Edinson Cavani |
UHAMISHO unaofanywa na wanasoka kwa kuhamia klabu zenye upinzani mkubwa, wakati mwingine huwa utata mkubwa katika viwango vyao.
Miongoni mwa uhamisho kama huo ni wa wachezaji
Luis Figo, aliyehama kutoka Barcelona na kwenda kujiunga na Real Madrid
au Sol Campbell alipohama Tottenham Hotspur na kutimkia Arsenal.
Kwenye Ligi Kuu England, uhamisho wa siku za hivi
karibuni uliotingisha ni wa Robin van Persie na Juan Mata, waliozihama
klabu zao na kuhamia Manchester United, licha ya kwamba timu zao zina
ushindani mkubwa na miamba hiyo ya Old Trafford.
Van Persie alihama kutoka Arsenal na Mata alihama
kutoka Chelsea na wote wamejiunga na Man United. Mashabiki wa timu zao
za awali, mara nyingi wamekuwa wakiwaona wachezaji hao kuwa ni
wasaliti.
Mbaya zaidi kwa wachezaji wanaofanya uhamisho kama
huo, ni kwamba mara nyingi wanakuwa hawaendi kufurahia maisha kwenye
timu mpya tofauti na ilivyokuwa kwenye klabu zao za awali.
Kwa mantiki huyo, kuhamia kwenye klabu pinzani
siku zote ni kama mchezo wa kamari, huna uhakika wa kwenda kufanya
vizuri huku ukifahamika wazi kwamba mashabiki kutoka kwenye timu
uliyoihama daima watakuwa wapinzani wako.
Makala hii inawazungumzia wanasoka mastaa ambao
wamehama kutoka kwenye timu walizozichezea kwa muda mrefu hadi kujiwekea
heshima kubwa na kuhamia timu nyingine na matokeo yake wamekutana na
nyakati ngumu tofauti na matarajio yao. Lazima watakuwa wanajutia uamuzi
wao.
Fowadi huyo wa Uruguay alijengea jina kubwa
klabuni Napoli kabla ya kutimkia Paris Saint-Germain. Uhamisho wake
ulikuwa wa pesa nyingi hasa kutokana na kiwango cha soka lake alilokuwa
akicheza Napoli, lakini tangu alipotua PSG mambo yamekuwa tofauti na
matarajio.
Staa huyo kwa siku za hivi karibuni amekuwa
hakosekani kwenye vichwa vya habari vya magazeti kila kukicha kwamba
anataka kuihama PSG baada ya kuona maisha yamekuwa magumu kwenye Ligi
Kuu Ufaransa.
Kitu kimoja kikubwa, alipokuwa Napoli, Cavani
alihesabika kama staa wa klabu hiyo, lakini kwenye kikosi cha PSG,
amekutana na Zlatan Ibrahimovic ambaye amejenga jina lake katika klabu
hiyo ya Paris.
Jambo hilo linakwenda sambamba na Cavani kushindwa kuchezeshwa
kwenye nafasi anayotaka ya straika wa kati kwa sababu nafasi hiyo
anapewa Ibrahimovic. Cavani alihama kwa ushawishi wa pesa na sasa
ametambua kuwa pesa hazina maana tena na ndiyo maana anataka kuhama.
Stevan Jovetic
Kwenye timu ya Fiorentina, usingeweza kutaka
kikosi cha kwanza cha timu hiyo na kisha ukaliweka kando jina la Stevan
Jovetic. Lakini, habari imekuwa tofauti sana baada ya kutua Manchester
City. Jovetic alikuwa na furaha sana kwenye maisha yake nchini Italia na
hivyo aliondoka kwenye klabu ya Fiorentina mwaka jana na kuhamia Man
City akiwa na matumaini ya kwenda kufanya kweli kwenye Ligi Kuu England.
