mbwambo Toleo la 310 7 Aug 2013
UKIACHA suala la ujio wa Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na kutunishiana misuli kwa Kikwete na Kagame, hakuna suala jingine, wiki iliyopita, lililotawala vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini kupita lile la kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya katika Tanzania.
Suala hilo lilianza kupamba moto baada ya mitandao ya kijamii kuweka habari za mbunge wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, kutuhumiwa kuhusika na biashara hiyo haramu ya kimataifa, na yeye mwenyewe kujipeleka polisi na kuipa changamoto imchunguze. Ni wiki hiyo hiyo ya jana tulielezwa pia kwamba, vijana wa Tanzania 176 wanatumikia vifungu huko China baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya.
Ripoti za wiki jana zinasema pia kuwa, vijana wa Kitanzania walioko kifungoni huko Brazil kwa kukamatwa na madawa hayo wanafikia 103. Tarakimu hizi zinatisha; maana kama katika nchi mbili tu (China na Brazil) vijana wa Tanzania waliofungwa kwa kukamatwa na madawa hayo ni 279, vipi kama ungefanyika utafiti kote duniani kujua idadi kamili ya Watanzania wanaotumikia vifungo kwa kukamatwa na madawa hayo?! Naamini kama ungefanyika utafiti huo, tarakimu ya mwisho ingetutisha mno sote, na ingethibitisha kile ambacho nilikiandika katika safu hii, toleo Na.138, mwaka 2010, kwamba Tanzania tuko katika hatari ya kufanana na Mexico – nchi inayosumbuliwa sana na tatizo la biashara ya madawa hayo.
Tatizo la kuongezeka kwa biashara hiyo katika Tanzania limelalamikiwa mno kwa muda mrefu na raia wema, lakini Serikali imeziba masikio. Nasema imeziba masikio kwa sababu hatua inazochukua hazilingani kabisa na ukubwa wa kilio cha raia hao wema. Angalau nakumbuka kwamba kuna Watanzania wawili raia wema walipata kujitokeza hadharani na kusema kwamba wana orodha ya vigogo wa biashara hiyo katika Tanzania (mmojawao – Amina Chifupa sasa ni marehemu), lakini Serikali haikuchukua hatua yoyote kupata orodha hiyo. Imeziba masikio.
Hata ile orodha ya vigogo 58 wa biashara hiyo aliyokabidhiwa Septemba 18, 2006 nayo hatujui imeishia wapi. Lakini jambo la kushangaza na lililotisha zaidi, ni pale Rais wetu mwenyewe, Jakaya Kikwete, Juni 5, 2011, akiwa Mbinga kwenye sherehe za kumsimika Askofu Ndimbo, alipoutangazia umma kwamba baadhi ya viongozi wa dini nchini ni washirika wakubwa wa biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya.
Kauli hiyo ilitushangaza wengi kwa sababu kama Rais anawajua viongozi wa dini wanaoshiriki katika biashara hiyo haramu, kwa nini haagizi wakamatwe na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake? Na hata baada ya viongozi wa dini walipojibu mapigo ya Kikwete kwa kumpa changamoto ya kutaja majina ya viongozi hao wa dini wanaoshiriki katika biashara hiyo, Rais aliloa na kuamua kukaa kimya mpaka leo! Hali hiyo iliibua maswali mengi ambayo mpaka leo hayajapata majibu: Je, Rais anawaogopa viongozi hao wa dini wanaoshiriki biashara hiyo? Je, mbali ya viongozi wa dini, yawezekana labda pia anawajua vigogo wengine wanaoshiriki biashara hiyo lakini nao hataki kuwachukulia hatua kwa sababu zile zile zinazomfanya asiwachukulie hatua viongozi hao wa dini? Na sababu zenyewe hizo ni zipi hasa?
Yawezekana hatutapata majibu ya maswali hayo, lakini ni mtazamo wangu kwamba Tanzania hatutafanikiwa kuishinda vita hii dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya kama Rais mwenyewe anaingia woga kuwachukulia hatua watu ambao anawafahamu wanahusika na biashara hiyo. Na ndiyo maana, binafsi, niliichukulia kwa wepesi mno kauli ile ya wiki iliyopita ya Kamanda wa Polisi Kikosi Maalumu cha Kupambana na Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, kwa gazeti la Nipashe, kwamba eti wanakosa vidhibiti vya kuwatia hatiani vigogo wa biashara hiyo haramu.
Kauli hiyo ya Nzowa ya ‘kukosa vidhibiti’ kwa namna fulani inafanana na ile iliyopata kutolewa na Rais Kikwete huko nyuma kwamba eti ni vigumu kuwakamata mafisadi papa nchini kwa kuwa ni wajanja! Vyovyote vile, kauli hiyo ya Kikwete na hiyo ya Nzowa vinathibitisha ni kwa nini hapa nchini wanaoendelea kukamatwa kwa ufisadi na kwa kuhusika na biashara hiyo ya madawa ya kulevya, ni ‘vijidagaa’ tu; huku ‘mijipapa’ ikiachiwa kuendelea kula maraha yanayotokana na uovu wao huo.
