CHACHA KUCHEZESHA
MICHUANO YA AYG
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) limeteua mwamuzi msaidizi wa Tanzania anayetambuliwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ferdinand Chacha ameteuliwa
kuchezesha michezo ya Vijana ya Afrika (AYG- African Youth Games).
Michezo hiyo ya kwanza ya
Afrika itachezesha jijini Gaborone, Botswana kuanzia Mei 22-31 mwaka huu.
Tanzania pia itashiriki katika mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya
miaka 15.
SIMBA, ASHANTI UTD
KUVAANA TAIFA
Michuano ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho(Aprili 12 mwaka
huu) katika raundi ya 25 ambapo Simba na Ashanti United zitapambana Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi nyingine zitakuwa kati
ya Tanzania Prisons na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini
Mbeya) wakati Coastal Union itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
Keshokutwa (Aprili 13
mwaka huu) kutakuwa na mechi nyingine nne za kukamilisha raundi hiyo. Uwanja wa
Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya
wenyeji Oljoro JKT na Yanga.
Mtibwa Sugar itacheza na
Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Mgambo Shooting na Kagera Sugar
zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mbeya City
ikiumana na Azam kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI
YATAMBULISHWA BUNGENI
Timu ya Watoto wa Mitaani
ya Tanzania iliyotwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani nchini Brazil baada
ya kuifunga Burundi mabao 3-1 kwenye fainali imetambulishwa leo (Aprili 11
mwaka huu) katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
National Team Main Sponsor
Baadaye timu hiyo leo itapata chakula cha mchana na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda. Saa 10 jioni itatembeza
kombe hilo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma katika gari za wazi.
Jioni imeandaliwa hafla maalumu ya chakula pamoja na burudani
hapo hapo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Post a Comment