Kwa bahati mbaya kocha, Manuel Pellegrini, amemwona hana jipya na matokeo yake amemfanya kuwa chaguo la nne kwenye safu ya washambuliaji nyuma ya Sergio Aguero, Alvaro Negredo na
Edin Dzeko.
Kutokana na hilo, Jovetic ameingia kwenye orodha
ya wachezaji wanaojutia kuhama kwenye timu ambazo walikuwa wakiabudiwa
kama miungo watu na kwenda kwenye timu ambazo wanaonekana kuwa wa
kawaida sana.
Kitu pekee anachofurahia staa huyo ni kupokea
mshahara mnono, ambao kama mwanasoka amekuwa haufanyii kazi kwa sababu
muda mwingi amekuwa akisugua benchi.
Erik Lamela
Hayakuwa matarajio kabisa. Erik Lamela wakati
anahama AS Roma na kutimkia White Hart Lane, kulikuwa na ahadi nyingi
kwamba Tottenham Hotspur ingebadilika na kuwa hatari sana kwenye Ligi
Kuu England.
Kwa bahati mbaya, kocha aliyemsajili, Andre
Villas-Boas, alitimuliwa. Sasa Lamela ameshindwa kabisa kuonyesha cheche
zake alizokuwa akizionyesha kwenye Ligi Kuu Italia.
Staa huyo wa kutoka Argentina, alisajiliwa kwa ada
ya Pauni 30 milioni na ameshindwa kuonyesha thamani halisi ya pesa
iliyotumika kwenye usajili wake.
Mbaya zaidi amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kuwa
majeruhi mara kwa mara, kitu kinachomfanya kushindwa kutimiza malengo
huku akijiona kuwa uhamisho wake umekuwa mikosi tu, afadhali angebaki AS
Roma.
Cesc Fabregas
Ni wazi kabisa, Cesc Fabregas, angeonekana kuwa ni mjinga mkubwa kama angegomea nafasi ya kusajiliwa tena na Barcelona mwaka 2011. Nyota huyo alianzia maisha yake ya soka kwenye akademia ya klabu hiyo ya Catalan kabla ya kuhamia Arsenal, ambapo alijenga jina lake na kuwa staa mkubwa wa kikosi hicho ikiwamo kupewa unahodha.
Barcelona ilikuwa kwenye ubora mkubwa duniani,
hivyo isingekuwa rahisi kwa mchezaji yeyote kugoma kujiunga nayo kama
walikuwa wakimhitaji. Hilo lilimkuta Fabregas na aliamua kutimkia
Barcelona na kuupa kisogo umaarufu wake wote aliokuwa nao Arsenal kwa
kipindi hicho.
Hata hivyo alipotua Nou Camp tu, akaanza kukutana
na kikwazo cha kupata namba kutokana na klabu hiyo kuwa na watu wao
kwenye kiungo. Aliwakuta; Andres Iniesta, Xavi na Sergio Busquets ambao
wanaonekana kuwa na ushirikiano mzuri.
Maisha yalianza kubadilika kwa kasi kwa Fabregas
na kupoteza umaarufu wake tofauti na alivyokuwa kwenye Ligi Kuu England,
ambapo alikuwa akitajwa kuwa moja ya wachezaji mahiri kabisa kwenye
ligi hiyo.
Kwenye La Liga, Fabregas haonekani kuwa kama
mchezaji makini ukiweka kando kwenye kikosi cha Barcelona peke yake.
Fabregas anaonekana kuwa ni mchezaji wa kawaida sana. Ni kama hakuwahi
kuwa nahodha wa klabu kubwa kabisa nchini England.
Juan Mata
Wakati kocha, Jose Mourinho, alipomruhusu Juan
Mata kuondoka Stamford Bridge Januari mwaka huu kwenda Man United,
jambo hilo liliwashangaza sana mashabiki kama ilivyokuwa kwa makocha wa
timu nyingine pamoja na vyombo vya habari.