Nimesema awali kwamba kama ungefanyika utafiti kote duniani kujua ni vijana wangapi wa Kitanzania wanatumikia vifungo Ughaibuni kwa kukamatwa na madawa ya kulevya, idadi yake ingekuwa kubwa kuliko hao 279 waliofungwa China na Brazil. Lakini tujiulize: Mpaka sasa ni vigogo wangapi katika Tanzania wanaotumikia vifungo kwa kujihusisha na biashara hiyo haramu? Kama wapo, nina hakika hawafiki watatu au wanne. Kwa maneno mengine ni kwamba, vigogo wa Tanzania wanaotumia ‘njaa’ na ukosefu wa ajira wa vijana wetu kuwarubuni wawasafirishie madawa hayo huko China, Brazil, Afrika Kusini nk, bado wako huru hapa nchini wakiogelea kwenye utajiri wao; ilhali vijana hao wanasota magerezani Ughaibuni!
Ndugu zangu, hofu yangu ni kwamba kiasi tunavyochelewa kuwabana watawala wetu kuidhibiti kikweli kweli biashara hii, ndivyo pia Tanzania yetu inavyoelekea kuwa ‘Mexico nyingine’; kama nilivyoeleza katika makala yangu hiyo ya Juni 16, 2010. Niliandika katika makala hiyo kwamba Rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Felipe Calderon, ameishindwa vita hiyo kwa sababu taifa lilichelewa kuianza. Nina hakika hata huyu wa sasa, Enrique Pena Nieto, naye ataishindwa vita hiyo licha ya kusaidiwa mno na Marekani.
Na sababu ni ile ile ya kuchelewa kuianza vita hiyo. Nasi Tanzania tunaweza kuishindwa vita hii tukizidi kuchelewa kuianza; maana, kwa hakika, naweza kusema bila kupepesa macho kuwa hatujaianza kabisa vita hii kikweli kweli. Jambo muhimu kwa wasomaji wangu kufahamu ni kwamba huko Mexico biashara hiyo ilianza kidogo kidogo. Na ingawa umma ulipiga kelele ukisaidiwa na vyombo vya habari, lakini watawala waliziba masikio. Kidogo kidogo mashamba ya kulima mimea inayotengeneza madawa hayo ya kulevya (cocaine) yakaongezeka vijijini. Ikafikia hatua kikaanzishwa kikundi cha kiharamia cha kusimamia biashara hiyo haramu, lakini bado watawala waliendelea na upofu na ukiziwa wao. Na kwa sababu ya ukiziwa na upofu wao, sasa biashara hiyo Mexico imekuwa zimwi kubwa ambalo halikamatiki.
Kutoka katika kuwa na kikundi kimoja tu cha kiharamia kinachosimamia biashara hiyo, sasa Mexico ina vikundi (cartels) vikubwa visivyopungua sita. Baadhi ya vikundi hivyo vya kiharamia, kama kile kinachoitwa Sinaloa Cartel, kinachoongozwa na Joaquim “El Chapo” Guzman, kimefikia hata hatua ya kuwa na jeshi lake kwa ajili ya kupambana na vikundi vingine kugombea maeneo na ruti za biashara hiyo, na pia kwa ajili ya kupambana na polisi au vikosi vya serikali. Watawala wa Mexico walipozinduka na kuanza kupambana na biashara hiyo, wakakuta zimwi limeshakuwa kubwa. Hivi sasa, si tu kwamba vikundi hivyo vina majeshi yake, lakini pia vina mtandao mkubwa kiasi kwamba vimechomeka ‘watu wao’ ndani ya serikali – kuanzia kwenye polisi na majaji hadi kwenye wanasiasa na watawala serikalini. Kama Mexico, nasi Tanzania tumeanzisha Kikosi Maalumu cha Polisi cha Kupambana na Madawa ya Kulevya lakini hakuna dalili za mafanikio.
Kama Mexico, nasi tumefanya mabadiliko katika sheria zetu kadhaa ikiwemo ya utakatishaji pesa (money laundering) lakini hakuna mafanikio ya wazi yanayoonekana. Ni kwa nini vita hii inaelekea kutushinda Watanzania? Jibu ni kama lile lile la Mexico; nalo ni kwamba tumechelewa kujitosa katika uwanja wa mapambano, na sasa mtandao wa vigogo wanaojishughulisha na biashara hiyo umekuwa mkubwa mno kiasi kwamba hata Rais Kikwete mwenyewe sasa anaonyesha dalili za kuugopa!
Lakini ukweli mchungu ni kwamba tusipombana Rais Kikwete akajipa ujasiri wa kupambana na biashara hii, tunaweza kufanana kabisa na Mexico ambako mitandao ya vigogo wa biashara hiyo (drug lords) wamefikia hatua ya kuwa na wanajeshi wao, mapolisi wao, mahakimu wao, majaji wao, wabunge wao, mawaziri wao, madiwani wao, madaktari wao, watu wao katika vyama vya siasa nk – yaani kila mahali wana watu wao wa kuwalinda, na hata wana uwezo wa kuchomeka watu wao katika nafasi za uongozi wa juu serikalini! Tuombe Mungu tusifike huko; lakini tunavyoenenda, nina hofu miaka si mingi drug lords wetu katika Tanzania watakuwa na mtandao mkubwa wenye mabilionea kibao unaoweza hata kumfadhili mtu wao akagombea urais, na akashinda! Bado kidogo tu hayo yatatokea Tanzania!
Tafakari. 

Post a Comment

Previous Post Next Post