Liverpool inaweza kupata Ubingwa msimu huu - Gerrard

Gerrard:Liverpool inaweza kupata Ubingwa msimu huu.
Nahodha wa Liverpool,Steven Gerrard anaamini kuwa ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Manchester United kwenye uwanja wa Old Trafford umeleta matumaini zaidi ya kushinda taji la ligi kuu ya Uingereza.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 alifunga penati mbili na kukosa ya tatu wakati Nemanja Vidic alipotolewa nje kabla ya Luis Suarez kufunga kwenye dakika sita kabla ya mpira kuisha.
Ushindi huo ulifanya kikosi hicho cha Brendan Rodgers kupanda mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya Chelsea kwa pointi nne lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi huku ratiba ikionesha michezo dhidi ya Manchester City na vinara hao bado itapigwa Anfield.
Liverpool hawajapoteza mchezo wowote wa ligi tangu kuingia kwa mwaka 2014 wakishinda michezo nane kati ya 10 na wanamatumaini makubwa sana ya kutwaa taji la kwanza la ligi kuu ya Uingereza katika kipindi cha miaka 24.
Katika hatua kama hii msimu uliopita,Man United walikuwa pointi 29 mbele ya Liverpool.Na sasa wapo mbele kwa pointi 14 dhidi ya mashetani wekundu hao na Gerrard anaamini hii inatokana na jinsi walivyojiandaa vizuri na kujituma kwa nguvu zaidi.
Nyota huyo alisisitiza kuwa,”Nafikiri tumeonyesha leo(Jumapili) kuwa sisi ni wapinzani wakubwa na tunaenda kupambana mpaka tuone mwisho wake.”
Na akaongeza kuwa amecheza katika dimba la Old Trafford kwa miaka mingi na ni timu bora huku akikiri kuwa sehemu hiyo ni ngumu zaidi kucheza vizuri na kumudu mchezo mwanzo mpaka mwsiho na kuibuka na ushindi.
Pia akaongelea kuhusu penati zake na kusema kuwa,”Nilikuwa imara na mwenye kujiamini sana lakini katika penati ya tatu sikuhisi kama ntakosa ila penati ya pili niliifurahia zaidi.”
Gerrard alidai kuwa wanachoangalia sasa ni kujitahidi kushinda mchezo unaofuatia dhidi ya Cardiff City kama walivofanya kwa Man United na baadae kufanya hivyo tena dhidi ya Sunderland na michezo mingine ili waweze kuwa katika hali nzuri zaidi katika mbio zao za Ubingwa.
Licha ya nahodha huyo wa timu ya Taifa ya England kipindi cha nyuma kuwahi kukataa kabisa kuhusu Liverpool kuwania taji la ligi huku akisema wanatazamia kupata tiketi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya alithibitisha kuwa kwasasa wana uwezo wa kufanya hivyo na watajitahidi kuendelea kufanya vizuri.

Post a Comment

أحدث أقدم