Kuhamia dijiti kwaipaisha Tanzania.


Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy akielezea ukuaji wa teknolojia nchini, wakati wa semina ya wafanyakazi katika vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao 
Na Julius Mathias, Mwananchi
.
Tanzania inasherehekea Siku ya Mawasiliano Duniani, huku ikijivunia mafanikio ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kuhama kwa mafanikio kutoka mfumo wa analoji kwenda dijiti.
Siku hii inaadhimishwa tangu mwaka 1983 baada ya kupendekezwa na aliyekuwa Rais wa Marekani, John Kennedy ili kutambua haki za watumiaji na wadau mbalimbali wa mawasiliano kote duniani, ambao walipendekeza Tarehe 15 Machi ya kila mwaka.
Katika baadhi ya nchi kama Kenya na Afrika Kusini, mawasiliano ni miongoni mwa haki za binadamu inayotambuliwa katika katiba za nchi hizo. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wadau wengine wapo katika harakati za kuhakikisha suala hili linaingizwa katika katiba mpya ijayo.
Akizungumzumza katika semina na waandishi wa habari iliyofanyika jana katika ukumbi wake wa mikutano, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema sekta ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali za uchumi kama kilimo, biashara, huduma za fedha, afya na hata usafirishaji.
“Matumizi ya simu hivi sasa ni ya lazima kwa watu wengi na siyo anasa, kwani zinawezesha upatikanaji wa huduma nyingi mahali mteja alipo bila kumtaka kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” alisema Profesa Nkoma.
Kuna ongezeko kubwa la matumizi ya simu miongoni mwa Watanzania, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 1994 kulikuwa na watumiaji wa simu wapatao laki moja, lakini kutokana na rekodi za laini zilizosajiliwa idadi hiyo imepanda na kufikia 28 milioni.
Ongezeko hili la simu hasa za mkononi limekuja na kushamiri kwa vitendo vya uhalifu kwa njia ya mtandao ikijumuisha makosa binafsi, kifedha na hata udhalilishaji
Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Watumiaji, Isaac Mruma alionya juu ya matumizi ya simu zinazopatikana kwa njia isiyo rasmi kuwa zina madhara ya kisheria kwa mtumiaji mpya iwapo kuna uhalifu kuhusu laini hiyo.
“Usitumie simu ya kuokota na ikitokea ukaokota ipeleke polisi kwa usalama wako binafsi, ili kuepuka mkono wa sheria kwani mmiliki anaweza akapatwa na jambo lolote baya kama kuuawa nawe ukahusishwa kutokana na simu hiyo ya marehemu,” alisema.
- mwananchi-

Post a Comment

Previous Post Next Post