Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent
Mungy akielezea ukuaji wa teknolojia nchini, wakati wa semina ya
wafanyakazi katika vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na
Salim Shao
Na Julius Mathias, Mwananchi
.
.
Tanzania inasherehekea Siku ya Mawasiliano
Duniani, huku ikijivunia mafanikio ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kuhama
kwa mafanikio kutoka mfumo wa analoji kwenda dijiti.
Siku hii inaadhimishwa tangu mwaka 1983 baada ya
kupendekezwa na aliyekuwa Rais wa Marekani, John Kennedy ili kutambua
haki za watumiaji na wadau mbalimbali wa mawasiliano kote duniani, ambao
walipendekeza Tarehe 15 Machi ya kila mwaka.
Katika baadhi ya nchi kama Kenya na Afrika Kusini,
mawasiliano ni miongoni mwa haki za binadamu inayotambuliwa katika
katiba za nchi hizo. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wadau
wengine wapo katika harakati za kuhakikisha suala hili linaingizwa
katika katiba mpya ijayo.
Akizungumzumza katika semina na waandishi wa
habari iliyofanyika jana katika ukumbi wake wa mikutano, Mkurugenzi Mkuu
wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema sekta ya mawasiliano ina mchango
mkubwa katika nyanja mbalimbali za uchumi kama kilimo, biashara, huduma
za fedha, afya na hata usafirishaji.
“Matumizi ya simu hivi sasa ni ya lazima kwa watu
wengi na siyo anasa, kwani zinawezesha upatikanaji wa huduma nyingi
mahali mteja alipo bila kumtaka kuhama kutoka sehemu moja kwenda
nyingine,” alisema Profesa Nkoma.
Kuna ongezeko kubwa la matumizi ya simu miongoni
mwa Watanzania, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 1994 kulikuwa na
watumiaji wa simu wapatao laki moja, lakini kutokana na rekodi za laini
zilizosajiliwa idadi hiyo imepanda na kufikia 28 milioni.
Ongezeko hili la simu hasa za mkononi limekuja na
kushamiri kwa vitendo vya uhalifu kwa njia ya mtandao ikijumuisha makosa
binafsi, kifedha na hata udhalilishaji
Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Watumiaji, Isaac
Mruma alionya juu ya matumizi ya simu zinazopatikana kwa njia isiyo
rasmi kuwa zina madhara ya kisheria kwa mtumiaji mpya iwapo kuna uhalifu
kuhusu laini hiyo.
“Usitumie simu ya kuokota na ikitokea ukaokota
ipeleke polisi kwa usalama wako binafsi, ili kuepuka mkono wa sheria
kwani mmiliki anaweza akapatwa na jambo lolote baya kama kuuawa nawe
ukahusishwa kutokana na simu hiyo ya marehemu,” alisema.
- mwananchi-
- mwananchi-

إرسال تعليق