Si tu kwamba Mata alikuwa mchezaji bora wa Chelsea
kwa misimu miwili mfululizo, bali ni kiungo mwenye ujuzi mkubwa sana wa
kuuchezea mpira na kutengeneza nafasi uwanjani.
Kuhamia Man United kunatajwa kuwa pigo kwa Mata
kwa sababu kwa kipaji chake, atashindwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya
msimu ujao kutokana na nafasi ya timu yake mpya kwenye Ligi Kuu England
kwa sasa.
Mata anashuhudia timu yake mpya ikikomea kwenye
robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huku klabu yake ya zamani wa
Chelsea ikiendelea kutesa kwenye michuano hiyo kwa kutinga nusu fainali.
Kuhitaji kucheza Kombe la Dunia nchini Brazil
mwaka huu ndicho kitu kinachotajwa kumshawishi Mata kuhamia Man United
kwa sababu Chelsea hakuwa hana namba na kuendelea kubaki kwenye klabu
hiyo kungevuruga zaidi nafasi yake kwenye kikosi cha Hispania
kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Fernando Torres
Staa huyo hahitaji maelezo mengi. Kila kitu kimejiweka bayana
kwamba uhamisho wake wa pesa nyingi kwenye kikosi cha Chelsea umekuwa
mbaya.
Fernando Torres alikuwa kwenye ubora mkubwa
klabuni Liverpool na kwamba alikuwa na heshima mahali hapo, lakini kila
kitu kimetibuka baada ya kuhamia Chelsea.
Torres amekuwa si tishio tena kwa mabeki wa timu
pinzani tangu alipotua Stamford Bridge mwaka 2011. Straika huyo
aliyewahi kuwa tishio kwenye kikosi cha Atletico Madrid, ameshindwa
kurejesha makali yake ya zamani baada ya kutua Chelsea licha ya kwamba
amekutana na makocha wengi wenye hadhi klabuni humo.
Robin van Persie
Sawa, Robin van Persie, ametimiza dhamira yake ya
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuhama kutoka Arsenal na
kwenda Manchester United. Lakini, uhamisho huo si kitu ambacho
kilitarajiwa kutokea mwanzoni.
Baada ya msimu mmoja kutesa, msimu uliofuata kocha
Sir Alex Ferguson alistaafu ukocha Old Trafford na hapo Van Persie
akaanza kupotea na kulalamikia mafunzo ya kocha mpya, David Moyes.
Kutokana na hilo, staa huyo msimu huu anahusishwa
na mpango wa kurudi Arsenal na ripoti za kila siku zinazotawala mwenye
vyombo vya habari ni kwamba Mdachi huyo hana furaha tena ya kubaki Old
Trafford.
Neymar
Kwa sifa kubwa alizozipata akiwa bado na umri
mdogo kabisa katika kikosi cha Santos, siku zote kilikuwa ni kitu
kinachotarajiwa kwa staa wa Brazil, Neymar kwamba angehamia kwenye soka
la Ulaya. Hilo lilitimia baada ya mchezaji huyo kuhamia Barcelona kwa
pesa nyingi, huku klabu nyingine kama za Real Madrid na Chelsea nazo
zikiwa zimesikitika kwa kuikosa saini yake.
Hata hivyo, Barcelona ambayo amekwenda kujiunga
nayo si ile iliyokuwa chini ya kocha Pep Guardiola. Hii ya sasa imeshuka
kiwango na Neymar anaonekana kuwa mzigo tu licha ya kwamba alipokuwa
Santos alionekana kuwa mmoja wa mastaa wenye viwango vya maana duniani
na kulinganishwa na wakali kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Kiukweli kwenye soka la klabu, Neymar atakuwa
anatamani kuzirudisha zama zake za klabuni Santos, ambapo alikuwa
akitajwa kuwa staa wa kikosi hicho tofauti na ilivyo kwa sasa Barcelona,
mahali ambapo Messi ana jina kubwa na timu hiyo inaundwa kwa kumtegemea
Muargentina huyo.
Post a Comment