Kaduguda atoboa siri ya Simba kuboronga .

KATIBU Mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda, amesema udhaifu wa viongozi waliopo madarakani chini ya Mwenyekiti, Ismail Aden Rage, ndiyo uliosababisha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne, kwani haukutazama athari za kuwatumia makocha wanne ndani ya misimu miwili tu.
Timu hiyo imemaliza ligi hiyo na pointi 38 huku Azam FC ikiwa mabingwa wa ligi hiyo ikivuna pointi 62, Yanga 56 wakati Mbeya City iliyopanda daraja kwenye msimu huu wakiwa na 47.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaduguda alisema kitendo cha viongozi hao kubadili makocha wanne ndani ya misimu miwili ya ligi kuu 2012-2013 na 2013-2014 ndiyo kumechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kuyumba.
Alisema msimu wa 2012-2013 timu hiyo ilifundishwa na makocha wawili wote wa kimataifa ambao wamefundisha mzunguko mmoja mmoja ambao ni Mserbia, Milovan Cirkovic na baadaye Mfaransa, Patrick Liewig.
Aliongeza kuwa katika msimu wa 2013-2014 timu na Abdallah Kibadeni aliyesaidiana na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kabla ya Zdravko Logarusic kupewa kazi.
“Makocha wote hao, hakuna hata mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kufundisha na aliyeipa mafanikio yoyote Simba, huo ni upungufu wa kiuongozi, hivyo wanachama wawe makini sana katika uchaguzi ujao, wasifanye makosa kama hayo,” alisema.
- mwanasport

Post a Comment

Previous Post Next Post