
MWANAFUNZI aliyehitimu Darasa la Saba
mwaka jana, jina tunalo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu wa Wilaya
ya Nkasi mkoani Rukwa, kwa madai ya kumuoa msichana waliyekuwa wakisoma
naye darasa moja mwenye umri wa miaka 15.
Binti huyo alifanikiwa kupata nafasi ya
kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Chala wilayani Nkasi, lakini
ameshindwa kujiunga kwa kuwa ni mke wa mtu. Wawili hao walikuwa wakisoma
Shule ya Msingi Kacheche kijijini Kacheche wilayani Nkasi .
Mshitakiwa ambaye kwa sasa ni mkulima
katika kijiji cha Kacheche alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya
Hakimu wa mahakama hiyo, Ibrahim Mgalamalira ambapo alikana shtaka hilo.
Mtuhumiwa alidai kuwa anafahamu kuwa amemaliza elimu ya msingi, lakini
hakuwa na taarifa kama alikuwa amechaguliwa kujiunga na elimu ya
sekondari mapema mwaka huu.
Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa
alimuoa msichana huyo, Februari 24, mwaka huu na kuishi naye nyumba moja
kijijini Kacheche kama mume na mke kwa siku sita hadi alipotiwa nguvuni
Machi 3, mwaka huu.
"Msichana huyu bado ni mwanafunzi kwa
kuwa alichaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari
Chala wilayani hapa lakini ameshindwa kuendelea na masomo kwa kuwa
alikuwa ameolewa na mtuhumiwa ambaye sasa amemkatisha masomo yake,"
alidai mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa
alipohojiwa kwa mara ya kwanza kabla ya kufikishwa mahakamani hapo,
alikiri kumuoa msichana huyo kwa kuwa alifahamu kuwa ameshamaliza darasa
la saba mwaka jana.
Hakimu Mgalamalira aliamuru mshtakiwa
arudishwe rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo
alimtaka awe na wadhamini wawili wenye mali zisizoweza kuhamishika
zenye thamani isiyopungua Sh milioni moja. Shauri hilo limeahirishwa
hadi Machi 26, mwaka huu litakapotajwa tena.
>>>Habari leo
إرسال تعليق