Sheikh Azzan Khalid Hamdan
|
Na Mwiny Sadallah
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji, amesema hakuna tatizo kwa
kiongozi mwandamizi wa Uamsho, Sheikh Azzan Khalid Hamdan, kutibiwa nje
ya nchi kama jopo la madaktari litapitisha uamuzi huo.
Akizungumza na Mwananchi Ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar juzi, Duni
alisema kwa mujibu wa katiba, mwananchi yeyote ana haki ya kutibiwa nje
ya nchi kwa maradhi ambayo tiba yake haipatikani nchini.
Alisema hata hivyo hatua hiyo itategemea uwezo wa Serikali kifedha na ukubwa wa ugonjwa.
“Bado sijapokea ripoti kuhusu Sheikh Azzan, wajibu wangu ninapopokea
nalazimika kupeleka Hazina, hakuna ombi hata moja nililowahi
kulitupa,”alisema waziri.
Alisema daktari anayemtibu sheikh huyo, anapaswa kuwasilisha ripoti ya
mgonjwa katika Bodi ya Matibabu ya Nje ambayo ndiyo yenye uamuzi wa
mwisho kulingana na ukubwa wa ugonjwa.
Alisema ingawa Sheikh Azzan ni mshtakiwa, hicho hakiwezi kuwa kigezo cha kukosa kutibiwa nje.
Kiongozi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmmoja mjini Zanzibar
akisumbuliwa na maradhi ya figo kuwa na vijiwe na anapaswa kupelekwa nje
ya nchi kwa matibabu.
Katibu wa hospitali hiyo, Omar Abdallah Ali alisema kwa utaratibu Bodi
ya Matibabu ya Nje inakutana kila baada ya miezi miwili kufanya uamuzi
kuhusu wagonjwa wanaotakiwa kutibiwa nje ya nchi.
Alipia pia inaweza kukutana kwa dharura pale panapokuwa na mgonjwa anayehitaji uharaka wa matibabu.
Kiongozi huyo wa uamsho anakabiliwa na mashtaka ya kufanya uchochezi na kusababisha uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment